Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-26 16:35:05    
Mabadiliko kwenye sehemu ya Linzhi mkoani Tibet

cri

Mkoa unaojiendesha wa Tibet uko kwenye uwanda wa juu, na inajulikana kama paa la dunia. Linzhi iliyoko mashariki mwa Tibet ni sehemu ya ajabu sana. Kuna dawa ya miti shamba ya Xuelianhua ambayo hukua kwenye sehemu yenye baridi ya mzizimo, pia kuna ndizi ambazo hukua kwenye sehemu ya joto. Kutokana na hali ya utatanishi wa ardhi ya huko, watu wa makabila madogo madogo ya Waluoba na Wamenba wanaoishi kwenye sehemu hiyo walikuwa na tatizo kubwa la kuwa na mawasiliano na sehemu nyingine. Lakini sasa wafanyakazi wa kampuni ya posta na simu ya China wamewaondolea wenyeji wa Linzhi matatizo hayo baada ya juhudi kubwa za miaka zaidi ya kumi.

Motuo ni wilaya moja ya sehemu ya Linzhi. Mkurugenzi wa idara ya mtandao wa Internet ya kampuni ya posta na simu ya Linzhi Bw. Cirenluobu alisema,

"Motuo ni wilaya pekee nchini China ambayo haina barabara kubwa kwa magari. Ukitaka kuingia kwenye wilaya hiyo, lazima utembee kwa miguu kwa siku nne kwa kupitia sehemu nyingi zenye hatari, ikiwemo mlima wa Duoxiongla wenye mwinuko wa mita zaidi ya 5000 toka uswa wa bahari unaofunikwa na theluji, eneo la ardhi oevu lenye luba wengi, na njia nyembamba isiyofikia upana wa mita moja iliyoko kando ya jabali."

Lakini hivi sasa simu zinaweza kutumika kwenye wilaya hiyo ya mlimani isiyokuwa na barabara, watu wanaoishi huko wanaweza kuwasiliana na watu wa sehemu nyingine bila kutembea kwa miguu.

Mwaka 2003, serikali ya mkoa unaojiendesha wa Tibet pamoja na kampuni ya posta na simu ya mkoa huo na serikali katika ngazi mbalimbali kwenye sehemu ya Linzhi zilianzisha mradi wa kuwezesha matumizi ya simu kwa njia ya satilaiti kwenye vijiji vyote vya sehemu ya Linzhi. Kwa kuwa milima ya sehemu hiyo inafunikwa na theluji mara kwa mara, ilikuwa ni vigumu sana kwa wafanyakazi wa kujenga mradi huo, hata siku moja farasi wa kubeba vifaa alianguka kwenye jabali na kufa papo hapo, lakini wafanyakazi hao hawakuogopa, walijifunga kwenye kamba moja na kutembea juu ya njia ndogo kando ya jabali lililofunikwa na theluji na barafu, na kujenga vituo vya simu kwenye wilaya mbalimbali za sehemu ya Linzhi zilizoko milimani. Bw. Cirenluobu alisema,

"Siku moja mawimbi ya satilaiti kwenye wilaya ya Motuo yalipotea, watu wa wilaya hiyo hawakuweza kuwa na mawasiliano ya simu na sehemu nyingine. Wakati huo yalikuwa ni majira ya baridi, milima inayozunguka wilaya ya Motuo ilifunikwa na theluji, na wilaya hiyo ikawa imefungwa. Ingawa maporomoko ya theluji yalitokea siku kadhaa kabala ya hapo, lakini tuliwatuma mafundi wawili hodari kwenda kwenye wilaya hiyo ili kufanya kazi ya utengenezaji. Nilikuwa na wasiwasi mkubwa sana kuhusu usalama wao hata nilitokwa na machozi."

