Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-01 19:50:13    
Filamu ya katuni ya "Matembezi ya Fu Wa wa Olimpiki" yavutia

cri

Wanasesere Fu Wa wa kuashiria baraka kwenye michezo ya 29 ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008 wanawavutia sana watu wa China na wa nchi za nje. Tokea tarehe 8 Agosti, filamu ya katuni yenye sehemu 100 inayolenga kueneza elimu ya michezo ya Olimpiki ilianza kuoneshwa katika kituo cha televisheni CCTV nchini China. Filamu hiyo sio tu inawavutia watoto, bali pia inawavutia watu wazima.

Filamu ya "Matembezi ya Fu Wa wa Olimpiki" ilitengenezwa kwa fedha kutoka kwenye kituo cha televisheni cha Beijing karibu Yuan milioni 50, ni filamu yenye sehemu 100 na kila sehemu ina dakika 11. Hii ni filamu ndefu kabisa inayoeleza mambo ya michezo ya Olimpiki, ambayo inaeleza kwamba mtoto mwenye umri wa miaka 8, Da You, alipewa zawadi na baba yake yaani wanasesere watano ambao wanaashiria baraka kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008. Hadithi iliyotokea kati ya Da You na wanasesere Fu Wa inaeleza jinsi michezo ya Olimpiki ilivyoanza, ilivyoendelea, ilivyokamilishwa kisheria na mambo yaliyotokea katika historia ya Olimpiki.

Tokea tarehe 8 Agosti, siku ambayo ulibaki mwaka mzima kabla ya kufunguliwa kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing, filamu hiyo ilipoanza kuoneshwa katika kituo cha televisheni, watazamaji walikuwa ni wengi zaidi kuliko hata filamu nyingine zilizooneshwa kwenye televisheni. Mtazamaji wa Beijing Bw. Ding Yiming alisema,

"Filamu hiyo inatujulisha mambo mengi ambayo hatukuyafahamu hapo kabla, wanasesere watano Fu Wa wanacheza kama wako hai, wanatuelimisha na huku wanatuchekesha."

Baadhi ya watazamaji wanapenda sana picha zake za mtindo wa Kichina. Bi. Lin Lu alisema,

"Picha za filamu hiyo zinatuvutia hata sisi watu wazima kwa sababu ya kuwa na mtindo pekee wa Kichina ambao ni tofauti na filamu za katuni za nchi nyingine."

Filamu za katuni za China zinatengenezwa kwa picha za mtindo wa Kichina ambazo kimsingi zinachorwa kwa brashi ya wino. Picha za katuni katika filamu moja kwa kawaida zinahitaji muda wa miaka kadhaa kuchorwa. Filamu za hadithi za China kama "Ne Zha Achafua Bahari" na "Mfalme Kima Avuruga Kasri la Mbinguni" zilipata tuzo kubwa katika mashindano ya kimataifa ya filamu. Katika miaka 10 iliyopita, filamu za katuni kutoka Japan na nchi za Ulaya na Marekani zilioneshwa nchini China na ziliwavitia sana watazamaji, filamu hizo zilitumia teknolojia ya hali ya juu ya utengenezaji, na zilileta athari kubwa kwa watoto. Lakini kadiri siku zinavyopita wadau wa China wa filamu za katuni ndivyo wanaelewa zaidi kwamba kitu muhimu cha kuendeleza filamu za katuni za China ni kutumia teknolojia ya kisasa na kuunganisha maisha ya leo.

"Filamu ya katuni ya 'Matembezi ya Fu Wa wa Olimpiki' imetengenezwa kwa busara za pamoja. Miaka kadhaa iliyopita kituo cha televisheni cha Beijing kilianza kukusanya hadithi na maoni kote nchini China, na kilipata vitabu vya hadithi zaidi ya mia mbili, ingawa vitabu hivyo havikutumiwa katika filamu hiyo, lakini vilipanua mtazamo wa wahariri wa filamu hiyo. Filamu hiyo iliwashirikisha waigizaji na waimbaji mashuhuri kuweka sauti. Kwa mfano, mwimbaji mwanamke Zhang Lianying aliweka sauti ya mmoja wa wanasesere watano aitwaye "Ying Ying". Katika filamu hiyo Ying Ying ni mtoto anayependa kuimba mashairi, basi mwimbaji huyo alijitahidi kubadilisha sauti yake ili ilingane na sauti ya mwanasesere huyo. Alisema anaona fahari ya kuweza kutia sauti yake kwenye filamu hiyo. Alisema,

"Kwangu mimi hii ni kazi mpya, na mimi napenda kuiga sauti ya katuni, nilifanya hivyo na nimefanikiwa ."

Msimamizi mkuu wa matengenezo ya filamu hiyo wa kituo cha televisheni cha Beijing Bw. Shuai Min alisema sababu ya kuvutia kwa filamu hiyo ni uchangamfu na kuchekesha. Katika maandalizi ya filamu hiyo, wachoraji wengi mashuhuri wa picha za katuni walialikwa na kutoa mapendekezo yao.

Katika miaka ya hivi karibuni, watengenezaji wa filamu za katuni wamekuwa na mtazamo mpya, kwamba filamu za katuni ni lazima ziunganishwe na maisha ya leo, wala si kueleza tu hadithi za kale za China ambazo mkazo unatiliwa katika kuwaelimisha na kuwafundisha tu watoto. Bw. Shuai Min alisema, filamu ya katuni ya "Matembezi ya Fu Wa wa Olimpiki" imezingatia namna ya kuwafurahisha watoto. Alisema,

"Watoto wa hivi leo ni werevu kuliko watoto wa zamani, tusitumie hali ya zamani kuwatengenezea filamu, mambo mengi wanayaelewa, kwa hiyo filamu zetu za katuni ni lazima ziungane na hali yao ya ufahamu wa mambo na ni lazima zifungamane na maisha yao ya sasa."