Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-08 14:50:49    
Mpiga piano mashuhuri wa China Yin Chengzong

cri

Mpiga piano mashuhuri wa China Bw. Yin Chengzong ana umri wa miwaka 66, alipokuwa na umri wa miaka kumi na zaidi aliwahi kupata tuzo katika mashindano ya kimataifa ya muziki wa piano. Katika miaka ya 50 na 60 alianza kuwajulisha wakazi wa kawaida muziki wa Kimagharibi na huku akianza kupiga muziki wa Kichina kwa piano.

Bw. Yin Chengzong alizaliwa mwaka 1941 katika kisiwa cha Gulangyu mjini Xiamen, mji uliopo kwenye pwani ya kusini mashariki ya China. Wakati huo mji huo ulikuwa unamilikiwa na nchi za nje. Alipokuwa mtoto alikuwa mara kwa mara alikuwa anasikia muziki kutoka kanisani kila alipocheza barabarani, hali hiyo ilimfanya aanze kupenda muziki. Alipopata tu bahati ya kusikia mtu fulani akipiga piano, aliweza kukaa pembeni yake na kusikiliza siku nzima. Kutokana na kuwa hali ya nyumbani haikumruhusu kupata mwalimu wa kumfundisha, alikuwa anajifunza mwenyewe na mwishowe alijipatia ujuzi wa kupiga piano. Baadaye kutokana na kuhamasishwa na mwalimu mmoja wa muziki, aliamua kwenda mjini kujifunza muziki. Safari ya kwenda Shanghai ilikuwa ngumu sana lakini hii ilikuwa ni hatua ya kubadilisha maisha yake. Alisema,

"Kisiwa cha Gulangyu ni sehemu inayolea wanamuziki wa piano, lakini wakati huo huko hapakuwa na walimu hasa wa upigaji piano, ukitaka kuwa mpigaji ni lazima ujifunze mahali pengine. Hali ya usafiri ilikuwa ngumu sana, hapakuwa na basi, meli, ndege wala garimoshi. Nilisafiri siku nne kwa lori kabla sijaona garimoshi. Safari yangu ilikuwa ni hatua muhimu sana kwa maisha yangu, kama nisingeondoka huko, pengine hivi sasa ningekuwa shabiki tu wa muziki wa piano."

Bw. Yin Chengzong alijifunza rasmi kwenye shule ya muziki iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai na baada ya juhudi za miaka kadhaa aliibuka na kuwa na mafanikio makubwa. Mwaka 1959 alipata nafasi ya kwanza katika mashindano ya kimataifa ya wapiga piano vijana yaliyofanyika huko Vienna. Nafasi hiyo ilimtia moyo na baada ya miaka miwili alipata fursa ya kwenda kusoma nchini Urusi kuendeleza upigaji wake katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Leningrad. Mwaka 1962 alipata nafasi ya pili katika mashindano ya kimataifa ya piano ya Tchaikovsky.

"Nilikwenda Urusi kujiendeleza kwa upigaji wa piano baada ya kutumwa na serikali, wakati huo wa miaka ya 60 Urusi ilikuwa ni nchi iliyokuwa na kiwango cha juu zaidi duniani katika sanaa, kwa hiyo hiyo ilikuwa ni fursa nzuri kwangu mimi kupanua upeo wa macho."

Baada ya kurudi nyumbani kutoka Urusi, hayati mwenyekiti Mao Zedong alimpokea na kumhamasisha astawishe muziki wa Kichina kwa piano. Mwaka 1969 alitunga koncheto ya piano "Mto Huanghe".

Ili kutunga muziki huo, Bw. Yin Chengzong alikwenda kwenye mto Huanghe, alifanya kazi pamoja na wapiga makasia na kuhisi mwenyewe machafuko makali ya maji ya mto huo yanavyokwenda kwa kasi na muungurumo. Kabla ya kukamilisha muziki huo Bw. Yin Chengzong alijifungia chumbani kwa siku tatu akizama katika utungaji, kila siku alikuwa anakula tambi za haraka tu. Kabla ya kuonesha hadharani muziki huo bahati mbaya vidole vyake vilikuwa vimevimba, ili aweze kuonesha muziki huo kwa wakati uliopangwa kila siku alitia vidole ndani ya maji ya dawa. Maonesho ya muziki huo yalipata mafanikio makubwa, wasikilizaji walifurahi kutokana na fikra zilizoelezwa katika muziki huo. Katika miongo kadhaa ya baadaye muziki huo ulikuwa muziki wake uliovutia zaidi. Mwaka 2005 miaka 60 ya ushindi wa vita dhidi ya Ufashisti ilipoadhimishwa, nchi zaidi ya 50 duniani zilitangaza au kupiga muziki huo.

Mwaka 1983 Yin Chengzong alihamia Marekani. Mwanzoni alipokuwa Marekani maisha yake yalikuwa magumu. Kwa sababu ya kuhofia kuwasumbua majirani alipofanya mazoezi ya piano, alihama mara kadhaa kabla ya kupata mahali panapofaa. Kila alipofanya mazoezi ya muziki sauti ya piano ilikuwa inawasimamisha wapita njia na alipomaliza alikuwa anasikia makofi yakipigwa nje ya dirisha. Yin Chengzong alisema maisha ya huko Marekani yalimpanulia njia ya sanaa yake. Alisema,

"Hivi leo New York ni kitovu cha utamaduni duniani. Wasanii wengi wa piano na bendi hodari kutoka nchi mbalimbali wanakusanyika huko, katika mji huo licha ya kuweza kuwasiliana na wanamuziki niliowafahamu wa Urusi pia naweza kuwasiliana na wanamuziki wengine waliotoka nchi tofauti. Huu ni mwanzo wangu mpya."

Nchini Marekani aliwahi kufanya maonesho binafsi ya muziki wa piano mara mbili katika jumba la muziki la Carnegie mjini New York, alisifiwa kuwa ni "mpiga piano hodari kabisa wa China". Aliwahi kufanya maonesho ya kuzunguka nchini humo na amekuwa profesa wa Chuo Kikuu cha Muziki cha Ceveland.

Bw. Yin Chengzong alipokumbuka njia aliyopita alisema, kila mtu ana upendo wake, na upendo huo ndio nguvu iliyomhamasisha kuendelea na safari yake yenye shida nyingi. Alipokuwa katika hali ya shida, alipokaa tu mbele ya piano alikuwa anasahau usumbufu wote. Aliwafundisha wanafunzi wake wasiwe na tamaa ya umaarufu wala maslahi binafsi, bali wawe na nia imara mpaka mwisho, huu ndio msingi wa kupata mafanikio.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-08