|
Katika hali isiyotarajiwa, waziri mkuu wa Uingereza Bw. Gordon Brown tarehe 2 Oktoba alifanya ziara ya ghafla nchini Iraq. Baada ya kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Iraq Bw. Nouri Maliki, Brown aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wanajeshi elfu moja wa Uingereza kati ya wale walioko huko Basra, mji wa kusini mwa Iraq wataondolewa kabla ya mwishoni mwa mwaka huu. Wachambuzi wa mambo ya siasa wanasema hatua hiyo ya Brown huenda ni ishara ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Uingereza kabla ya mpango uliowekwa, lakini haimaanishi kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya sera ya serikali ya Uingereza katika mambo ya Iraq.
Mwezi Juni mwaka huu Bw Brown alifanya ziara nchini Iraq alipokuwa waziri mkuu mteule. Ziara hiyo iliwapa watu matumaini kuwa huenda atarekebisha kwa kiasi kikubwa sera ya Uingereza kuhusu mambo ya Iraq. Baada ya Bw. Brown kuingia madarakani, mwanzoni mwa mwezi Septemba alitoa amri ya kuondoa wanajeshi wa Uingereza kutoka mji wa Basra hadi nje ya mji huo. Hadi sasa idadi ya wanajeshi wa Uingereza nchini Iraq imepungua hadi kufikia 5500, lakini uamuzi huo ulitolewa na serikali ya Bw. Blair. Mbali na kuwahamishia wanajeshi wa Uingereza kwenye kitongoji cha mji wa Basra, Bw. Brown hakuchukua hatua yoyote nyingine kubwa. Na safari hii amefanya ziara nchini Iraq bila matarajio na kutangaza kuondoa wanajeshi elfu moja wa Uingereza kutoka nchini humo, idadi hiyo ni ndogo kuliko makadirio ya wanajeshi elfu 2 yaliyofanywa na vyombo vya habari vya Uingereza.
Wachambuzi wanasema hatua hiyo ya Bw. Brown kupunguza idadi ya wanajeshi wa Uingereza nchini Iraq ni maonesho ya kisiasa tu. Kutokana na maslahi ya Uingereza na hali ya kimataifa inayoikabili nchi hiyo, haiwezekani kwa Bw. Brown kuifanyia marekebisho makubwa sera iliyotungwa na mtangulizi wake Bw. Tony Blair, hususan katika suala la Iraq, viongozi hao wawili hawana maoni tofauti juu ya suala hilo. Awali ilipojadili suala kuhusu Uingereza kutuma wanajeshi wake nchini Iraq, Bw Brown alikuwa anaunga mkono kidete msimamo wa kutuma wanajeshi. Na katika miaka iliyofuata, Bw. Brown aliyekuwa waziri wa fedha, alishughulikia kutoa fedha kwa shughuli za jeshi la Uingereza nchini Iraq. Lakini Bw Brown alijifunza kutokana na hatma ya kujiuzulu iliyomkuta Bw. Blair, na ili kurudisha uungaji mkono wa wananchi, ilimlazimu achukue hatua fulani kuhusu suala la Iraq. Na hatua alizochukua Bw. Brown ni kurekebisha kidogo sera kuhusu mambo ya Iraq, hata kufanya marekebisho ya maneno tu.
Mbali na hayo nchini Uingereza ilipoamua kutuma wanajeshi nchini Iraq au la, chama cha upinzani wahafidhina na chama tawala Labour vilikuwa na misimamo sawa. Hivi sasa machafuko nchini Iraq yanatumiwa na chama cha upinzani kama silaha ya kukishambulia chama tawala. Kutokana na hali hii, serikali ya Brown ikibadilisha sera kuhusu mambo ya Iraq na kuondoa wanajeshi wote kutoka kwenye nchi hiyo, hakika itapondwa vikali na upande wa upinzani.
Zaidi ya hayo, Bw. Brwon aliamua wakati huu kuizuru Iraq na kutangaza mpango wa kuondoa wanajeshi, kunahusiana na makadirio kwamba Brown huenda itafanya uchaguzi mkuu kabla ya mpango uliowekwa. Tangu Brown ashike wadhifa wa waziri mkuu, Uingereza imekuwa ikikumbwa na mafuriko na magonjwa ya midomo na kwato za wanyama, pamoja na wimbi la watu kutoa fedha kutoka kwenye akaunti zao benkini. Na serikali ya Brown ilipambana na matatizo hayo kwa ufanisi, na sasa inaungwa mkono na watu wengi nchini Uingereza. Kwa hiyo sasa kutangaza mpango wa kupunguza idadi ya wanajeshi wa Uingereza nchini Iraq, hakika ni hatua inayolenga kuondoa athari ya uamuzi wa kutuma wanajeshi nchini Iraq uliotolewa na serikali ya Blair na kukisaidia chama tawala cha Labour kipate kura nyingi zaidi kwenye uchaguzi mkuu.
|