Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-02 18:03:39    
Vladimir Putin amepanga kugombea nafasi ya ubunge kwenye baraza la chini la bunge la Russia

cri

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema atagombea nafasi ya ubunge kwenye baraza la chini la bunge la Russia kwa tiketi ya chama cha Allied United Russia katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 2, mwezi Desemba. Rais Putin alitoa kauli hiyo tarehe 1 Oktoba kwenye mkutano mkuu wa chama hicho. Hata hivyo alisema hatajiunga na chama hicho, bali anashiriki kwenye uchaguzi kwa kupitia chama hicho, kama mtu aliyependekeza kuanzishwa kwa chama hicho. Rais Putin aliongeza kuwa, yeye si mwanachama wa chama chochote, hali ambayo inafanana na watu wengi kabisa wa Russia, na hana nia ya kubadilisha hali hiyo.

Rais Putin si mwanachama wa chama cha Allied United Russia, lakini ana uhusiano wa karibu na chama hicho. Mwezi Desemba mwaka 2001 ulipofanyika uchaguzi wa baraza la chini la bunge la Russia, Rais Putin alishiriki kwenye mkutano wa kuanzishwa kwa chama hicho, ambapo jina lake lilibadilishwa kutoka "chama cha umoja na taifa". Kwenye mkutano huo Putin hakukubali ombi la kumwalika ajiunge na chama hicho. Lakini kuanzia hapo rais Putin amekuwa akifuatilia maendeleo ya chama hicho. Hivi sasa nchini Russia wanachama makumi kadhaa wa chama hicho wanashika nyadhifa za wakuu wa mikoa na nafasi za ubunge kwenye baraza la juu la bunge la Russia, na chama hicho pia kina nia ya kuvutia kura nyingi za wananchi kwa kutumia heshima kubwa ya rais Putin. Kwenye kampeni ya uchaguzi utakaofanyika mwezi Desemba mwaka huu, chama hicho kimetoa kauli mbiu isemayo "mpango wa Putin, ni ushindi wa Russia."

Uchunguzi wa maoni ya watu wa Russia uliofanyika hivi karibuni unaonesha kuwa, asilimia 55 ya watu wa Russia wanakiunga mkono chama cha Allied United Russia, huku rais Putin mwenye akiwa na asilimia 80 ya uungaji mkono miongoni mwa watu wa Russia. Ndiyo maana hatua hiyo ya Rais Putin kugombea nafasi ya ubunge kwenye baraza la chini la bunge la Russia kwa tiketi ya chama cha Allied United Russia, hakika itaimarisha hadhi ya chama hicho nchini Russia.

Mbali na hayo, kwenye mkutano wa tarehe 1 Oktoba, rais Putin alisema anapenda kupokea pendekezo la yeye kuchukua wadhifa wa waziri mkuu wa serikali ijayo mwaka 2008, kwa sharti kwamba chama cha Allied United Russia kinapata ushindi kwenye uchaguzi wa bunge na rais mpya atakayepatikana kwenye uchaguzi wa mwaka kesho atakuwa mtu makini, mwenye uwezo na ufanisi mkubwa.

Hivi sasa matamshi hayo ya rais Putin yanafuatiliwa sana nchini Russia. Baadhi ya vyombo vya habari vimetoa hoja kuhusu katiba na sheria ya uchaguzi ya Russia kuruhusu rais mwenyewe kugombea kiti cha ubunge au la. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Russia Bw. Vladimir Chiulov akijibu hoja hilo, alisema inapaswa kutafuta vifungu vinavyohusu suala hilo kwenye sheria, hata hivyo wajumbe wengi wa tume ya uchaguzi wameeleza wazi kumwunga mkono rais Putin kugombea nafasi ya ubunge.

Wachambuzi wanasema matamshi hayo ya rais Putin yatakuwa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa uchaguzi wa baraza la chini la bunge la Russia utakaofanyika mwezi Desemba mwaka huu, na hata uchaguzi wa urais utakaofanyika mwezi Machi mwaka kesho. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, rais Putin alikuwa anakanusha mara kwa mara uvumi kuhusu yeye kugombea nafasi ya urais kwa awamu ya tatu, na kwenye mkutano mkuu wa chama cha Allied United Russia uliofanyika tarehe 1 Oktoba, alirudia msimamo huo. Lakini hatua mbalimbali alizochukua hivi karibuni, zikiwemo kumteua Bw. Viktor Zubkov kuwa waziri mkuu na kutangaza yeye mwenyewe kugombea nafasi ya ubunge, huenda zitamwezesha Rais Putin kubaki na nguvu ya ushawishi hata baada ya muda wake wa urais kumalizika. Suala hilo linafuatiliwa na watu wengi.