Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-08 18:57:13    
Ziwa Qinghai: maskani ya pamoja ya ndege na binadamu

cri

Mkoa wa Qinghai uliopo magharibi mwa China unajulikana duniani kutokana na kuwa na vyanzo vya mito muhimu barani Asia, mito hiyo ni pamoja na Mto Changjiang na Mto Huanghe ambayo ni mito mikubwa ya kwanza na ya pili nchini China, na Mto Mekong unaopita kwenye nchi mbalimbali za kusini mashariki ya Asia. Mazingira ya asili katika hifadhi ya vyanzo vya mito hiyo mitatu yanahusiana moja kwa moja na maisha ya nusu ya idadi ya watu duniani. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China katika ngazi mbalimbali na watu wake wamekuwa wakifanya juhudi za kuboresha na kuhifadhi mazingira ya huko, hivi sasa juhudi hizo zimepata mafanikio na mazingira ya asili mkoani Qinghai yameboreshwa kidhahiri.

Hivi karibuni waandishi wetu wa habari walitembelea mkoa wa Qinghai na kuandaa vipindi mfululizo. Sasa sikilizeni maelezo yasemayo: Ziwa Qinghai ni maskani ya pamoja ya ndege na binadamu. Karibuni.

Mwezi Februari kila mwaka, ndege wanaohamahama wa aina zaidi ya 10 huwa wanaanza kusafiri kutoka sehemu ya kusini ya China na kusini mashariki ya Asia wakielekea sehemu ya kaskazini. Mwisho wa safari hiyo ni Ziwa Qinghai lililopo mkoani Qinghai. Ziwa hilo maarufu linalopendeza kabisa nchini China, limekuwa kama dunia ya ndege, na eneo wanakoishi kwa ndege hao wengi linalojulikana kama kisiwa cha ndege na kuwa maskani ya pamoja ya ndege na binadamu.

Naibu mkurugenzi wa Idara ya usimamizi ya hifadhi ya Ziwa Qinghai Bw. He Yubang alisema "Katika kisiwa cha ndege, watu wanaambiwa kuacha nyayo na kuchukua furaha tu. Hapa hakuna majengo ya kisasa kama vile hoteli na mikahawa, badala yake kuna sura ya asili ya maumbile."

Ziwa Qinghai lenye eneo la kilomita za mraba 4,300 ni ziwa kubwa la maji ya chumvi kuliko maziwa mengine hapa nchini China, vile vile ni eneo oevu muhimu ambalo kila mwaka ndege wanaohama laki kadhaa wanakwenda kuishi huko. Awali kulikuwa na kisiwa kidogo maarufu kama kisiwa cha mayai kutokana na ndege wengi kutagia mayai huko kisiwani. Lakini tangu miaka ya 1970, kutokana na kupungua kwa kina cha maji ya ziwa, kisiwa cha mayai kilianza kuungana na ardhi, na watu wengi walikuwa wanakwenda kisiwani kuchukua mayai ya ndege. Shughuli za binadamu zilisababisha kupungua sana kwa idadi ya ndege, kiasi kwamba ndege 200 tu waliishi huko kisiwani wakati fulani.

Mwaka 1975 mkoa wa Qinghai ulifanya kisiwa cha ndege kiwe ndani ya hifadhi ya mazingira ya asili na kulindwa na walinzi. Hadi kufikia mwaka 1997 serikali kuu ya China iliamua kuanzisha hifadhi ya ziwa Qinghai yenye eneo la hekta zaidi ya 495,000, na kisiwa cha ndege ni sehemu ya hifadhi hiyo.

Katika miaka ya hivi karibuni idadi ya ndege na mimea imekuwa inaongezeka pole pole katika Ziwa Qinghai. Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa ndege wanaohamahama wapatao elfu 50 hivi wanakwenda kuishi katika kisiwa cha ndege kila mwaka.

Kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya ndege wanaohamahama, watalii wengi pia wanakuja. Tangu mwaka 2003, kwa wastani watalii laki moja wanatembelea kisiwa cha ndege kila mwaka.

