|
Habari zilizochapishwa kwenye gazeti moja kubwa la mjini Tokyo, toleo la tarehe 10 mwezi Oktoba zinasema, waziri mkuu wa Japan Bw. Yasuo Fukuda katika mkutano wa majadiliano wa kamati ya bajeti ya baraza la chini na bunge la Japan, alieleza msimamo wake wa kupinga kutumia "haki ya kujihami kwa pamoja", msimamo huo wa Bw Yasuo Fukuda ni tofauti na ule wa waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo Bw. Shinzo Abe, ambaye alitaka kufikia lengo la kutumia "haki ya kujihami kwa pamoja" kwa kuhimiza marekebisho ya katiba ya nchi.
Katika mazungumzo hayo Bw. Fukuda Yasua alisema, kutokana na ukomo wa shughuli za kimataifa ulioagizwa katika maelezo ya ufafanuzi wa katiba ya nchi, wanapaswa kujadili kwa makini, na tena kwa uangalifu mkubwa. Maoni yake ni tofauti kabisa na msimamo wa waziri mkuu wa zamani wa Japan Bw. Shinzo Abe. Baada ya Bw Shinzo Abe kushika madaraka ya serikali, alichukulia kuachana na mfumo ule wa baada ya vita, kubuni katiba mpya na kuhimiza utumiaji wa "haki za kujihami kwa pamoja" kuwa ni sera zake muhimu, na kuziendeleza katika pande mbalimbali. Vitendo vya Bw Abe vilikosolewa sana na vyombo vya habari vya baadhi ya nchi ikiwemo Korea ya Kusini. Gazeti la Dong-a Ilbo liliwahi kutoa makala ya maoni ya mhariri mwezi Agosti mwaka huu ikikosoa kuwa, vitendo hivyo vya Japan vinafanya watu kuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa sehemu ya Asia ya kaskazini, endapo Japan haitaki kufanya tena vitendo vya mashambulizi kama vile ilivyofanya katika historia, basi inapaswa isiguse hata kidogo katiba ya amani.
"Haki ya kujihami kwa pamoja" inasema, wakati nchi zenye uhusiano mkubwa na Japan zinaposhambuliwa kwa silaha na nchi nyingine, Japan ina haki ya kuizuia bila hata kujali kama Japan yenyewe inashambuliwa. kwa kufuata kanuni ya kifungu cha 51 cha katiba ya Umoja wa Mataifa iliyotungwa mwaka 1945, nchi yenye mamlaka ina "haki kabisa ya kujihami peke yake au kujihami kwa pamoja", kifungu hicho kilikuwa msingi wa kisheria kwa Marekani na Urusi ya zamani ya kuunda jumuiya ya NATO na jumuiya ya mkataba wa Warsaw. Baada ya vita baridi kwisha, wazo hilo la "haki ya kujihami kwa pamoja" nchini Japan, linaonekana zaidi katika uhusiano wa washirika wa Japan na Marekani, hasa baada ya tukio la mashambulizi ya kigaidi la "tarehe 11 Septemba", Marekani mara kwa mara iliitaka Japan itumie "haki ya kujihami kwa pamoja".
Wachambuzi wanasema, msimamo wa Bw. Fukuda unalingana na wazo lake la kisiasa la kufuata njia isiyopendelea upande wowote. Mwanzoni baada ya Bw. Fukuda kuingia madarakani, alieleza wazi kuwa hatakwenda kwenye hekalu la Yasukuni kuwaombea mizimu ya wahalifu wa vita; katika hotuba yake kuhusu utekelezaji wa sera za utawala, licha ya kusisitiza kuwa uhusiano wa washirika wa Japan na Marekani pamoja na ushirikiano wa kimataifa ni msingi wa shughuli za kidiplomasia za Japan, alitaka kuhimiza kwa nguvu shughuli za kidiplomasia za Asia, na kuunda uhusiano wa kunufaishana na uaminifu pamoja na nchi jirani za China na Korea ya Kusini; Katika hutoba yake kuhusu sera zake za utawala, Bw. Fukuda hakutaja hata neno moja kuhusu kuhimiza marekebisho ya katiba ya nchi. Yote hayo yamedhihirisha kuwa Bw. Fukuda anafuata njia ya kisiasa ya utulivu na kudumisha uhusiano wa mapatano na nchi jirani.
Kwa upande mwingine, maelezo aliyotoa Bw. Fukuda ni kufuata maoni ya umma wa Japan. Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni na vyombo vya habari vya Japan ikiwemo Kyodo Tsushin unaonesha kuwa, zaidi ya nusu ya watu wa Japan wanaona kuwa hakuna haja ya kubadilisha katiba ya nchi ya hivi sasa; Na zaidi ya nusu ya idadi ya watu wa Japan wanapinga kutumia "haki ya kujihami kwa pamoja".
Lakini Bw. Yasuo Fukuda anakabiliwa na shinikizo kubwa katika utekelezaji wa msimamo huo. Kwanza, Marekani inaitarajia kuwa Japan itatumia mapema "haki ya kujihami kwa pamoja". Pili, nguvu inayoshikilia mambo ya zamani nchini Japan inaendelea kuunga mkono matumizi ya "haki ya kujihami kwa pamoja".
|