Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-24 15:27:07    
Mbinu 36: Kutoa tofali ili kupata jade

cri

"Kutoa tofali ili kupata jade" ni usemi wa Kichina unaotumiwa na Wachina mara kwa mara. Kutokana na maneno ya usemi huo ni rahisi kuelewa maana yake, kwamba wewe unatoa tofali ili kumfanya mwingine atoe jade, yaani jiwe lenye thamani kubwa. Wachina wana tabia ya kuwa wanyenyekevu, wao hutumia usemi huo hadharani kuonesha maoni yao ni ya kawaida kabisa, na kutaka yaliyo ya busara na mazuri yatokee. Kwenye mkutano kabla ya wengine kusema, mtu fulani hutangulia kusema, "Niseme machache kama ni kichochezi cha mazungumzo."

Usemi wa "kutoa tofali ili kupata jade" ulianza karne ya 9 wakati wa Enzi ya Tang nchini China. Enzi ya Tang ni kipindi ambacho shughuli za utungaji mashairi zilikuwa zimepamba moto, wasomi walikuwa wanashindana kwa mashairi, ingawa hawakufahamiana lakini waliweza kuwa marafiki mara moja walipoandikiana mashairi. Kulikuwa na mshairi mmoja aliyeitwa Chang Jian, aliposikia kwamba mshairi mwingine mkubwa aliyeitwa Zhao Gu atakwenda kutembelea hekalu la Lingyinsi la mji wa Suzhou, alikuwa na hamu kubwa ya kumtaka aandike mashairi. Ili kumchochea aandike mashairi Chang Jian alifika mapema kwenye hekalu na kwenye ukuta aliandika beti mbili za shairi. Shairi la kale nchini China huwa na beti nne, lakini Chang Jian aliandika beti mbili tu kwa makusudi. Baadaye Zhao Gu alifika kwenye hekalu, alipoona beti mbili za shairi mara alipata msukumo akaandika beti mbili nyingine kukamilisha shairi, na beti mbili hizo zilikuwa nzuri sana kupita zile beti mbili za mwanzo. Njia aliyotumia Chang Jian wasomi wa baadaye waliita "kutoa tofali, ili kupata jade".

"Kutoa tofali ili kupata jade" pia ni moja kati ya mbinu 36 za kivita. Katika mambo ya kivita, "tofali" inamaanisha kutoa faida kidogo au ushawishi mdogo, na "jade" ni mawindo unayotumai kupata. Katika vita vya kale mbinu za kuwadanganya maadui zilikuwa nyingi. Kitu muhimu cha kutumia "mbinu ya kutoa tofali, ili kupata jade" ni kufahamu vya kutosha hali ya maadui. Ufuatao ni mfano wa matumizi ya mbinu hiyo katika vita vya kale nchini China.

Miaka 700 K.K. kilikuwa ni kipindi cha vita kati ya madola kadhaa nchini China ili kupanua maeneo ya utawala. Jeshi la dola la Chu lilifanya mashambulizi dhidi ya mji wa Jiaocheng, ingawa jeshi la Chu lilikuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko jeshi lililolinda mji wa Jiaocheng, lakini kutokana na kuwa mji huo ulikuwa kwenye sehemu iliyokuwa rahisi kujikinga, jeshi la Chu halikuweza kuuteka kwa muda mrefu. Kutokana na hali hiyo, mawaziri wa dola la Chu walifafanua mazingira ya mapambano, waliona kuwa mji huo ulizingirwa kwa zaidi ya mwezi mmoja, mjini humo hakika kulikuwa na ukosefu wa kuni. Mawaziri hao walimshauri mfalme mbinu yao. Kwa mbinu ya mawaziri hao mfalme alituma askari wachache waliojifanya kuwa wanatafuta kuni, na kila siku walipanda mlimani kukata kuni. Wakati huo jeshi la kulinda mji lilikuwa likikumbwa na ukosefu wa kuni za kupikia chakula, lilipoona watu wakitafuta kuni mlimani, liliona ni fursa nzuri ya kupata kuni, basi lilituma askari wachache kwenda kunyang'anya kuni. Jeshi la kulinda mji lilifanya hivyo kwa siku kadhaa na jeshi la Chu lilijidai kama halijali. Kwa kuona hakuna hatari yoyote, jeshi la kulinda mji lilipunguza tahadhari bila kufahamu kuwa wakati huo jeshi la Chu lilikuwa tayari limeweka mtego. Siku moja jeshi la kulinda mji lilituma askari wengi kwenda mlimani kunyang'anya kuni, watu wa Chu waliokuwa wanatafuta kuni walijidai kuwakimbia, askari wa kulinda mji waliwafukuza, na bila kufahamu waliingia kwenye sehemu ya mtego, watema kuni wakatupa kuni zao, askari wa kulinda mji walifurahi na kukusanya kuni. Wakati huo ghafla kelele za "ua!" zilirindima, askari wa jeshi la Chu waliwavamia na kuwaua askari wa kulinda mji. Kutokana na ukosefu wa askari ndani ya mji, jeshi la Chu liliuteka mji huo kirahisi.

Katika zama hizi, mbinu ya "kutoa tofali ili kupata jade" pia inatumika mara kwa mara. Kwa mfano baadhi ya waigizaji filamu wanataka kujitangaza ili wajulikane zaidi, kwa makusudi wanatoa habari kuhusu maisha yao binafsi kupitia vyombo vya habari na baadaye habari hizo zinaenea kwa kuchapishwa kwenye magazeti na kuwavutia watu.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-24