Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-28 16:25:50    
Waafrika waliosoma nchini China

cri

Barani Afrika kuna vijana wengi waliowahi kusoma nchini China, vijana hao walisoma katika vyuo vikuu nchini China kwa miaka mitatu au mitano hata miaka kumi. Baada ya kurudi barani Afrika, vijana hao wanafanya kazi kwenye sekta mbalimbali za nchi zao kwa kutumia elimu waliyopata nchini China. Wao ni mabalozi wa urafiki na daraja la ushirikiano kati ya China na Afrika. Pia wanaonesha umuhimu katika kueneza utamaduni wa China na kulaani hoja na maneno yasiyoisaidia China.

Bw. Michael Romeo alipewa udhamini wa masomo nchini China mwaka 1998, alijifunza lugha ya Kichina kwa mwaka mmoja katika chuo kikuu cha walimu cha Nanjing, halafu alisomea mambo ya dawa kwa miaka minne katika chuo kikuu cha dawa cha China mjini Nanjing. Mwaka 2003 alirudi Uganda. Kutokana na kanuni husika, alipokea mafunzo ya matibabu kwa mwaka mmoja nchini Uganda, baadaye alitumwa kwenye shirika la usimamizi wa dawa la Uganda.

Hivi sasa katika shirika la usimamizi wa dawa la Uganda kazi ya Bw. Michael anashughulikia mambo ya uandikishaji wa dawa na upimaji wa dawa. Bw. Michael alisema kusoma nchini China kulimsaidia kupata kazi hiyo. Alisema Uganda ina upungufu wa watu wenye ujuzi wa matibabu, wanafunzi wa Uganda waliosoma katika vyuo vikuu nchini China wanakaribishwa sana. Ikilinganishwa na vyuo vikuu nchini Uganda, vyuo vikuu nchini China vina walimu wengi zaidi na mazingira mazuri zaidi ya masomo.

Akiwa ni mtu pekee anayeweza kuongea lugha ya Kichina katika shirika la usimamizi wa dawa la Uganda, Bw. Michael pia anashughulikia mawasiliano na kikundi cha madaktari wa China nchini Uganda. Aliwasiliana mara kwa mara na kikundi cha madaktari wa China kutokana na dawa zilizopita kwenye forodha. Maelezo ya dawa nyingi zinazonunuliwa kutoka China ni ya lugha ya Kichina, hakuna maelezo ya lugha ya Kiingereza, kwa hivyo Bw. Michael hutafsiri maelezo ya dawa hizo kutoka lugha ya Kichina kuwa ya lugha ya Kiingereza. Kutokana na msaada wa Bw. Michael, mawasiliano kati ya kikundi cha madaktari wa China na shirika la usimamizi wa dawa la Uganda yanaendelea vizuri.

Alipokumbuka kipindi cha kupewa udhamini wa masomo nchini China, Bw. Michael alisema mwanzoni alikabiliwa na matatizo mengi katika maisha na masomo, kutokana na tofauti ya lugha na utamaduni kati ya China na Afrika, lakini baadaye si kama tu alizoea mazingira ya huko, bali pia alipenda vyakula na utamaduni wa China.

Bw. Michael alisema anapenda muziki wa kikabila wa China, vilevile anapenda sana muziki wa pop wa China, hasa anapenda kusikiliza nyimbo zilizoimbwa na Bw. Liu Dehua na Bi. Lin Yilian. Kutokana na kufanya vizuri katika masomo yake, Chuo kikuu alichosoma Bw. Michael kilimpa sifa ya "mwanafunzi mzuri wa nje anayesoma nchini China". Alipozungumzia jambo hilo, Bw. Michael alifurahi huku akionesha picha ya hati ya sifa kwenye kompyuta. Bw. Michael alisema hatasahau maisha yake yalivyokuwa wakati akisoma nchini China, na maisha hayo yana thamani kubwa kwake, alijifunza mambo mengi yanayomnufaisha.

