|
Mkutano wa baraza kuu la awamu ya 62 la Umoja wa Mataifa ulifunguliwa mjini New York alasiri ya tarehe 18 mwezi Septemba, wajumbe wa nchi mbalimbali wanashiriki kwenye mkutano mkuu wa baraza hilo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na kujadili masuala wanayofuatilia. Ikilinganishwa na mikutano ya miaka iliyopita, umaalumu wa mkutano wa mwaka huu ni kuwa, kwanza washiriki wa mwaka huu ni wa ngazi ya juu zaidi, pili, mikutano mingi ya ngazi ya juu ya pande nyingi itafanyika nje ya mkutano mkuu.
Habari zinasema wawakilishi wa zaidi ya nusu ya idadi ya nchi wanachama ni wakuu wa nchi au wakuu wa serikali, wakiwemo marais wa nchi 76, mawaziri wakuu 32 na makamu wa marais 14, hivyo mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka huu ni mkutano unaohudhuruiwa na wawakilishi wa ngazi ya juu zaidi tangu mkutano wa wakuu wa nchi wa mwaka 2005 wa kuadhimisha miaka 60 tangu Umoja wa Mataifa uanzishwe. Wakuu hao wa nchi na serikali watatumia nafasi ya kushiriki kwenye mkutano mkuu wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, kufanya majadiliano ya pande nyingi. Wanafikiria kuwa wakuu wa nchi au serikali kushiriki kwenye mkutano wanazingatiwa zaidi, jambo ambalo linachangia kupatikana kwa mafanikio halisi.
Sababu nyingine inahusiana sana na kazi muhimu za katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon. Tangu ashike wadhifa huo mwanzoni mwa mwaka huu, alihimiza utatuzi wa masuala mengi muhimu, akitumia shughuli za kidiplomasia za pande nyingi. Kutokana na pendekezo lake, itafanyika mikutano mingi ya ngazi ya juu katika muda wa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ikiwemo mkutano wa pili wa ngazi ya juu kuhusu suala la Darfur la Sudan na mkutano wa mabadiliko ya hali ya hewa. Aidha katika muda huo itafanyika mikutano mingi kuhusu masuala ya Iraq, Afghanistan, mashariki ya kati, Afrika na Kosovo.
Uwe mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka huu, au mikutano mbalimbali ya ngazi ya juu ya pande nyingi itakayofanyika katika muda wa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa, mikutano hiyo inaweza kugawanyika kuwa ya aina mbili, yaani masuala nyeti ya duniani na suala la Umoja wa Mataifa, ambalo ni kuhusu mageuzi yake. Mada 160 zilizowekwa kwenye ajenda ya mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ni kuhusu masuala ya maeneo 9 yakiwa ni pamoja na ya amani na usalama, maendeleo, haki za binadamu, upunguzaji wa silaha, kupambana na ugaidi na mageuzi ya usimamizi. Mwenyekiti mpya wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa Bw. Srgjan Kerim atatoa kipaumbele katika mambo ya maeneo matano ya mabadiliko ya hali ya hewa, uchangishaji fedha za maendeleo, lengo la maendeleo ya milenia, ubunifu wa makubaliano ya kupambana na ugaidi kwa pande zote na mageuzi ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Anatarajia kupata maendeleo halisi katika maeneo hayo katika muda wa mwaka mmoja atakaokuwa mwenyekiti wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kutokana na jitihada za baraza la Umoja wa Mataifa.
Lakini watu wana maoni tofauti kuhusu kufanyika kwa mikutano mingi ya ngazi ya juu ya kimataifa. Baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa huenda mikutano mingi ya ngazi ya juu itapunguza umuhimu wa mkutano wa baraza kuu; Lakini baadhi ya watu wengine wanaona, kuongezeka kwa mikutano ya ngazi ya juu kunaonesha pande mbalimbali kuzingatia nafasi hiyo ya pande nyingi ya Umoja wa Mataifa. Katika hali, ambayo masuala ya kawaida yanachanganywa na masuala nyeti, kufanyika mikutano ya ngazi ya juu ya pande nyingi kunachangia utatuzi wa masuala hayo, pia kunaonesha umaalumu wa Umoja wa Mataifa wa kutatua masuala ya kimataifa katika ngazi mbalimbali na kwa njia mbalimbali.
Suala lingine linalofuatiliwa na watu ni suala la ombi la Taiwan kujiunga na Umoja wa Mataifa. Huu ni mwaka ambao nchi zenye uhusiano wa kidiplomasia na Taiwan zimewasilisha kwa mara ya 15 mswada wa Taiwan kujiunga na Umoja wa Mataifa, ambayo ni mara ya kwanza kutaka kujiunga na Umoja wa Mataifa kwa Taiwan kwa kutumia jina la Taiwan. Mswada huo utajadiliwa tarehe 19 kwenye mkutano wa kamati ya shughuli za Umoja wa Mataifa, lakini mswada huo utapingwa kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita.
|