Bw. Li Shehui, mke wake na binti yao mwenye umri wa miaka 6 wanatoka Xian, mji wa kaskazini magharibi mwa China, wao ni miongoni mwa watalii wanaovutiwa na kisiwa cha ndege. Mtoto wao anayeishi mjini hajawahi kuona ndege wengi namna hii, alifurahi sana. Bw. Li alisema  "Tunatoka mji wa Xian, kutembelea kisiwa cha ndege ili mtoto wetu apate fursa ya kuangalia ndege wengi. Nilimwambia mtoto kuwa, ndege wanaishi hapa, na sisi binadamu kuhifadhi mazingira ni sawa na kuwahifadhi ndege hao, kwani wanaishi pamoja na binadamu."

Ziwa Qinghai lipo kwenye uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet, ambapo ni sehemu inayokabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa duniani. Kwa hiyo inapaswa kuzingatia suala la hifadhi ya mazingira katika kuendeleza shughuli za utalii huko.

Naibu mkurugenzi wa Idara ya utalii ya mkoa wa Qinghai Bw. Xu Hao alisema wazi kuwa, kamwe binadamu hawaruhusiwei kuharibu mazingira kwa ajili ya kuendeleza utalii. Alisema "Tunaona ni lazima kuendeleza utalii kwa taratibu kwenye mazingira mazuri ya asili. Ziwa Qinghai lina mandhari nzuri maalumu, kamwe haturuhusu mandhari hiyo iharibike au kupotea kabisa. Kwa upande mwingie, kama siku moja mazingira ya huko yataharibika, italeta matokeo mabaya kiasi kwamba binadamu wenyewe hawataweza kuendelea kuishi huko."

Kuhusu uhusiano kati ya utalii na hifadhi ya mazingira, kijana Zheng Liang ambaye ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Qinghua cha China anayefanya uchunguzi katika Ziwa Qinghai, alitoa maoni yake. Akisema "Naona inafaa vitu hivyo viwili visaidiane. Hatuwezi kuwazuia watu wasitembelee sehemu fulani kwa ajili ya kuhifadhi mazingira ya huko, wala haifai kuharibu mazingira kutokana na kuendeleza shughuli za utalii."

Katika juhudi za kuhifadhi ndege, hatua mbalimbali zimechukuliwa, kama vile watalii kutoruhusiwa kuingia kwenye sehemu ya katikati ya kisiwa cha ndege, na shughuli za watu ni lazima zifuate kanuni kwa makini. Watalii wanapaswa kutembea kwa kutumia magari ya umeme kwa kufuata njia zilizowekwa za utalii, na wanaweza tu kuangalia ndege wakiwa kando ya kisiwa.

Naibu mkuu wa Idara ya usimamizi wa hifadhi ya Ziwa Qinghai Bw. He Yubang alisema  "Umbali kati ya watalii na ndege usiwe karibu. Watalii kusimama kwenye kundi la ndege si hali yenye masikilizano, bali ina athari kubwa kwa ndege."

Ili kuondoa athari ya shughuli za binadamu kwa ndege, kwenye kisiwa cha mayai watalii wanapaswa kuangalia ndege kwenye ngome iliyojengwa chini ya ardhi, ambayo paa la ngome hiyo linafunikwa kwa nyasi na kuifanya ngome hiyo ionekane kama sehemu ya maumbile. Hatua hiyo ina lengo la kuwafanya ndege wasiwaone watalii.

Kuangalia kutoka kwenye ngome hiyo kunawafanya watalii wasiwe na furaha ya kutosha, lakini hatua hiyo inakubaliwa na watalii wengi kabisa. Mtalii kutoka mji wa Xian, China Bw. Li Shehui alisema "Hatua hiyo ina lengo la kutoathiri maisha ya ndege ili waweze kuzaliana na kulea vifaranga vyao kwenye mazingira ya asili. Naunga mkono hatua hiyo, naona huu ni mfano mzuri unaostahili kuigwa."

Kila mwaka maua yanapochanua ndege wanaohamahama wanaambatana kufika kwenye Ziwa Qinghai kuzaliana, na mwezi Septemba ndege hao pamoja na vifaranga vyao wanaanza kurudi kwenye sehemu ya kusini. Siku nenda siku rudi, hali hii inaendelea kuonekana kwenye Ziwa Qinghai.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-09