|
Ukitembea barabarani huko Baghdad, mji mkuu wa Iraq, ukiambiwa chukua tahadhari juu ya mabomu yaliyotegwa kando ya barabara pamoja na kampuni binafsi za usalama za Marekani, si mzaha wala jambo la kuchekesha, bali hii ni hali ilivyo sasa inayowatia watu wasiwasi mkubwa. Tangu Marekani ianzishe vita vya Iraq mwaka 2003, yametokea matukio mbalimbali ya watu walioajiriwa na kampuni za usalama za Marekani kuwaua raia wa Iraq kwa makusudi. Tukio la kampuni ya usalama ya "Black Water" kuua raia 11 wa Iraq tarehe 16, Septemba mjini Baghdad ni moja ya matukio mbalimbali kama hayo, ambalo limefichuliwa hivi karibuni tu.
Kutokana na taarifa ya uchunguzi iliyotolewa na bunge la Marekani, tokea mwaka 2005 watu wa kampuni ya usalama ya "Black Water" walijihusisha na matukio 195 ya mashambulizi ya risasi nchini Iraq pamoja na matukio zaidi ya 160 ya matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Kabla ya kutokea kwa tukio hilo, serikali ya Marekani ilikuwa inafumbia macho tu mauaji yaliyofanywa ovyo na kampuni binafsi za usalama za Marekani. Kufuatia kufichuliwa kwa tukio hilo la "Black Water", Marekani haina budi kutangaza wazi kuwa, watu wa kampuni hiyo walichukua hatua kali za kupita kiasi. Ili kutuliza tukio hilo Marekani ilianzisha uchunguzi wa kisheria juu ya tukio hilo. Hata hivyo wachambuzi wanadhihirisha kuwa, hatua zilizochukuliwa na serikali ya Marekani zinaonesha kuwa, haina nia ya kuacha kuwalinda watu wa kampuni ya "Black Water" ili wasifikishwe mahakamani nchini Iraq.
Mbali na hayo tukio hilo ni sehemu ndogo tu ya mauaji yaliyofanywa na watu wa kampuni za usalama za Marekani nchini Iraq, pia ni matokeo ya sera ya umwamba inayofuatwa na Marekani. Baada ya Marekani kuanza kuikalia Iraq, mfumo wa kisheria ulijengwa upya nchini Iraq, na kutokana na mfumo huo, maslahi ya Marekani na sheria nchini Marekani yamewekwa juu ya mamlaka ya nchi ya Iraq.
Kwa mfano agizo No. 17 lililotungwa na wakaliaji wa jeshi la Marekani nchini Iraq, lina vifungu vya kutoa haki ya kinga kwa kampuni za usalama za nchi za nje nchini Iraq. Kwa upande mwingine kutokana na sheria ya Marekani, ni kampuni za usalama zinazoajiriwa na wizara ya ulinzi ya Marekani tu ndizo zinazochukuliwa hatua za kisheria zikitenda makosa, lakini kampuni nyingine binafsi za usalama mfano wa kampuni ya "Black Water" zinazoajiriwa na wizara ya mambo ya nje na idara nyingine za serikali ya Marekani, zinanufaika kihalisi na haki hiyo ya kinga.
Mwandishi wa habari wa gazeti la Newsweek Bw. Mikel Hursh kwenye makala yake anasema, kuhusu shughuli za kijeshi nchini Iraq, Marekani inafuata kanuni inayotambuliwa ambayo haijatangazwa wazi, yaani kuwadhani Wairaq wote kama magaidi, kwa hiyo inapaswa kuchukua hatua kwanza dhidi yao, ama kuwakamata ama kuwaua. Kutokana na mantiki kama hii ambayo msingi wake ni umwamba na nguvu kali, si ajabu ikaonekana kuwa watu wa kampuni binafsi za usalama za Marekani wanaweza kufanya mambo kama wanavyopenda. Ndiyo maana ni serikali ya Marekani yenyewe ndiyo inayostahili kuwajibika na tukio la "Black Water".
|