Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-03 19:50:05    
Chuo kikuu cha Tongji cha Shanghai chajenga chuo kikuu kinachobana matumizi ya nishati

cri

Hivi sasa China inajitahidi kuchukua hatua mbalimbali za kupunguza uchafuzi na kubana matumizi ya nishati ili kuhakikisha kuwa, ifikapo mwaka 2010 nchi nzima inatimiza lengo la kupunguza asilimia 20 ya nishati katika uzalishaj mali wenye thamani ya yuan elfu 10 kuliko ile ya mwaka 2005. Chuo kikuu cha Tongji cha Shanghai ni mfano mmoja wa kuigwa, kwa kuwa kimejitahidi kujenga chuo kikuu chenye kubana matumizi ya nishati kwa kutumia teknolojia mpya.

Wasikilizaji wapendwa, mkiingia kwenye chuo kikuu hicho, hamuwezi kuona kuwa chuo kikuu hicho chenye historia ya miaka mia moja kinatofautiana na vyuo vikuu vingine. Lakini mkitazama kwa makini mtaweza kugundua kuwa majengo mengi katika chuo kikuu hicho yana usanifu maalum, au yamerekebishwa kwa njia maalum. Mabadiliko hayo yote yana lengo moja yaani kubana matumizi ya nishati.

Msichana Liu Wen anayesoma katika chuo kikuu hicho alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, mwanzoni jambo lililomvutia sana ni kwamba maji taka yaliyotolewa kwenye mabafu yalikuwa yanatumika kumwagilia maua baada ya kushughulikiwa. Liu Wen alisema:

"naupenda mfereji unaotoka kwenye mabafu, maji ya kuoga yakitoka kwenye mabafu yanayotolewa baada ya kushughulikiwa na kwenda kwenye mfereji huo. Hatua hiyo si kama tu unahifadhi mazingira, bali pia imeongeza uzuri wa mazingira ya chuo chetu."

Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, katika chuo kikuu cha Tongji miundombinu ya kushughulikia maji taka imejengwa karibu na mabafu, wafanyakazi wa huko walieleza kuwa, maji taka yanashughulikiwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya viumbe inayoitwa MBR (Membrane bioreactor). Teknolojia hiyo ni teknolojia mpya ya kushughulikia maji taka inayounganisha teknolojia za kisasa za viumbe, inaweza kuondoa kikamilifu takataka za kiviumbe zilizoko kwenye maji. Ikilinganishwa teknolojia ya kawaida ya kushughulikia maji taka, teknolojia hiyo inaweza kutoa maji safi zaidi, vifaa vinavyotumia teknolojia hiyo ni vidogo zaidi na vinaendeshwa kwa urahisi zaidi. Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, maji taka yaliyoshughulikiwa yanaonekana safi na angavu, na yanaweza kutumika moja kwa moja katika umwagiliaji.

Mbali na hayo mabafu ya chuo kikuu hicho pia yanatumia teknolojia ya nishati ya jua, kila siku tani 30 za maji zinapashwa joto kwa nishati ya jua. Aidha, mabomba mengi ya shaba yamewekwa chini ya vyumba hivyo, maji yenye joto yanayotoka mabafuni yakipita nje ya mabomba hayo, yanaweza kuongeza nyuzi joto kati ya 3 na 5 kwa maji safi yaliyomo kwenye mabomba hayo. Hatua hiyo pia inapunguza kiasi matumizi ya nishati.

Chuo kikuu cha Tongji kilitoa mpango wa kujenga chuo kikuu kinachobana matumizi ya nishati mwaka 2003, ilikuwa ni mapema zaidi kuliko vyuo vikuu vingine kote nchini China. Naibu mkuu wa chuo kikuu hicho Bw. Chen Xiaolong alisema, ili kutimiza lengo hilo, chuo kikuu hicho kilianzisha kamati ya usimamizi wa shughuli za kubana matumizi ya nishati na ofisi ya usimamizi wa nishati, pia kilitunga kanuni mbalimbali za kubana matumizi ya nishati na kujenga au kurekebisha majengo yanayobana matumizi ya nishati. Mbali na hayo, chuo kikuu hicho pia kimeanzisha utafiti wa teknolojia kuhusu shughuli hizo. Bw. Chen Xiaolong alisema:

