Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-15 16:01:25    
Moja ya mbinu 36, Kuondoa kuni chini ya sufuria

cri

"Kuondoa kuni chini ya sufuria" ni moja ya mbinu 36 za kivita, na pia ni msemo wa kawaida wa Kichina, maana yake ni kwamba ukitaka kupooza maji yanayochemka ndani ya sufuria ni bora uondoe kuni zinazowaka chini ya sufuria kuliko kutia maji baridi, ikiwa na maana ya kutatua kikamilifu tatizo. Katika mambo ya vita, wataalamu wanaona kwamba maji yanachemka kutokana na kupashwa moto, na maji yanayochemka na moto vyote ni vitu vya kuumiza, lakini kuni zinaweza kuondolewa kwa mikono. Kwa hiyo unapopambana na maadui wenye nguvu kubwa, hakika utapata hasara kubwa na huenda utashindwa vibaya, wakati huo ni busara ukwepe nguvu kubwa ya maadui, na ushambulie sehemu dhaifu ya maadui kwa kutumia fursa nzuri ili kupunguza nguvu za maadui. Njia za kudhoofisha nguvu za maadui kwa kushambulia sehemu dhaifu ni nyingi, kwa mfano, kuvunja ari ya maadui ya mapambano kwa kufanya mashambulizi kisaikolojia, kushambulia vituo vya maadui vilivyo nyuma ya medani, ghala, kukata njia za uchukuzi wa maadui na njia wanazopita askari wanaokwenda kutoa msaada. Yote hayo ni kama "kuondoa kuni chini ya sufuria". Katika mazingira tofauti zikitumika mbinu kama hizo zinaweza kuleta matokeo mazuri.

Katika Enzi ya Song, karne ya kumi nchini China, kulikuwa na afisa mmoja aliyeitwa Xue Changru. Siku moja uasi ulizuka katika wilaya aliyotawala, waasi waliwaua maofisa wengi na hata walichoma moto makao ya serikali, maafisa wote walishikwa na hofu bila kuthubutu kujitokeza ila Xue Changru tu ambaye peke yake alikwenda ndani ya kambi za waasi, kwa ukali aliwakemea waasi akisema, "Nyie mna wazazi na watoto, mkiendelea na uasi licha ya kuwa hamtapata mwisho mwema pia mtawaathiri jamaa zenu, janga litakuwa kubwa. Lakini mkiweka chini silaha, nitawasamehe bila adhabu yoyote." Miongoni mwa waasi, wengi walifuata uasi kwa kulazimishwa, walipomsikia Xue Changru aliyosema watu hao walionekana kuyumbayumba, Baada ya kugundua hali hiyo, Xue Changru aliendelea, "Sasa, watu wanaotaka kufanya uasi wasimame upande wa kushoto, na wasiotaka wasimame upande wa kulia." Baada ya kusikia hayo waasi mia kadhaa wote walisimama upande wa kulia, kwa kuona hali hiyo viongozi wa waasi walikimbia na kujificha kwenye vijiji vya karibu. Xue Changru aliongoza askari kuwasaka na kuwahamasisha wanavijiji watoe ripoti juu yao, baadaye viongozi hao walikamatwa.

Katika tukio hilo, Xue Changru alitumia vizuri mbinu ya "kuondoa kuni chini ya sufuria". Mbele ya Xue Changru nguvu za waasi zilikuwa kubwa, lakini mbele ya serikali ya wilaya jamaa wa waasi ni wanyonge, kwanza Xue Changru aliwatahadharisha waasi matokeo mabaya watakayopata kama wakiendelea na uasi, kisha aliwaambia wanaweza kusamehewa kama wataacha uasi, hivyo aliwavuta waliolazimishwa kufanya uasi kwenye upande wake na kuwatenga viongozi wachache, ari ya waasi ya kufanya uasi ilivunjika, na viongozi waliokuwa wamepoteza uungaji mkono walikuwa hawana budi ila kutoroka.

Cha muhimu katika matumizi ya mbinu hiyo ni kugundua na kushambulia sehemu zinazoathiri hali nzima ya vita. Kuna mifano mingi ya matumizi ya mbinu hiyo nchini China na katika nchi za nje, na katika zama hizi na za zamani. Wakati pande mbili zinapokabiliana bila upande mmoja kuweza kuushinda upande mwingine, au upande mmoja unapozidiwa sana na upande mwingine, mbinu ya kushambulia sehemu ya nyuma ya medani, kunyakua akiba ya zana, kuvunja ari ya maadui ya kupambana, kukata njia nyuma za maadui, huwa zinaleta matokeo mazuri. Mbinu kama hizo ndio mbinu za "kuondoa kuni chini ya sufuria".

Katika jamii ya leo, mbinu hiyo pia mara kwa mara inatumika. Kwa mfano, katika kipindi kilichopita kutokana na kuwekeza sana kwa kutumia mikopo kutoka benki, biashara ya viwanja na nyumba ilikua haraka kupita kiasi, hali hiyo isiyo ya kawaida inaweza kusababisha mfumuko wa bei, kwa hiyo benki kuu ya China ilichukua hatua za kuongeza riba ya mikopo, biashara ya nyumba na viwanja mara ilipungua.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-15