Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-01 20:03:59    
Mbinu 36: Ukitaka kuwakamata magaidi, kwanza mkamate kiongozi wao

cri

"Ukitaka kuwakamata magaidi, kwanza mkamate kiongozi wao" ni sentensi inayotoka kutoka shairi la Du Fu, mshairi mkubwa wa Enzi ya Tang nchini China aliyeishi katika karne ya nane. Kwenye shairi lake aliandika hivi, "Ukitaka kumfyatulia mtu mshale, kwanza mfyatulie farasi wake. Ukitaka kuwakamata magaidi, kwanza mkamate kiongozi wao." Yaani ukitaka kumkamata mtu anayekimbia kwa farasi, ni busara kumfyatulia mshale farasi wake. Na ukitaka kuwakamata magaidi ni busara umkamate kwanza kiongozi wa genge lao.

Kuhusu "Ukitaka kuwakamata magaidi, kwanza mkamate kiongozi wao" kitabu cha mbinu za kivita kinaeleza hivi: Kusambaratisha kikosi muhimu, kumkamata kiongozi mkuu au kubomoa makao ya viongozi na kuwatia maadui katika hali ya mahangaiko ni njia inayofaa kuwashinda maadui. Vinginevyo, kama ukipoteza fursa nzuri na kuwaachia kikosi muhimu cha maadui na kiongozi wao akatoroka, ni sawa kujiletea matatizo mengi baadaye. Ufuatao ni mfano wa matumizi ya mbinu hiyo katika vita vya kale nchini China.

Katikati ya karne ya nane ilikuwa ni kipindi cha Enzi ya Tang kufikia kileleni kwa ustawi wake. Wakati huo mfalme wa enzi hiyo alizama katika maisha ya ubadhirifu na anasa, alikuwa hashughulikii hata kidogo utawala wake, jamii ilikuwa na migogoro mingi na watawala wa mitaa walifanya uasi dhidi ya utawala wa mfalme.

Mwaka 755 kwa kutumia fursa hiyo ya utawala dhaifu wa mfalme, diwani mwenye askari wengi, An Lushan, kwa kushirikiana na maofisa wake alifanya uasi wa kijeshi na mwaka wa pili akauteka mji wa Chang An, mji mkuu wa enzi hiyo. Mfalme alikimbia nje ya nchi, An Lushan alijitawaza kuwa mfalme.

Mwanzoni, kutokana na kushinda kila vita, An Lushan alikuwa mjeuri wa vita. Wakati huo jemadari mmoja wa An Lushan aliyeitwa Yin Ziqi aliongoza askari wake laki moja kushambulia mji wa Huaiyang ambao ulikuwa muhimu kwa vita. Lakini jemadari aliyelinda mji huo Zhang Xun alikuwa na askari elfu kadhaa tu. Jeshi la uasi lilizingira mji huo na liliushambulia kwa zaidi ya mara ishirini bila kuweza kuuteka.

Ili kulishinda jeshi la uasi, Zhang Xun alitumia ujanja wa kuwasumbua maadui. Kila usiku maadui walipoanza kulala, Zhang Xun aliwaamrisha askari wake kupiga ngoma na kelele kwa nguvu zao kuwaghasi. Jemadari wa waasi Yin Ziqi alidhani anashambuliwa, akawaamrisha askari wake kujiandaa kwa mapambano, lakini Zhang Xun aliwatuliza tu askari wake bila kufanya mashambulizi. Alitumia ujanja huo kwa siku nyingi mfululizo na kuwafanya maadui wachoke kabisa. Siku moja Zhang Xun alitumia nafasi ya maadui kulala usingizi aliwaongoza askari wake kutoka mjini na kuwashambulia kwa ghafla, maadui waliozinduka usingizini walihangaika ovyo, Zhang Xun aliwaua maadui elfu kadhaa.

Kutokana na kuwa Zhang Xun alizidiwa kwa idadi ya maadui mara dufu, alitumia mbinu ya "Ukitaka kuwakamata magaidi, kwanza mkamate kiongozi wao", alitaka kumwua jemadari wa waasi Yin Ziqi, lakini yeye na askari wake hawakufahamu Yin Ziqi yukoje, na wangewezaji kumtambua kati ya askari waasi wengi? Wakati huo Zhang Xun aliwaambia askari wake wafyatue mishale kwa vijiti vya bandia vilivyochongwa kwa ncha. Maadui wengi waliopigwa mishale walijiona salama, wakagundua kwamba mishale yenyewe ilikuwa ya bandia, wakamkimbilia Yin Ziqi ili kutoa ripoti. Zhang Xun alipoona hali hiyo mara alimtambua Yin Ziqi mwenyewe na kuwaamrisha askari wake wamfyatulie mishale ya kweli, moja ya mishale ulimchoma Yin Ziqi kwenye jicho lake la kushoto, akaanguka kutoka kwenye farasi, askari wake wakachanganyikiwa na kukimbia ovyo. Zhang Xun aliwashinda kabisa maadui kwa kutumia askari wachache.

Mbinu hiyo ya "Ukitaka kuwakamata magaidi, kwanza mkamate kiongozi wao" ni rahisi kuelewa, lakini matumizi yake yana ugumu wake, kwa sababu "kiongozi" hulindwa kabisa, kwa hiyo ni lazima kutumia udanganyifu wa kila aina ili kumshawishi ajitokeze hadharani.