Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-25 19:40:57    
Viongozi wa nchi mbalimbali wakusanyika kwenye Umoja wa Mataifa kujadili suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani

cri

Mkutano wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani ulifunguliwa tarehe 24 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa yaliyopo mjini New York. Kwenye ufunguzi wa mkutano huo katibu mkuu wa Umoja huo Bw. Ban Ki-moon alizitaka nchi zilizoendelea ziwe mfano katika juhudi za kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani.

Lengo la mkutano huo ni kuzipatia nchi mbalimbali nafasi za kubadilishana maoni, ili kuandaa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika mwezi Desemba mwaka huu katika kisiwa cha Bali, nchini Indonesia. Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 150 wameshiriki kwenye mkutano huo, kati ya wajumbe hao kuna viongozi waandamizi wa nchi zaidi ya 80. Mkutano huo umepanga kuwa na mijadala minne ikiwa ni mabadiliko ya hali ya hewa, kupunguza utoaji wa hewa chafu, matumizi ya teknolojia na ukusanyaji wa fedha.

Kwenye ufunguzi wa mkutano huo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Bw. Ban Ki-moon alisema, Umoja wa Mataifa unakubaliwa na nchi zote kuwa ni jukwaa linalofaa kushauriana kuhusu namna ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, lakini watu wengi akiwemo yeye mwenyewe wamekata tamaa na majadiliano hayo ambayo yanasuasua. Alisema mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa yana maana ya kuwa nchi zilizoendelea ziwe mfano wa kupunguza utoaji wa hewa chafu; nchi zinazoendelea zinatakiwa zichukue hatua ambazo hazitaathiri kukua kwa uchumi na jihudi za kuondoa umaskini; kuongoeza kwa kiasi kikubwa nguvu za kusaidia nchi zinazoendelea; kuendeleza teknolojia na kuongeza msaada wa kifedha. Bw. Ban Ki-moon aliongeza kuwa nchi moja peke yake haiwezi kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, bali ni lazima kujenga ushirikiano wa kimataifa wa ngazi ya juu kabisa duniani na kupata mafanikio makubwa, kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa duniani, jumuiya ya kimataifa inaona kuwa hili ni suala linalotokana na nchi zilizoendelea kutoa hewa chafu kwa miaka mingi. Hivi sasa nchi hizo badala ya kupunguza kutoa hewa chafu zinaendelea kuongeza kutoa hewa chafu. "Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa" na "Mkataba wa Kyoto" zote ni nyaraka za kisheria zinazolenga hali hiyo, na kuzitaka nchi zilizoendelea zitangulie kupiga hatua ya kupunguza utoaji wa hewa chafu. "Mkataba wa Kyoto" umeweka kiasi cha kupunguza utoaji wa hewa chafu kwa nchi zilizoendelea baina ya mwaka 2008 na 2010. Kadiri kipindi cha mwanzo kilichowekwa na "Mkataba wa Kyoto" kinavyokaribia, ndivyo suala la namna ya kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa linavyozidi kuzingatiwa.

Ripoti ya Kamati ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, chanzo cha ongezeko la joto duniani ni shughuli za binadamu. Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw. Pachauri kwenye mkutano alisema, katika karne iliyopita kwa wastani joto uliongozeka kwa nyuzi 0.74, lakini katika karne hii kwa makadirio joto litaongezeka kwa kiasi cha nyuzi 1.8 hadi 4. Kama hatua za uhakika zisipochukuliwa, janga kubwa litaikumba dunia. Kutokana na sababu hiyo, suala la mabadiliko ya hali ya hewa limekuwa kazi muhimu kwa Umoja wa Mataifa.

Vyombo vya habari vinaona kuwa Marekani ni nchi inayozingatiwa sana katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa. Ingawa nchi hiyo inachukua 4% ya watu wote wa dunia, lakini hewa chafu inayotolewa na nchi hiyo inachukua 25% duniani. Kutokana na kukataa kutia saini "Mkataba wa Kyoto" Marekani kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka nchini na nchi za nje. Rais George Bush hakuhudhuria mkutano huo wa siku mbili, lakini atahudhuria mkutano wa nchi 16 zinazotoa hewa chafu kwa wingi utakaofanyika katika tarehe 27 na 28 mjini Washington. Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na kukabiliwa na shinikizo kubwa la ndani na nje, serikali ya George Bush itaonesha msimamo fulani kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa.