|
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Russia na Marekani tarehe 23 Septemba zilikuwa na mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi kamili wa mgogoro kati ya Palestina na Israel. Kwenye mazungumzo hayo, wawakilishi wa pande hizo nne ambazo zinasimamia utaratibu wa amani ya Mashariki ya Kati walisikiliza ripoti ya kwanza kuhusu hali ya Mashariki ya Kati iliyowasilishwa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Bw. Tony Blair, ambaye aliteuliwa kuwa mjumbe mpya wa suala la Mashariki ya Kati wa Umoja wa Mataifa mwezi Julai mwaka huu. Bw Blair ameitembelea sehemu hiyo mara mbili baada ya kuteuliwa kuchukua nafasi hiyo. Imefahamika kuwa mazungumzo hayo pia yalifanya maandalizi kwa ajili ya mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Palestina na Israel, uliopendekezwa kufanyika baadaye mwaka huu na rais George Bush wa Marekani.
Taarifa iliyotolewa na pande hizo nne baada ya mazungmzo hayo inasema, hivi sasa hali ya wasiwasi inaendelea kuwepo katika sehemu ya Gaza, ambapo Israel inaendelea na vizuizi kwenye vituo mbalimbali vya kuingia Gaza, na mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel yanatokea mara kwa mara huko Gaza. Taarifa hiyo pia inasema, kuendelea kuwapa Wapalestina misaada ya dharura ni jambo muhimu sana katika kuepusha hali iwe mbaya zaidi.
Taarifa hiyo pia inaeleza kuunga mkono pendekezo la rais George Bush wa Marekani la kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Palestina na Israel baadaye mwaka huu. Mkutano huo unaotazamiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu, utahudhuriwa na wawakilishi wa Palestina na Israel pamoja na pande nne zinazosimamia suala la Mashariki ya Kati, vile vile nchi 11 za kiarabu ikiwemo Syria zitahudhuria mkutano huo. Taarifa hiyo inatumai kuwa, mkutano huo utaweka bayana kuunga mkono pande mbili za Palestina na Israel ziache matumizi ya nguvu, kuanzisha mazungumzo kwa msingi wa kuwepo kwa nchi mbili, na hatimaye kufanikisha kuanzishwa kwa nchi ya Palestina ambayo itaishi kwa amani na Israel. Taarifa pia inataka Bw. Tony Blair na mamlaka ya utawala wa Palestina zifanye juhudi za pamoja, ili kutunga mpango wa kuhimiza maendeleo ya siasa na uchumi wa Palestina katika muda wa kati na mrefu. Taarifa hiyo inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa itoe misaada kwa ajili ya hayo.
Kabla ya kufanyika kwa mazungumzo hayo, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Lynn Pascoe alipojulisha hali ya Mashariki ya Kati, alitoa tahadhari kuwa hivi sasa sehemu hiyo inakabiliwa na hali mbaya, kiasi kwamba mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel unapaswa kuanzishwa tena mara moja. Alinukuu takwimu za benki ya dunia zikionesha kuwa, pato la wastani kwa mpalestina limeshuka hadi dola za kimarekani 1,129 kwa mwaka kutoka dola za kimarekani 1,612 kwa mwaka 1999, hali ya kuugua magonjwa mbalimbali ya nyemelezi imeongezeka kwa theluthi moja, asilimia 10 ya watoto wa Palestina wasiozidi umri wa miaka mitano wanasumbuliwa na utapiamlo, na uchumi wa Gaza unazidi kutegemea misaada ya kimataifa. Aidha mapigano kati ya makundi mawili ya Palestina, Hamas na Fatah yanaendelea na kusababisha vifo na majeruhi.
