Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-04 16:27:14    
Kwa nini jeshi la Marekani limeshindwa kupata mahala pa kujenga ofisi za kituo chake barani Afrika?

cri

Jeshi la Marekani tarehe 2, Oktoba lilitangaza kuwa, kituo chake kinachoshughulikia kuratibu shughuli za kiusalama na mapambano dhidi ya ugaidi barani Afrika kilianza kufanya kazi tarehe mosi Oktoba. Hivi sasa makao makuu ya kituo hicho yako mjini Stuttgart, nchini Ujerumani.

Kituo hicho kinaoongozwa moja kwa moja na wizara ya ulinzi ya Marekani, ambayo inashughulikia mambo ya jeshi la Marekani barani Afrika isipokuwa Misri. Rais George Bush wa Marekani alitoa idhini ya kuanzishwa kwa kituo hicho mwezi Februari mwaka huu. Kufuatia tukio hilo, ujumbe wa wizara ya ulinzi ya Marekani ulitembelea nchi zaidi ya 10 barani Afrika, ukizishawishi nchi hizo zipokee mpango wa kuanzishwa kwa kituo hicho cha Marekani barani Afrika na kuchagua sehemu ya kujenga makao makuu ya kituo hicho. Lakini mpango huo ulipingwa na nchi za Afrika.

Wachambuzi wanasema, msimamo huo wa nchi za Afrika unatokana na kuhofia kuharibika kwa ukamilifu wa mamlaka ya nchi hizo. Nchi za Afrika zinaona hatua hiyo ya Marekani hakika italeta kuingilia mambo ya ndani ya nchi za Afrika, na kuzifanya nchi za Afrika zipoteze uhuru wa kujiamulia baadhi ya mambo. Waziri wa mambo ya nje wa Nigeria Bw. Ojo Maduekwe alieleza wazi wasiwasi wake, akisema bara la Afrika halikaribishi majeshi ya nje, na jeshi la Marekani kukaa barani humo hakika litasababisha kuharibika kwa mamlaka ya nchi za Afrika.

Mbali na hayo Marekani ikiwa ni nchi yenye nguvu kubwa za kijeshi kuliko nyingine duniani, inapenda kutumia nguvu za kijeshi katika kutatua masuala ya kimataifa, hali ambayo inaongeza wasiwasi kwa nchi za Afrika. Mwaka 2003 serikali ya George Bush iliishambulia Iraq na kuuangusha utawala wa Saddam Hussein bila ridhaa ya Umoja wa Mataifa, matukio kama hayo yanazifanya nchi za Afrika ziwe na wasiwasi kwamba, Marekani pia itaweza kutumia nguvu katika kuangusha serikali za nchi za Afrika zisizoifurahisha Marekani.

Maofisa wa Marekani wanapogusia kuhusu kuanzisha kituo hicho barani Afrika, wanazungumza sana kuhusu uhusiano wa kiushirikiano na kiwenzi kati ya Marekani na nchi za Afrika. Hata hivyo nchi nyingi za Afrika zinaamini kuwa, Marekani kuanzisha kituo chake barani Afrika kuna lengo la kulinda maslahi yake tu. Marekani imesisitiza mara kwa mara kuwa, kuanzishwa kwa kituo hicho barani Afrika hakulengi kuweka shinikizo kwa nchi za Afrika, wala haulengi kushindana na nchi nyingine zenye nguvu ya ushawishi barani Afrika, lakini nchi za Afrika zinahofia kuwa Marekani itaweza kudhibiti bara la Afrika kwa urahisi kwa kupitia kituo hicho, na kuitumia Afrika katika kulinda maslahi ya Marekani duniani. Kuanzishwa kwa kituo hicho pia kutaisaidia Marekani ipate maliasili za Afrika kwa urahisi, hususan kupata udhibiti wa maliasili ya mafuta barani Afrika. Mtaalamu kutoka taasisi ya usalama ya Pretoria nchini Afrika Kusini alisema, nchi za Afrika zinafuatilia suala la maendeleo, lakini kuanzishwa kwa kituo cha kijeshi cha Marekani barani humo hakutaweza kuondoa umaskini. Ikiwa Marekani ina nia ya kuisaidia Afrika, ni wazi kwamba kuanzisha kituo cha kijeshi sio njia sahihi.

Ingawa Marekani imesema itaendelea na mazungumzo na nchi za Afrika ili kituo hicho kijengwe barani Afrika, lakini kutokana na hali ilivyo sasa, si kazi rahisi kutimiza lengo hilo bila kuondoa wasiwasi wa nchi za Afrika.