Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-26 16:46:52    
China yafufua sera ya kutoa bure elimu ya mafunzo ya ualimu

cri

Kuanzia muhula huu wa masomo mwezi Septemba mwaka huu, vyuo vikuu 6 vya ualimu vinavyoongozwa moja kwa moja na wizara ya elimu ya China, kikiwemo chuo kikuu cha ualimu cha Beijing, vitafufua sera ya kutoa bure elimu ya mafunzo ya ualimu. Kwa mujibu wa sera hiyo, wanafunzi wa ualimu wa vyuo vikuu hivyo wanafutiwa ada zote za masomo na pia watapewa ruzuku za maisha. Wachambuzi wanaona kuwa, hatua hiyo si kama tu inawasaidia wanafunzi wanaotoka kwenye familia zenye matatizo ya kiuchumi waweze kumaliza masomo yao, bali pia inasaidia kutatua tatizo la upungufu wa walimu kwenye sehemu za vijijini nchini China.

Tangu China mpya iasisiwe, China imeendelea kutekeleza sera za nafuu kwa wanafunzi wa ualimu. Lakini kuanzia mwaka 1997, kutokana na mageuzi ya mfumo wa elimu, vyuo vikuu vya ualimu vya China vilianza kutoza kiasi fulani au ada kamili za masomo. Mwanzoni mwa mwaka huu, waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alipotoa ripoti ya kazi za serikali kwenye mkutano wa tano wa bunge la 10 la umma la China alisema, ili kuhimiza maendeleo na usawa wa elimu, kuimarisha maendeleo na mageuzi ya elimu ya ualimu na kuwavutia wanafunzi wengi zaidi hodari kuchagua masomo ya ualimu, China itaanza tena kutoa bure elimu ya ualimu kwenye vyuo vikuu vya ualimu vinavyoongozwa moja kwa moja na wizara ya elimu ya China na kuanzisha utaratibu husika. Hatua hiyo inamaanisha kuwa sera ya elimu bure ya ualimu imerejeshwa katika vyuo vikuu vya China.

Kijana Zhu Minzan ni mwanafunzi mhitimu wa shule ya sekondari ya juu ya mji wa Guilin mkoani Guangxi. Katika mtihani wa taifa wa kujiunga na vyuo vikuu uliofanyika mwezi Juni mwaka huu, alipokelewa kwenye mchepuo wa historia katika chuo kikuu cha ualimu cha Beijing kwa kupata alama 617, na kuwa mwanafunzi anayepata elimu ya ualimu bure.

"Mwanafunzi: Hujambo, mwalimu? Nimekuja kuchukua barua ya kuruhusiwa kujiunga na chuo.

Mwalimu: Haya, subiri kidogo. Hii hapa ni ya kwako. Hongera!"

Sera ya kutoa bure elimu ya ualimu ilirejeshwa kuanzia muhula wa Autumn wa mwaka huu. Kwa mujibu wa sera hiyo, kwa muda wa miaka minne ya masomo katika vyuo vikuu, ada zote za masomo kwa wanafunzi wa ualimu zinalipwa na serikali. Lakini kabla ya kujiunga na vyuo vikuu, wanafunzi hao wanapaswa kusaini mkataba na chuo kikuu na idara ya elimu ya sehemu wanazotoka kwa kuahidi kufanya kazi ya ualimu katika shule za msingi au za sekondari kwa miaka 10 baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu. Kama wanafunzi hao wakiajiriwa na shule za mijini, lazima kwanza wafanye kazi ya ualimu katika shule za elimu ya lazima za vijijini kwa miaka miwili.

