|
Baraza la usalama la Israel lilipiga kura tarehe 19 mwezi Septemba kuamua kuichukulia Hamas inayodhibiti ukanda wa Gaza hivi sasa kuwa adui yao, na kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya ukanda wa Gaza. Hayo ni matokeo ya watu wenye silaha wa ukanda wa Gaza kushambulia Israel kwa makombora mara kwa mara. .
Habari zinasema watu wenye silaha wa ukanda wa Gaza wamekuwa wanaishambulia miji ya sehemu ya kusini mwa Israel kwa makombora zaidi ya elfu moja, na kusababisha watu kumi kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa katika miaka 7 iliyopita. Kutokana na vitendo hivyo, Israel ilichukua hatua za kushambulia kwa ndege, kuteketeza sehemu maalumu, kufunga mpaka na kuweka vikwazo vya biashara, lakini hatua hizo hazikuwa na mafanikio. Tarehe 11 mwezi Septemba kituo cha kijeshi cha Zikim kilichoko kwenye sehemu ya kusini mwa Israel kilishambuliwa tena kwa makombora, ambapo askari zaidi ya 60 wa Israel walijeruhiwa, jambo hilo lilifanya serikali ya Bw Ehud Olmert ikabiliwe na shinikizo kubwa la nchini humo. Katika hali ya kama hiyo, baraza la usalama la Israel lilipitisha uamuzi wa kuuchukulia ukanda wa Gaza kuwa sehemu ya kiadui. Uamuzi huo inairuhusu Israel kuweka vikwazo vikali zaidi vikiwemo kupunguza utoaji umeme na nishati katika hali ya kutokiuka sheria za kimataifa. Lakini wachambuzi wanasema, uamuzi huo unakabiliwa na changamoto kutoka pande mbalimbali.
Kwanza ni changamoto inayoletwa na sheria ya kimataifa.
Ingawa Israel ilisema itazingatia suala la kibinadamu wakati inapoweka vikwazo kwenye ukanda wa Gaza, itahakikisha mahitaji ya lazima ya kibinadamu yakiwa ni pamoja na maji, chakula na matibabu, lakini ofisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa alisema, uwekaji wa vikwazo hivyo ni kwenda kinyume kabisa na sheria ya kimataifa. Ingawa jeshi la Israel liliondoka kutoka ukanda wa Gaza miaka miwili iliyopita, lakini hivi sasa bado linadhibiti mpaka, anga na bahari ya Gaza, na bado linawajibika kuhakikisha mahitaji ya lazima katika maisha ya wakazi wa sehemu hiyo. Hatua za uwekaji vikwazo zitaweza tu kuzidisha hali mbaya ya sehemu ya Gaza, na kufanya wakazi wa kawaida wa huko kupata adhabu isiyo ya haki. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon, alitoa taarifa siku hiyo ikifuatilia uamuzi huo wa serikali ya Israel, na kutaka serikali ya Israel ifikirie upya uamuzi wake huo.
Pili, ni kuwa Hamas si rahisi kutii kwa mbinu ya shinikizo. Israel inaona kuwa ingawa Hamas haikuwa mshiriki wa moja kwa moja katika mashambulizi mengi ya makombora, lakini haikuchukua hatua za kuyazuia mashambulizi hayo. Maofisa wa Israel wanatarajia kuwa kuweka vikwazo kutailazimisha Hamas kutekeleza majukumu yake. Waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Ehud Barak alisema, lengo la kuweka vikwazo ni kudhoofisha nguvu ya Hamas. Kuhusu maneno hayo, msemaji wa Hamas Bw. Faqzi Barhoum alisema, uamuzi wa Israel ni kama kutangaza vita, na ni kitendo cha kigaidi dhidi ya wapalestina.
Tatu, ni kitendo kisicho mwafaka kuhusu mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel, na kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa mwezi Novemba kuhusu suala la mashariki ya kati. Jambo linalotakiwa kutiliwa maanani, ni kuwa uamuzi huo ulitolewa baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice kufanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Israel. Wachambuzi wanasema, wapalestina wengi na vyombo vya habari vinamshutumu Bw. Abbas kwa kuzitegemea sana Israel na nchi za magharibi, na kumtaka achukue msimamo mkali katika mazungumzo ya baadaye.
Nne, uamuzi huo haukupendwa na wanasiasa wa pande zote mbili wa nchini. Chama cha Shas cha mrengo wa kulia kinaona, uamuzi umechelewa sana kutolewa, kinasema hayo ni kutokana na kusitasita kwa serikali ya Bw Olmert. Chama cha Meretz cha mrengo wa kushoto kinasema, hapo mwanzoni serikali ya Olmert ilipata nafasi ya utawala kutokana na ahadi ya amani aliyoitoa kwa wananchi, lakini hivi sasa inataka kutangaza vita. Wanaona kuwa uamuzi huo wa baraza la usalama la Israel ni wa kijinga na hatari, utazidisha mapambano ya kimabavu na kuharibu sura ya Israel.
|