Juhudi za wafanyakazi wa kampuni ya posta na simu zilirahisisha mawasiliano kati ya wakazi wa wilaya ya Motuo na watu wa sehemu nyingine wanaozuiwa na milima mirefu. Ili kutatua kabisa matatizo ya mawasiliano kwenye wilaya ya Motuo, mwaka 2004 kampuni ya posta na simu ya Tibet ya kundi la makampuni ya posta na simu ya China zilibadilisha simu ya kutumia mawimbi ya satilaiti kuwa simu isiyokuwa na waya ya kutumia vituo vya mawimbi. Baada ya jitihada kubwa za wafanyakazi wa kampuni hiyo, tarehe 19 mwezi Juni mwaka 2004, mfumo wa simu mijini na mfumo wa kuitisha mkutano kwa njia ya televisheni na simu ulizinduliwa rasmi. Mbali na hayo, mwaka jana kampuni ya posta na simu ya Linzhi ilianzisha shughuli ya mtandao wa Internet kwenye wilaya ya Motuo, ofisa wa serikali ya kijiji cha Bayi cha wilaya hiyo Bw. Yang Jihong alisema,

"Kutokana na hali duni ya mawasiliano ya barabara, wakati wa majira ya baridi theluji ikianguka, wanakijiji wetu wakitaka kwenda sehemu nyingine walikuwa wanakabiliwa na hatari ya kupoteza maisha. Lakini tangu mtandao wa Internet uanze kupatikana kwenye kijiji chetu mwezi Agosti mwaka 2006, tumepata maendeleo makubwa katika shughuli za kufanya mawasiliano na nje."

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka 2007, kampuni ya posta na simu ya China ilianza kutoa huduma ya simu kwenye vijiji vingine 432 vya sehemu ya Linzhi, na asilimia ya vijiji vinavyoweza kutumia simu kwenye sehemu hiyo imefikia 63. Sasa kwenye wilaya ya Motuo, kuna wateja 40 wa mtandao mpana wa Internet na sehemu moja inayotoa huduma ya Internet umekuwa sehemu muhimu ya maisha ya wakazi wa Motuo, na umelia nguvu mpya kwa ujenzi wa shughuli za posta na simu na maendeleo ya jamii ya wilaya hiyo. Naibu meneja wa kampuni ya posta na simu ya Linzhi Bw. BuCiren alisema kwa fahari kubwa,

"Baada ya juhudi za wafanyakazi wa shughuli za posta na simu, kampuni ya posta na simu ya Linzhi ilileta mwujiza mmoja baada ya mwingine. Kijiji cha kwanza kinachoweza kutumia simu na kijiji cha kwanza kinachotumia simu isiyokuwa na waya mkoani Tibet vyote viko kwenye sehemu ya Linzhi. Kwa kupitia njia mbalimbali ya mawasiliano ya habari zikiwemo kebo, mawimbi ya satilaiti na vituo vya kurusha mawimbi kwa simu, kampuni ya posta na simu ilitatua kabisa tatizo la mawasiliano na sehemu nyingine kwa vijiji vyote vya sehemu ya Linzhi."

Hali hiyo imewafurahisha sana wakazi wa sehemu hiyo. Kijana wa kabila la Wamenba kutoka wilaya ya Motuo Bw. Wei Ping alisema,

"Kabla ya kuanzishwa kwa huduma ya simu na mtandao wa Internet, wakazi wa Motuo walitembea kwa miguu kwa siku kadhaa ili kutuma barua moja. Lakini sasa simu na mtandao wa Internet vimetatua matatizo yetu."

Hivi sasa kampuni ya posta na simu ya Linzhi bado inaendelea na juhudi zake za kuendeleza shughuli za mawasiliano ya habari kwenye sehemu ya Linzhi. Malengo yao ni kuanzisha simu na mtandao mpana wa Internet kwenye vijiji vyote vya Linzhi. Sehemu ya Linzhi iliyojitenga na sehemu nyingine sasa imebadilika kuwa sehemu nzuri inayoweza kuwasiliana na nje kwa rahisi, na watu wengi siku hadi siku wanaweza kuishi maisha mazuri yanayosababishwa na urahisi wa posta na simu.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-26