Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-27 15:38:53    
Sura mpya ya kando za mto Changjiang mjini Wuhan

cri

Mji wa Wuhan uliopo katikati ya China ni mji mkuu wa mkoa wa Hubei. Mto Changjiang na tawi lake kuu mto Hanshui unapita kwenye mji huo. Tangu mwaka 2000, serikali ya mji wa Wuhan ilianza kukarabati kingo za kuzuia mafuriko na kuboresha mazingira kwenye kando za mito hiyo, hivi sasa sehemu hiyo inaonekana kuwa na sura mpya inayopendeza.

 

Hivi sasa mjini Wuhan, sehemu yenye urefu wa kilomita 7 ya kando ya mito imepandwa majani. Pamoja na hayo, vimefungwa vifaa mbalimbali vya mazoezi ya kujenga mwili na kuna viwanja mbalimbali. Nyumba ya mzee Li Yuzhen mwenye umri wa miaka 82 iko kwenye kando ya mto Changjiang, yeye ameshuhudia mabadiliko ya sehemu hiyo. Akikumbusha jinsi sura ya sehemu hiyo ilivyokuwa, mzee huyo alisema  "Zamani nilipokuja hapa, nilikuta takataka zikizagaa kila mahali, ilikuwa vigumu hata kutembea."

Kuanzia miaka ya 1970, sehemu ya kando za mito mjini Wuhan ilianza kutumiwa na watu kwa ajili ya kutupa takataka na vifusi, na baadhi ya watu walijenga nyumba kinyume cha sheria kwenye sehemu hiyo. Kutokana na kuwepo kwa vitu na majengo hayo, kazi muhimu ya sehemu hiyo katika kukinga mafuriko ilipungua sana. Takataka na majengo hayo haramu yalizuia mtiririko wa maji ya mto na kuongeza kina cha maji. Na kila miezi ya Julai na Agosti ambayo ni muda wa mafuriko, wakazi wa Wuhan walikuwa wanakabiliwa na hali ngumu ya kupambana na mafuriko.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya mji wa Wuhan iliimarisha mpangili wa mji, na ilitenga Yuan zaidi ya bilioni 1 kwa ajili ya mradi wa kukarabati kingo za mito na kuboresha mazingira ya sehemu ya kando za mito, mradi huo ulidumu kwa miaka mitano. Naibu mkuu wa Idara ya mambo ya maji ya Wuhan Bw. Liu Dongcai alisema  "Ili kuleta sura mpya ya sehemu ya kando za mito, serikali ya mji wa Wuhan iliunda tume ya wataalamu wa sekta mbalimbali, zikiwemo kingo za mafuriko, mpangilio wa mji, bustani, ujenzi, usimamizi wa mji na sanaa. Tulijifunza uzoefu mzuri wa miji mingine ya nchini na nje ya China, ambayo imejengwa kwenye kando za mito au bahari, kama vile Shanghai, Hangzhou, Suzhou, Hong Kong na Sydney. Katika usanifu wa kando za mito, tunazingatia upandaji wa mimea, kuonesha mandhari nzuri ya maji na kuwapa burudani wakazi wa mji."

Katika kutekeleza mradi huo kwenye kipindi cha kwanza, viwanda 58 vilihamishwa, majengo haramu yenye eneo la mita za mraba laki 3 yalibomolewa, na takataka zilizoachwa kando za mito ziliondolewa. Mbali na hayo, njia ya mito ilisafishwa, na miti zaidi ya elfu 80 na nyasi zenye eneo la mita za mraba karibu milioni moja zilipandwa. Sehemu ya kando za mito ilianza kuonekana kuwa na sura mpya. Mkazi wa mji wa Wuhan Bibi Wang Jing alisema  "Zamani nilipokwenda kwenye sehemu hiyo nilikuwa na wasiwasi, lakini sasa napenda kutembelea sehemu hiyo ili kuburudishwa na mandhari nzuri na muziki."

Kwenye kando za mito, kuna viwanja 19 vinavyowavutia sana watu ambavyo kila kiwanda kina umaalumu wake, ambapo seti zaidi ya 450 za vifaa vya mazoezi ya kujengea mwili vimefungwa na watu wanaweza kuvitumia bila malipo.

Hivi sasa watu wakifanya matembezi kando za mito, wanavutiwa na utulivu na mazingira ya kupendeza, hali ambayo inawafanya wasahau makali ya mafuriko yanayoukumba mji huo kila mwaka. Mzee Hu Zilai mwenye umri wa miaka zaidi ya 60 alieleza kufurahia mazingira ya kando za mito. Alisema "Hii ni bustani yetu, hatutakiwi kulipa ada yoyote. Tunakuja mara kadhaa kwa siku, tukiimba nyimbo na kucheza dansi hapa. Mradi huo wa serikali unawafurahisha sana watu, karibu asilimia 95 ya wakazi wanaishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huo."

Kutokana na maelezo ya wafanyakazi wa idara ya mambo ya maji ya mji wa Wuhan, baada ya kukamilika kwa mradi wa ukarabati, sehemu ya kando za mito mjini Wuhan ina urefu wa kilomita 20 na eneo la mita za mraba zaidi ya milioni 2, sehemu ambayo sasa ni uwanja mkubwa kabisa wa burudani barani Asia. Mpango wa utekelezaji wa mradi huo katika vipindi vijavyo tayari umetungwa. Kutokana na mpango huo, sehemu ya kando za mito mjini Wuhan itakuwa na urefu wa kilomita 54. Wataalamu wa maji wanasema, pamoja na kufanikiwa kuzuia mafuriko, mradi huo pia unaleta manufaa katika uhifadhi wa mazingira.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-27