Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-21 15:24:23    
Ziara ya pili ya Condoleezza Rice nchini Palestina na Israel haikupata matokeo yaliyotarajiwa

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice tarehe 20 amemaliza ziara yake nchini Palestina na Israel. Hii ni ziara yake ya sita mwaka huu kwenye nchi hizo. Shughuli za ziara ya Condoleezza Rice zilikuwa nyingi, tarehe 19 mchana alifika Jerusalem na tarehe 20 alasiri aliondoka. Katika muda huo mfupi alifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Israel Bi. Tzipi Livni, naibu waziri mkuu wa Israel Bw. Haim Ramon, waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Ehud Barak, waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert, na waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Palestina Bw. Salam Fayyad na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas. Mbali na shughuli hizo, pia alifanya mikutano mingi na waandishi wa habari. Baada ya ziara yake, vyombo vya habari vinaona kuwa ziara yake hiyo haikuwa na maana kubwa, ila tu alisema machache kuonesha msimamo wake alipozungumza na waandishi wa habari.

Kwanza, alikwepa tofauti za kimsingi zilizokuwepo katika mazungumzo ya amani. Inafahamika kwa wote kwamba, pande mbili za Palestina na Israel zilikubali pendekezo la Marekani la kufanya mkutano wa kimataifa mwezi Novemba kuhusu suala la Mashariki ya Kati, na viongozi wa pande mbili walifanya mazungumzo mara kadhaa.

Lakini tofauti kubwa zimetokea kati ya pande mbili kuhusu malengo yanayotakiwa kufikiwa kwenye mkutano huo. Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert anashikilia mkutano ufikie lengo la kutoa taarifa ya kimsingi, lakini Bw. Abbas anataka mkutano utoe taarifa yenye maelezo wazi ya mambo na kuweka ratiba kuhusu utatuzi wa migogoro ya mipaka, hatma ya Jerusalem na kurudishwa kwa wakimbizi.

Bi Condoleezza Rice alikwepa tofauti hizo katika ziara yake. Alisema kutilia mkazo kuhusu taarifa hiyo ambayo ni ya kimsingi au ya maelezo wazi ya mambo kutaleta umakini tofauti wa pande mbili kuhusu mkutano huo. Kitu muhimu ni kwamba pande mbili zinapaswa kuendelea kufanya juhudi na kujitahidi kupata mswada mmoja kabla ya mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Mashariki ya Kati, na bila kujali mswada huo utakuwa namna gani, ni lazima uwe msingi wa mazungumzo kuhusu suala la kujenga nchi ya Palestina. Msimamo huo wa Condoleezza Rice usio wazi haukuwa na msaada wowote katika kupunguza tofauti kati ya Palestina na Israel.

Pili, Bi Rice hakujibu suala linalofuatiliwa na nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati. Hivi sasa imebaki miezi miwili tu kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Mashariki ya Kati. Lakini hadi sasa ratiba ya mkutano, nani atahudhuria kwenye mkutano huo na mkutano huo utafanyika tarehe ngapi, yote hayo bado hayajaamuliwa. Mkutano kama huo unatiwa wasiwasi kama unaweza kusukuma mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, na hilo ndilo suala ambalo linazitia wasiwasi na nchi za Misri, Saudi Arabia na nchi nyingine za Kiarabu. Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Saud al-Faisal alionya kuwa kama mkutano huo hautajadili mambo halisi, Saudi Arabia haitashiriki kwenye mkutano. Rais Hosni Mubarak wa Misri ana wasiwasi kuwa, mkutano huo hautafanikiwa kutokana na kutokuwa na maandalizi ya kutosha. Baada ya kukutana na Bw Abbas, Condoleezza Rice alisema mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Mashariki ya Kati ni lazima uwe na mambo halisi, na kusema mkutano huo unapaswa usaidie ujenzi wa nchi ya Palestina. Lakini maneno hayo ni kama maneno matupu, nchi za Kiarabu za Mashariki ya Kati haziyaelewi vilivyo.

Ukweli ni kwamba Condoleezza Rice mwenyewe hana uhakika kama tofauti kati ya Palestina na Israel zinaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo hayo. Kwa hiyo anaweza tu kusema, "Kuna matatizo mengi katika maandalizi ya mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Mashariki ya Kati." Ni wazi kwamba ziara yake hiyo ya Palestina na Israel haikufikia matarajio ya kuondoa tofauti kati ya Palestina na Israel na kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Mashariki ya Kati kama watu wanavyotarajia.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-21