"tulichukua hatua na kutumia mbinu mbalimbali katika ujenzi wa chuo kikuu chetu. Kama vile katika kipindi cha mwanzo cha kutathmini na kuthibitisha mradi huo, tulitathmini kwa makini manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na hatua za kubana matumizi kwenye majengo, pia tulitumia raslimali za taaluma mbalimbali za chuo chetu katika kufanya uvumbuzi wa teknolojia ya ujenzi na teknolojia ya kubana matumizi ya nishati, kwa msingi wa kufikia au kuzidi kigezo cha taifa cha kubana matumizi ya nishati."

Bw. Chen Xiaolong alisema, elimu ya ujenzi, mazingira, mashine na teknolojia ya kujiendesha za chuo kikuu cha Tongji zinachukua nafasi ya mbele nchini China na hata kote duniani. Hivyo walijumuisha teknolojia za taaluma mbalimbali na kutumia mtizamo wa kubana matumizi ya nishati kwenye majengo katika usanifu wa majengo mapya na marekebisho ya majengo ya zamani, ili kufanya nishati atumiwe kwa ufanisi zaidi katika majengo.

Teknolojia mpya mbalimbali za kubana matumizi ya nishati zikiwemo kupanda mimea juu ya mapaa ya majengo na kutumia taa zinazobana matumizi ya umeme, pia zimetumiwa katika ujenzi wa chuo kikuu hicho. Chuo kikuu hicho pia kimeweka mitambo ya kutumia kadi ya IC kwenye mabweni ya wanafunzi na mabafu, ili kuimarisha usimamizi kuhusu matumizi ya maji na umeme. Aidha, chuo kikuu hicho pia kinafanya shughuli mbalimbali za kueneza ufahamu kuhusu kubana matumizi ya nishati, ili kueneza na kuinua mtizamo wa kutunza nishati kwa wanafunzi na walimu wa chuo kikuu hicho. Mwanafunzi wa mchepuo wa hisabati katika chuo kikuu hicho Bi. Cui Xuecan alisema, mbali na chuo kikuu kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa vya kubana matumizi ya nishati, hivi sasa mtizamo huo umeenea katika kila fani za maisha yao. Bi. Cui alisema:

"kwa mfano, chuo kikuu kimepunguza muda wa kutoa maji moto, wanafunzi wanapaswa kuchukua maji moto katika muda fulani wa mchana, ili mashine ya kuchemsha maji isije kufanya kazi mchana na usiku."

Ofisa wa chuo kikuu hicho Bw. Zhou Jialun alidokeza kuwa, shughuli za kubana matumizi ya nishati kwa njia ya teknolojia na usimamizi zimeleta manufaa makubwa ya jumla kwa chuo kikuu hicho. Mwaka jana, shughuli hizo peke yake zilipunguza gharama za matumizi ya nishati kwa Yuan milioni 12. Bw. Zhou Jialun alisema:

"katika miaka ya hivi karibuni, chuo kikuu cha Tongji kimepata maendeleo makubwa katika kujenga chuo kikuu chenye kubana matumizi ya nishati kwa kutumia raslimali za taaluma mbalimbali, kufanya utafiti na uzoefu kutokana na hali halisi ya chuo kikuu hicho. Tunaona kuwa shughuli hizo zina manufaa mbalimbali, ya kwanza, matumizi ya nishati na utoaji wa uchafuzi umepunguzwa kihalisi, gharama za matumizi ya nishati za chuo kikuu hicho pia zimepungua kidhahiri; ya pili, shughuli hizo zimewashirikisha walimu na watafiti wengi kwenye utafiti wa teknolojia na mbinu mpya za kubana matumizi ya nishati; ya tatu, shughuli hizo zimeeneza mtizamo wa kutunza raslimali, haki na usawa kwa wanafunzi, ambao utawasaidia kuwa watekelezaji na waenezaji thabiti wa mtizamo huo baada ya kujiunga na jamii."