Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-15 16:15:04    
Utalii kwenye ziwa zuri la Mwezi

cri

Katika lugha ya Kimongolia, "tenggeli" maana yake ni mbingu, na "dalai" ni ziwa. Kwa hiyo ziwa la mwezi la Tenggelidalai ni "ziwa zuri lililoko karibu na bahari ya mbinguni". Kwa kuwa umbo lake ni kama mwezi unaoandama, hivyo linaitwa na wakazi wa huko kuwa ni ziwa la mwezi.

Wilaya ya Alashan, ambayo ni sehemu liliko ziwa la mwezi, unavuma upepo unaopeperusha mchanga na vumbi mara kwa mara, sehemu hiyo ni ya kame, na ni nadra sana kwa mvua kunyesha kwenye sehemu hiyo. Siku nyingi zina jua kali, hivyo hata maji yanayopotea kutokana na jua ni mengi. Jangwa la Tengeli ni la nne kwa ukubwa nchini China, na pia ni jangwa linalohamahama kwa haraka. Katika mazingira ya namna hiyo, ziwa la mwezi ni kitu chenye thamani kubwa zaidi kwenye sehemu hiyo.

mwimbaji aliyeimba wimbo huu ni mzee, jina lake linaitwa Butugeqi, yeye alikuwa ni mwalimu, baada ya kustaafu kazi ya ualimu, alikwenda kufanya kazi nyingine kwenye ziwa la mwezi. Kila walipofika watalii, mara tu baada ya kushuka kutoka kwenye boti, mzee Butugeqi na wafugaji wengine huwa wanaimba "wimbo wa kukaribisha wageni" wenye umaalumu wa kabila la wamongolia, na kuwakaribisha kwa kuwapa vitambaa vyeupe vinavyoonesha heshima pamoja na pombe tamu.

Kwenye ziwa la mwezi, maji maangavu yanaonekana, maua ya matete yanayumbayumba kutokana na upepo, na bata mwitu wanacheza kwa furaha kwenye maji. Baada ya kupita kwenye daraja la mbao, na kutembea kwenye matete, watalii wanaweza kujisahau kama hivi sasa wako katikati ya jangwa, wakidhani kuwa wamefika kwenye sehemu yenye ziwa ya kusini mwa China. Lakini wanapoona vilima vingi vya mchanga, wanavutiwa sana na picha moja nzuri ya kipekee ya sehemu ya ziwa la mwezi.

Watalii wengi waliofika kwenye ziwa la mwezi, hushangazwa sana na uzuri wa mandhari ya sehemu ile, na wanaisifu sana mandhari ile nzuri. Mtalii mmoja kutoka sehemu ya kaskazini magharibi ya China, Bw. Wang Ming alisema,

"kila tunapofika hapa tunafurahi sana, mioyoni mwetu kumejaa furaha. Baada ya kufanya kazi kwa wiki moja, tunaona uchovu mwingi, lakini tukifika hapa katika wikiendi na kulala hapa kwa usiku mmoja, kesho yake tunaondoka. Tunaona uchovu umetoweka, hivyo inatusaidia kufanya vizuri kazi zetu na kudumisha moyo wa uchangamfu."

Kwenye ziwa la mwezi, licha ya kuweza kujiburudisha kwa mandhari nzuri ya maji ndani ya mashua, watalii pia wanaweza kupanda ngamia na kutembea kwenye jangwa, huu ni umaalumu wa utalii wa sehemu ya ziwa la mwezi. Wilaya ya Alashan ni mahali panapotoa ngamia bora kwa wingi, ngamia wa sehemu hiyo ni wazuri, wapole na wenye afya nzuri. Bw. Sunbuer ni mmoja wa wafugaji wa ngamia kwenye sehemu ya ziwa la mwezi, amefanya shughuli hiyo kwa miaka 7. Kabla ya kufanya kazi huko, alifanya shughuli ya ufugaji pia huko kwao. Alisema,

