|

Maonesho ya picha kuhusu maisha ya watu wa China yaliyoanza kufanyika tarehe 29, Septemba huko Cairo yanawavutia watu wengi wa Misri. Maonesho hayo ni kama madirisha yaliyofunguliwa kwa watazamaji, ambayo yanaweza kuwaletea ufahamu kuhusu historia ya China, utamaduni wake na maisha ya watu wa kawaida wa nchi hiyo. China na Misri ni nchi zenye historia ndefu, watu wa nchi hizo mbili wamekuwa wakijenga urafiki mkubwa tangu enzi na dahari. Balozi wa China nchini Misri Bw. Wu Sike alieleza kuwa, maonesho hayo yanawapa watu wa Misri fursa ya kutizama maisha ya watu wa China yalivyo. Alisema,

"Kwa kupitia kamera za wapiga picha, si kama tu watazamaji wanaweza kuangalia mabaki ya kiutamaduni kama vile, ukuta mkuu na makasri ya kifalme, pamoja na mito, milima na ardhi ambayo ni maumbile nchini China, bali pia wanaweza kutazama maendeleo ya China katika uchumi, jamii, sayansi na teknolojia, pamoja na jinsi watu wa China wanavyoishi. Ni matumaini yangu kuwa marafiki wa Misri watapata ufahamu mkubwa na wa pande zote kuhusu China ya hivi sasa na maisha ya watu wake."
Waziri wa utamaduni wa Misri Bw. Farouk Hosni alisema "Maonesho hayo ni mazuri sana, ambayo yanatuonesha nchi nzuri, jinsi inavyofanya jitihada na kushikilia kujiendeleza. Katika muda mfupi tu China imejiendeleza sana na kuwa nchi nzuri kweli. Picha hizo si kama tu zinaonesha mandhari na watu, bali pia zinaonesha vyema ambavyo China imekuwa inakwenda na wakati katika miaka ya hivi karibuni. Maonesho hayo ni muhimu, na yanaipa jamii ya Misri fursa ya kuangalia jinsi gani watu wa China wanavyokabiliana na changamoto."

Picha 156 zinazooneshwa kwenye maonesho hayo zilichaguliwa kutoka picha zaidi ya elfu 2 zilizopigwa na wapiga picha wa China na wa nchi za nje. Kijana Mohammed Said mwenye umri wa miaka 22 anasoma lugha ya Kichina kwenye Chuo Kikuu cha El-Azhar cha Misri. Alipotoa maoni yake baada ya kutazama maonesho hayo, alisema
"Nimevutiwa na picha nyingi, kwa mfano picha zinazohusu mito maarufu na Bw. Yang Liwei, mwanaanga wa kwanza wa China. Maisha nchini China ni mazuri, naona Wachina wa kawaida wanaishi kwa furaha, mimi nafurahia hali hii."
Profesa Magdi Amin kutoka Chuo Kikuu cha Ain Shams amewahi kuitembelea China mara mbili. Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari kwenye maonesho hayo, yeye aliongea kwa Kichina. Alisema
"Nafurahia kutazama maonesho haya ya picha. Kutokana na picha hizo, ninapata ufahamu kuhusu mambo mapya ambayo sijawahi kuyaona. Niliwahi kuitembelea China mwaka 1997 na 2002, nilitembelea miji ya Beijing, Shanghai na sehemu nyingine. Sasa ninaona mabadiliko mapya na makubwa ya China kutoka kwenye picha hizo."
Naibu mwenyekiti wa Shirika la urafiki kati ya Misri na China Bw. Ahmed Wali alisema
"Maonesho hayo ni muhimu kwa watu wa Misri, ambao wana urafiki mkubwa na watu wa China na wana hamu ya kupata ufahamu kuhusu maisha ya watu wa China. Picha zinazooneshwa zinahusu maisha ya wafanyakazi, wakulima na watoto wa China pamoja na maendeleo ya nchi hiyo katika mambo ya sayansi na teknolojia. Niliwahi kutembelea China mara tano, lakini kwa watu wa kawaida wasio na bahati ya kuitembelea China, maonesho ya picha ni njia nzuri ya mawasiliano ya kiutamaduni. Kutokana na picha hizo nzuri, watu wa Misri wanashuhudia maisha ya watu wa China."
|