Alipozungumzia mpango wa baadaye, Bw. Michael alisema ana matumaini kuwa atakuwa na fursa ya kusoma zaidi nchini China, na kuangalia maendeleo na mabadiliko nchini China katika miaka kadhaa iliyopita.

Bw. Michael alisema kwa furaha kuwa ana matumaini mengine kuwa mwaka 2008 atakuja Beijing kuangalia Michezo ya Olimpiki.

*************************************

Bw. James ni mhandisi wa ofisi ya kampuni ya Huawei ya China nchini Uganda, ambaye ana umri wa miaka 30. Aliwahi kusomea kozi ya miradi ya mashine katika chuo kikuu cha Makerere nchini Uganda. Mwaka 2002 alipewa udhamini wa masomo nchini China. Baada ya kujifunza lugha ya Kichina kwa mwaka mmoja, mwaka 2003 alichaguliwa kusomea kozi ya usimamizi wa miradi katika chuo kikuu cha Tsinghua, na mwaka 2005 alihitimu na kurudi nchini Uganda.

Baada ya kurudi nchini Uganda, Bw. James alianza kutafuta kazi. Kwa kuwa wanafunzi waliosoma nchini China wana elimu kubwa, na uwezo wao wa kuzoea mazingira pia ni mkubwa, hivyo wanapotafuta kazi wanakaribishwa sana na kampuni mbalimbali nchini Uganda. Kampuni nyingi zilieleza matumaini kuwa Bw. James anaweza kufanya kazi kwenye kampuni hizo. Bw. James alifikiria sana suala la kufanya kazi serikalini au kwenye kampuni. Aliomba mapendekezo ya walimu na wenzake wa China, hatimaye aliamua kufanya kazi kwenye kampuni ya Huawei ya China ambayo ni kampuni yenye nguvu kubwa na sifa nzuri nchini Uganda.

Wakati alipokuwa mtoto, Bw. James alikuwa na shauku kubwa kuhusu China. Hasa maendeleo ya uchumi yaliyopatikana nchini China katika miaka ya karibuni yalimvutia. Bw. James alisema anataka kufanya kazi katika kampuni ya China. Utamaduni wa kampuni ya Huawei na fursa ya maendeleo iliyotolewa kwa wafanyakazi wake vimemfanya Bw. James awe na imani kuwa atapata maendeleo makubwa katika kampuni hiyo.

Alipozungumzia kipindi cha alichokuwa anasoma nchini China, Bw. James alisema alishangazwa na mawasiliano ya barabarani na mazingira ya biashara mjini Beijing. Anaona kuwa Uganda inapaswa kujifunza uzoefu wa maendeleo wa China. Licha ya hayo Bw. James anapenda sana mtindo wa maisha na kazi ya wachina, baada ya kurudi nchini Uganda, tena alidumisha desturi ya vyakula aliyojifunza. Bw. James alisema ananufaishwa sana na mtindo wa maisha na kazi wa wachina, aliona mtindo huo unaonesha "busara za mashariki".

Baada ya kurudi nchini Uganda, Bw. James alifanya sherehe mara kwa mara na wanafunzi wa Uganda waliosoma nchini China. Sherehe hizo zilikuwa zinafanyika katika mkahawa wa vyakula vya kichina. Bw. James alisema zamani waganda wengi walikuwa hawaielewi China, lakini sasa hali hiyo imebadilika. Miradi mingi nchini Uganda inaendeshwa na kampuni za China. Vyuo vikuu vya China vikiwemo chuo kikuu cha Tsinghua, chuo kikuu cha Beijing na chuo kikuu cha mawasiliano cha Shanghai vina sifa nzuri nchini Uganda. Bw. James anaona fahari sana akiwa mganda wa kwanza aliyehitimu kwenye chuo kikuu cha Tsinghua cha China.

Bw. James alisema alipowakilisha kampuni ya Huawei kuzungumza na serikali au kampuni za Uganda, anaweza kuonesha umuhimu mkubwa wa mawasiliano kati ya kampuni yake na upande wa Uganda.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-28