|
Wakati uchaguzi mkuu wa Pakistani unapokaribia kufanyika hapo tarehe 6 Oktoba, rais Pervez Musharraf amechukua hatua mbalimbali ili achaguliwe tena kuwa rais wa nchi hiyo. Vyombo vya habari vya Pakistan vimechambua kuwa, rais Pervez Musharraf anatazamiwa kupata ushindi kwenye uchaguzi huo.
Katika juhudi zake za kushinda kwenye uchaguzi huo, suala kuu linalomkabili rais Musharraf ni yeye kugombea urais huku akiwa mnadhimu mkuu wa jeshi la nchi kavu la Pakistan. Hivi karibuni viongozi wa vyama vya upinzani walitoa mashtaka dhidi ya Musharraf kwenye mahakama kuu ya Pakistan, wakidai kwamba rais kushika wadhifa wa kijeshi ni hatua inayokwenda kinyume na katiba, vile vile walitaka mahakama kuu itoe uamuzi kuhusu Bw. Musharraf anastahili kugombea urais au la. Tarehe 28 Septemba, mahakama kuu ya Pakistan ilitoa uamuzi, ikipinga mashtaka hayo na kumruhusu Bw. Musharraf ashiriki kwenye uchaguzi wa urais huku akiwa kiongozi wa kijeshi. Uamuzi huo uliondoa tatizo kubwa linalomzuia Bw Musharraf kuweza kugombea wadhifa wa rais wa awamu nyingine. Tarehe 3 Oktoba rais Musharraf alieleza wazi kuwa, akishinda kwenye uchaguzi wa urais atajiuzulu wadhifa wake wa mnadhimu mkuu wa jeshi la nchi kavu kabla ya tarehe 15 Novemba. Na siku moja kabla ya hapo Bw Musharraf alikuwa amemteua mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi Bw Ashfag Parvez Kayani kuwa mrithi wake wa kijeshi. Habari zinasema kuwa Bw. Kayani ni mfuasi mkubwa wa Bw Musharraf, na uteuzi huo umeonesha nia imara ya Bw Musharraf kuwa atatekeleza ahadi yake baada ya uchaguzi.
Mbali na hayo rais Musharraf amekuwa akichukua hatua mbalimbali kuwasiliana na vyama vya upinzani. Kuanzia miezi kadhaa iliyopita rais Musharraf alikuwa ameanza kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Bi. Benazir Bhutto ambaye ni mwenyekiti wa chama kikubwa kabisa cha upinzani cha PPP, kuhusu ushirikiano katika uchaguzi na mgawanyo wa madaraka. Tarehe 4 Oktoba Bi. Bhutto alitangaza kuwa mazungumzo hayo yanakaribia kufikia makubaliano. Inasemekana kuwa serikali ya Pakistan imekubali kumsaheme Bi. Bhutto na kufuta mashtaka ya rushwa dhidi yake.
Lakini kwa waziri mkuu mwingine wa zamani Bw. Nawaz Sharif aliyeishi uhamishoni kwa miaka 7, alifukuzwa nje na serikali ya Pakistan tarehe 10 Septemba, mara alipofika uwanja wa ndege wa Islamabad. Kuwashughulikia Bi. Bhutto na Bw. Sharif kwa mbinu tofauti kunamaanisha kuwa, wakati wa kufanya mazungumzo na Bi. Bhutto, rais Musharraf hataki hali ya utatanishi inayoweza kusababishwa na kurudi nyumbani kwa Bw. Sharif itokee.
Tume ya uchaguzi ya Pakistan tarehe 29 Septemba ilithitibisha sifa za wagombea 6 wa urais, akiwemo Bw. Musharraf. Kati ya wagombea hao, Bw. Chaudry Hussain ambaye ni spika wa bunge la Pakistan alijitoa kwenye uchaguzi huo tarehe 1 Oktoba, na wagombea wengine wenye nguvu zaidi ni jaji wa zamani wa mahakama kuu Wajihuddin Ahmad na Bw. Amin Faim, ambaye ni naibu mwenyekiti wa chama cha PPP. Lakini wachambuzi wanasema hawana uwezo wa kushindana na Bw. Musharraf.
Kwa mujibu wa katiba ya Pakistan, rais anachaguliwa na wabunge wapatao 1,170. Hivi sasa chama tawala na washirika wake vinachukua asilimia 55 ya viti vya bunge, na Bw. Musharraf anagombea urais kwa tiketi ya vyama hivyo.
|