Kuhusu uamuzi uliotolewa wiki iliyopita na serikali ya Israel wa kukatisha huduma za mafuta, maji na umeme kwa sehemu ya Gaza, Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa hatua hiyo inakwenda kinyume na sheria za kimataifa na sheria ya ubinadamu ya kimataifa, na haifai kuwaadhibu watu milioni 1.4 wasio na hatia kwenye sehemu ya Gaza kutokana na vitendo vya watu wachache wenye siasa kali. Na Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Israel ifikirie tena matokeo mabaya yatakayoweza kusababishwa na hatua hiyo. Bw. Pascoe aliona mambo yatakayotokea katika miezi kadhaa ijayo, ni muhimu sana katika kuepusha hali ya Mashariki ya Kati isizidi kuwa mbaya. Kutokana na hali hiyo, juhudi mpya za kidiplomasia zinazofanywa na jumuiya ya kimataifa zikiwemo pande nne zinazosimamia suala la Mashariki ya Kati zina umuhimu mkubwa.
Habari kuhusu maandalizi ya michezo ya Olimpiki 0611
Watu elfu 40 wamejitokeza kutoa huduma kwenye michezo ya Olimpiki maalumu itakayofunguliwa tarehe 2 Oktoba huko Shanghai, mji wa mashariki mwa China. Michezo hiyo iliyoanzishwa kwa ajili ya watu wenye mtindio wa ubongo, mwaka huu itawashirikisha wachezaji wapatao elfu 7 kutoka nchi na sehemu zaidi ya 160 duniani. Kati ya watu wanaojitolea elfu 40, asilimia 66 ni wanafunzi wa vyuo vikuu, na watu 108 wanatoka nchi za nje wanaoishi mjini Shanghai pia wamejiunga na kundi la kujitolea kutoa huduma kwenye michezo hiyo.
Tarehe 22 Septemba harakati za kuadhimisha siku ya kutotumia magari zilifanyika kwa mara ya kwanza katika miji 108 nchini China, ikiwemo miji mikubwa kama vile Beijing, Shanghai, Tianjin na Chongqing. Katika siku hiyo, wakazi wa miji hiyo walihamasishwa kutembea kwa miguu au kutumia baiskeli au vyombo vya usafiri vya umma, badala ya kutumia magari yao binafsi. Vile vile viongozi wa miji hiyo walitoa mfano wa kutotumia magari, na serikali katika miji hiyo kila moja ilitangaza hatua zaidi ya moja ya kuboresha usafiri wa umma.
Wajumbe wa sekta za michezo na afya kutoka nchi 10 za Asia walikutana hapa Beijing, wakijadili suala la kinga ya ugonjwa wa ukimwi kwa kupitia michezo. Hivi sasa watu zaidi ya laki 4 duniani wameathirika na virusi vya ukimwi, wakiwemo wachezaji na mashabiki wa michezo. Kutokana na hali hiyo, kamati ya Olimpiki ya kimataifa imeamua kujikita kwenye kampeni ya kuzuia kuenea kwa ukimwi. Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw. Jacques Rogge kwenye salamu zake kwenye mkutano huo amesema, "michezo inaweza kutumika katika kuboresha maisha na kuwanufaisha binadamu, kwani ni wazi kwamba kuzuia ukimwi na kupambana na unyenyepa ni sehemu mbili muhimu kwenye shughuli za michezo, na michezo inaweza kuondoa hali ya kutengana na kujenga hali ya kujiheshimu, pia inaweza kuwaelimisha watu namna ya kuishi na kujenga afya." Hivi sasa wachezaji wawili maarufu kutoka China wameteuliwa kuwa mabalozi wa kinga za ukimwi, ambao ni Bibi Deng Yaping, mchezaji mstaafu wa mpira wa meza aliyetwaa medali nne za dhahabu za Olimpiki na Bw. Yao Ming ambaye ni mchezaji wa mpira wa kikapu.
Hapa mjini Beijing, familia zimehamasishwa kutekeleza hatua za kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani na kubana matumizi ya nishati. Wito huu umetolewa a Shirikisho la wanawake la China. Kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, shirikisho hilo limeanzisha shughuli za kueneza ujuzi kuhusu afya na uhifadhi wa mazingira miongoni mwa wazazi na watoto wao, kuwahamasisha wahiari kufanya mazoezi ya kujenga mwili, na kubana matumizi ya nishati katika maisha ya kila siku.
|