Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-02 19:43:12    
Barua 0930

cri

Msikilizaji wetu Mchana J Mchana wa sanduku la Posta 1878 Morogoro, Tanzania, ameanza barua yake kwa kutoa shukurani zake kwa uongozi wa Radio China Kimataifa kwa kuwajali wasikilizaji na hasa kuwakumbuka kwa kuwatumia vipeperushi mara kwa mara. Pia anapenda kuwashukuru watangazaji, kwani anasema bila wao wasingepata ujumbe kwa njia ya Radio.

Anasema lengo la barua yake ni kutoa shukurani zake kwa uongozi wa Radio China kimataifa kwa kuwasikiliza wasikilizaji na kutekeleza ombi lao la kuongeza muda wa kipindi cha salamu zenu. Anasema alifurahina baada ya mabadiliko hayo aliamua kufanya utafiti kuhusu vipindi vya Radio China Kimataifa na kulinganisha na vya zamani, na ameona kuwa katika siku zijazo kipindi cha salamu kitakuwa bora zaidi kwa siku zijazo. Anatoa pongezi nyingi sana na anasema tusiishie hapo bali tuzidi kuweka mikakati ya kukiboresha zaidi.

Kwa upande wa Radio China Kimataifa anasema sasa inasikika hadi vijijini kwani ameshuhudia makundi kama matatu kati ya makundi hayo, mawili yalikuwa yakisikiliza taarifa ya habari na ndipo yalipotokea mabishano kuhusu watangazaji kama ni watanzania au wakenya. Anasema ingawa alikuwa mgeni katika kijiji hicho, ilibidi aingilie kati kwa kuwaonesha kijitabu chake chenye anuani na kumbukumbu zote za Radio za nje, vipindi vya Radio China na watangazaji, na kumaliza ubishi huo. Mwisho anapenda kuipongeza China kwa maandalizi mazuri ya michezo ya olimpiki, ingawa siyo kazi ndogo lakini mungu ataiwezesha kufanikisha shughuli zote kwa ukamilifu. Pia anamuomba Mama Chen atakapostaafu aende Tanzania kuwaaga. Na kwenye barua yake nyingine Bw Mchana anasema, angependa watangazaji kutoka Tanzania wanaporudi Tanzania wawe wanawasiliana na wasikilizaji wa Radio China Kimataifa, ili kuwaelimisha zaidi na hivyo kujua nini cha kufanya ili kuiimarisha Radio China Kimataifa.

Tunakushukuru sana Bw Mchana J Mchana kwa barua yako inayotupongeza kwa mabadiliko tulivyofanya kwenye vipindi vyetu. Tulifanya mabadiliko hayo kutokana na matakwa yenu wasikilizaji, tunafurahi sana kusikia kuwa mnafurahia mabadiliko hayo, bila shaka fursa inapopatikana tutaendelea kuboresha vipindi vyetu. Na kuhusu wafanyakazi wa Radio China kimataifa kuwasiliana na wasikilizaji wetu wakiwa huko Tanzania, hilo ni jambo ambalo tunazingatia, Mimi mwenyewe Chen nilipokuwa Dubai nilijitahidi kupata fursa ya kuonana na mmoja wa wasikilizaji wetu wa huko Bw Mabruk Msabah, nilipokuwa Kenya na wafanyakazi wenzangu tuliweza kukutana na wasikilizaji, na hivi karibuni Bw Fadhili Mpunji alipokuwa Tanzania alifanya mawasiliano na wasikilizaji wetu Bw Ngogo, Bw Njereka na Bw Onesmo Mponda, kutokana na kuwa na muda mfupi hakupata nafasi ya kufanya nao mahojiano. Tunaona kuwa mapendekezo yako ni mazuri tutajitahidi kufanya hivyo

Msikilizaji wetu mwingine ni Stephen Magoye Kumalija wa sanduku la Posta 1067 Kahama Shinyanga, Tanzania, yeye kwenye barua yake anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa hatujambo, tukiwarushia matangazo kutoka hapa mjini Beijing. Anasema anaipongeza serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa michezo ya olimpiki itakayofanyika mwakani mjini Beijing, na kuipongeza pia kwa kuandaa vizuri mkutano wa mfuko wa maendeleo wa Benki ya Afrika, uliofanyika tarehe 16 Mei huko mjini Shanghai.

Anasema benki ya maendeleo ya Afrika ina wanachama wapatao 77 duniani kote, ikiwa wanachama 53 ni kutoka bara la Afrika na wanachama 24 wanatoka katika mabara ya Asia, Ulaya na Amerika. Anaendelea kuipongeza sana serikali ya China kwa kuwa mstari wa mbele kutoa wataalamu katika nyanja mbalimbali na misaada kwa nchi za Afrika, lakini pia kuendeleza uhusiano mzuri kwa njia ya Radio kwa kutangaza katika lugha 43, na kwa njia ya mtandao wa Internet. Mwisho anaomba uhusiano mzuri wa kirafiki kati yake na Radio China Kimataifa uendelee.

Msikilizaji wetu Abubakari S Omary wa sanduku la Posta 1345 Musoma Mara, Tanzania anaanza barua yake kwa kusema yeye ni msikilizaji wa Radio China Kimataifa, na anafurahishwa na huduma zetu na anatupa hongera na anashukuru kwa kumtumia kadi za salamu pamoja na zawadi nyingine. Anasema yeye alishiriki kwenye chemsha bongo na alituma majibu yake, lakini hana uhakika kama majibu yake yalitufikia. Pia anapenda kujua kama barua yake ya chemsha bongo ilifika, na anaomba tumrudishie majibu ya alama alizopata. Anapenda tumtumie nyaraka mbalimbali kuhusu historia ya Radio China na vitabu vinavyohusu mambo ya China na utamaduni.

Msikilizaji wetu mwingine ni Jacob Nyanda wa sanduku la Posta 473 wa shule ya Sekondari Kanadi, Bariadi, nchini Tanzania yeye kwenye barua yake anasema anaomba kuwa mwanachama wa Radio China kimataifa. Anasema yeye ni mwanafunzi wa sekondari ya kutwa, na anapenda kujifunza lugha mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kichina. Anasema ameamua kuomba kujiunga na Radio China Kimataifa, baada ya kuona kuwa ni Radio yenye vipindi vizuri sana.

Pia angependa atumiwe ratiba ya vipindi vyetu, kwani huwa ni shida kwake kupata matangazo yetu.