|
Kikundi cha maandalizi ya mazungumzo kati ya Palestina na Israel kilifanya mkutano tarehe 8 huko Jerusalem kuhusu mswada wa taarifa ya pamoja ya mkutano wa kimataifa wa suala la Mashariki ya Kati. Kikundi hicho kimeundwa kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya viongozi wa Palestina na Israel tarehe 10 Septemba. Katika kikundi hicho wajumbe wa upande wa Israel ni mkurugenzi wa ofisi ya waziri mkuu Bw. Yoram Turbowitz, mshauri wa mambo ya nje wa waziri mkuu Shalom Turgeman na mkuu wa ofisi za wizara ya mambo ya nje Bw. Aharon Abramovich; na wajumbe wa upande wa Palestina ni waziri mkuu wa zamani Bw. Ahmed Qureia na mjumbe wa kwanza wa mazungumzo Bw. Saeb Erekat na msaidizi wa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Yasser Abed Rabbo. Kwenye mazungumzo ya viongozi yaliyofanyika tarehe 3 mwezi huu kati ya Palestina na Israel, wajumbe wa kikundi hicho kwa mara ya kwanza walikutana na kufanya mazungumzo ya mwanzo kuhusu mswada wa taarifa ya pamoja. Baada ya mazungumzo Bw. Abbas na waziri mkuu wa Israel waliamua kikundi hicho kianze majadiliano kuhusu taarifa ya pamoja licha ya viongozi wa pande mbili kuendelea na mazungumzo mara mbili kila mwezi. Lakini wachambuzi wanaona kuwa kikundi hicho kitakumbwa na matatizo mengi.
Kwenye mazungumzo ya viongozi wa Palestina na Israel yaliyofanyika hivi karibuni, pande mbili ziliona mkutano wa kimataifa utakaofanyika mwezi Novemba kuhusu suala la Mashariki ya Kati, ni hatua moja katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati wala sio hatua ya mwisho, na pande mbili zimekubali kwamba ratiba halisi ya kutatua matatizo muhimu ya mipaka, hatma ya Jerusalem, wakimbizi na usalama wa Israel itaanza baada ya mkutano huo wa kimataifa. Hii inamaanisha kwamba pande mbili zinazingatia kuleta mazingira mazuri kwa ajili ya mazungumzo ya amani, na pia inaonesha kuwa mazungumzo kuhusu matatizo hayo muhimu yatakuwa magumu, na hii ndio sababu mojawapo ambayo tofauti kati ya Palestina na Israel kuhusu taarifa ya pamoja hazijaondolewa, ingawa walifanya mazungumzo mara sita katika miezi kadhaa iliyopita. Kutokana na kuwa ni lazima pande mbili zilegeze masharti ambayo hapo kabla ilikuwa ni vigumu kuyaacha, na shinikizo kubwa la nchini na uwezo wa serikali ni dhaifu, kama tahadhari isipochukuliwa mazungumzo hayo yanaweza kuvunjika wakati wowote.
Kuhusu suala la mipaka, Palestina inatetea iwe juu ya msingi wa kabla ya vita vya mwaka 1967, na maeneo ya ardhi yawe na 2-3% ya sehemu ya magharibi ya Mto wa Jordan, na Israel ni lazima isimamishe ujenzi wa makazi wa Wayahudi na kuondoka kutoka ukingo wa magharibi na kuifanya sehemu ya magharibi ya Mto wa Jordan isitenganishwe ardhi ya Palestina. Lakini Israel inataka Palestina izingatie sehemu yenye makazi mengi ya Wayahudi katika masuala ya mipaka na ugawaji wa ardhi.
Kuhusu suala la Jerusalem, Palestina inatetea sehemu ya mashariki ya Jerusalem ikiwa ni pamoja na mtaa wa zamani wa mji huo iwe mji mkuu wa Palestina na inataka iwe na mamlaka kamili kuhusu sehemu hiyo. Lakini Israel ina msimamo imara kuhusu mamlaka ya mji mzima wa Jerusalem baada ya vita vya mwaka 1967 kuiteka sehemu ya mashariki ya Jerusalem na ilipitisha sheria ya kutangaza mji wa Jerusalem kuwa ni mji mkuu wa Israel. Hivi karibuni naibu waziri mkuu wa Israel Bw Haim Ramon alitoa ushauri wa kuirudishia Palestina sehemu ya mashariki ya Jerusalem ambayo wanaishi Waarabu wengi, lakini ushauri ulipotolewa tu ulipingwa vikali mara moja. Kuhusu suala la wakimbizi, Palestina inaona kuwa Israel ni lazima itambue haki ya wakimbizi kurudi nyumbani, lakini Israel haitaki wakimbizi hao warudi kutokana na sababu za usalama wa taifa.
Kutokana na hali hiyo, wachambuzi wanaona kuwa ingawa kikundi cha maandalizi ya mazungumzo tarehe 8 kilianza kugusia matatizo hayo muhimu na kutafuta ufumbuzi, lakini mazungumzo hakika yatakuwa magumu, hali ya "vuta nikuvute" ili kila upande unufaike itakuwa ngumu.
Idhaa ya kiswahili 2007-10-09
|