Kuwa mwalimu hodari kumeendelea kuwa ni lengo la Zhu Minzan, elimu bure imepunguza kwa kiasi kikubwa mzigo kwa familia yake. Kwa hivyo anashukuru sana kuwepo kwa sera hiyo. Zhu Minzan alisema:

"nina imani imara kuwa nitajiunga na chuo kikuu kizuri kabisa cha ualimu na kuwa mwalimu hodari kabisa nchini China. Ninatoka kwenye sehemu ya vijijini, watoto wa huko wana hamu kubwa ya kuwa na ujuzi mbalimbali. Natumai kwamba baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha ualimu cha Beijing, naweza kuwafundisha ujuzi niliojifunza na kuwafahamisha kuwa ujuzi unaweza kubadilisha mustakabali wa mtu, pia unaweza kubadilisha hali ya uchumi wa maskani yetu."

Imefahamika kuwa, sera hiyo inatekelezwa kwanza katika vyuo vikuu 6 vya ualimu vinavyoongozwa moja kwa moja na wizara ya elimu ya China, mwaka huu vyuo vikuu hivyo vimeandikisha wanafunzi zaidi ya elfu 10 wa ualimu, wengi wao wanatoka kwenye sehemu za magharibi zilizo nyuma kiuchumi. Kila mwanafunzi kati ya hao atapewa msaada ya Yuan elfu 10 kwa mwaka.

Katika chuo kikuu cha ualimu cha Beijing, idadi ya wanafunzi walioandikishwa mwaka huu na wanaotoka kwenye sehemu za vijijini imeongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko ile ya miaka iliyopita, na kufikia asilimia 52 kuliko asilimia 26 ya mwaka jana. Mkurugenzi wa ofisi ya uandikishaji wa wanafunzi ya chuo kikuu hicho Bw. Tu Qingyun alisema, wengi kati ya wanafunzi hao ni hodari sana, jambo muhimu zaidi ni kwamba wanapenda kazi ya ualimu.

Bw. Tu Qingyun anaona kuwa, sera ya kutoa elimu ya ualimu bure si kama tu inaweza kusaidia wanafunzi wanaotoka familia zenye matatizo ya kiuchumi wamalize masomo yao, bali pia inasaidia kutatua suala la upungufu wa walimu kwenye sehemu za vijijini nchini China.

Aidha kwa mujibu wa sera hiyo, vyuo vikuu vitachagua walimu hodari kuwafundisha wanafunzi wa ualimu, kuanzisha utaratibu wa kuweka watu wa kuwaongoza wanafunzi hao, na kukamilisha utaratibu wa kutuma wanafunzi kufanya mazoezi katika shule za msingi na za sekondari. Chuo kikuu cha ualimu cha Beijing kimefanya maandalizi mazuri katika utekelezaji wa sera hiyo, ili kuhakikisha wanafunzi hao wanaweza kuwa walimu hodari baada ya kuhitimu. Naibu mkuu wa chuo kikuu hicho Bw. Han Zhen alisema:

"elimu ya ualimu ni lazima iunganishe masomo ya nadharia na mazoezi halisi ya kazi, yaani mbali na kujifunza darasani, chuo chetu pia kinatilia maanani kutoa fursa kwa wanafunzi kufanya mazoezi ya kazi za ualimu, kwa kufuata utaratibu huo wanafunzi wanaweza kumudu vizuri kazi baada ya kuhitimu. Tunapanga kujenga vituo vya mazoezi ya kazi za ualimu katika mikoa ya Mongolia ya Ndani na Shanxi."

Waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao alitembelea chuo kikuu cha ualimu cha Beijing na kufanya mazungumzo na wanafunzi wa ualimu. Bw. Wen Jiabao alisema, kutekeleza sera ya kutoa elimu bure ya ualimu kunalenga kuweka mazingira ya kuheshimu walimu na elimu katika jamii, na kuifanya kazi ya ualimu iwe kazi inayoheshimiwa kabisa. Sera hiyo pia inataka kuwashirikisha vijana wengi zaidi hodari kujitolea katika shughuli hiyo. Bw. Wen Jiabao aliwahamasisha wanafunzi hao kufanya bidii ili kuwa walimu hodari wenye ujuzi na maadili.