"Nyumbani kwetu na kwenye ziwa la mwezi kuna umbali wa kilomita 60, tokea mwezi Mei hadi mwezi Oktoba, familia yetu inaleta ngamia kwenye ziwa la mwezi na kufanya kazi hapa. Wakati mwingine tunaishi kwenye maskani yetu wenyewe. Mwanzoni tulipoanza kufanya kazi kwenye ziwa la mwezi, tulikuwa na ngamia watano au sita hivi. Hivi sasa kutokana na uungaji mkono wa sehemu ya mandhari ya ziwa la mwezi, idadi ya ngamia wetu imeongezeka na kuwa zaidi ya 30. Mwaka huu watalii wengi wamefika hapa, ingawa hatuna ngamia wengi, lakini pato letu si dogo, na kiwango cha maisha yetu kimeinuka."

Licha ya ngamia, magari ya jeep pia ni chombo muhimu cha usafiri kwenye jangwa, na kusafiri kwa kutumia magari hayo ni mchezo wa kujifurahisha katika sehemu ile. Kupita kwenye njia iliyopangwa kwa magari, watu wanaona furaha kubwa kama katika mchezo wa kuzunguka kwenye njia reli ndogo. Mchezo wa aina hiyo uko kwenye sehemu hiyo moja tu kwa China bara.

Sehemu ya ziwa la mwezi iliendelezwa kuwa sehemu yenye mandhari nzuri ya utalii ya mazingira ya viumbe kwenye jangwa mwaka 2001. Sifa za sehemu hiyo ya utalii ni kuwa, imehifadhi vitu vyote vya asili vilivyoko huko. Mkurugenzi mkuu wa sehemu ya utalii ya ziwa la mwezi Bw. Song Jun alisema, ziwa la mwezi limemfahamisha umuhimu wa kuishi kwa mapatano kati ya binadamu na mazingira ya maumbile. Ana matumaini kuwa kutokana na jitihada zake, ziwa la mwezi litakuwa sehemu moja ya kuigwa kwa maeneo yenye jangwa. Bw. Song Jun alisema,

"Kuhusu ziwa la mwezi, tunataka kuweka mfano wa kuigwa wa utalii wa mazingira ya kupatana kwa viumbe. Kuhusu ushiriki wa watalii, tunataka watalii waliotembelea kwetu hapa, wawe wanafahamu maana ya mazingira ya kupatana kwa viumbe kutoka watalii wa kawaida, halafu wabadilike kuwa waungaji mkono wa mazingira ya kupatana kwa viumbe kutoka watalii wanaofahamu umuhimu wa mazingira ya aina hiyo, na hatimaye wabadilike kuwa washiriki kabisa."

Katika miaka ya hivi karibuni, ziwa la mwezi limekuwa linawavutia watalii wengi wa nchi za nje, wakiwemo wale wa kutoka Uingereza, Marekani, Canada, Japan na Korea ya Kusini. Bw. Song Jun alisema, maofisa wote wa kidiplomasia wa ubalozi wa Korea ya Kusini nchini China waliwahi kufika kwenye ziwa la mwezi. Nia yao ni kutaka kuangalia namna jangwa la huko linavyobadilika kuwa sehemu yenye mimea. Safari yao kwenye ziwa la mwezi haikuwavunja moyo.

Haya, wasikilizaji wapendwa, maelezo yetu kuhusu utalii kwenye sehemu yenye mandhari nzuri ya ziwa la mwezi yanakamilika kwa sauti nzuri ya wimbo unaoitwa "Usiku wa Mbalamwezi" ulioimbwa na vijana wa huko, wafugaji wa sehemu ya ziwa la mwezi wanatarajia kuwa siku moja utafika huko kutalii. Kipindi hiki cha safari nchini China kinaishia hapa kwa leo, tutakuwa nanyi tena wiki ijayo wakati kama huu, asanteni kwa kutusikiliza.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-15