Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-15 18:48:52    
Itakuwa ni vigumu kwa ziara ya Bi Rice kwenye sehemu ya mashariki ya kati kupata mafanikio

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi Condoleezza Rice tarehe 14 Oktoba aliwasili nchini Israel kwa ziara nyingine katika sehemu hiyo, na kuendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba nchini Marekani. Lakini vyombo vya habari vinaona kuwa, itakuwa vigumu kwa ziara hiyo ya Bi Rice kufanikiwa.

Kutokana na mpango uliowekwa, katika siku tatu zijazo Bi Rice atafanya usuluhisho kati ya Israel na Palestina. Baada ya kuwasili nchini Israel Bi Rice atakuwa na mazungumzo na waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Ehud Barak, kisha atafanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israeli Bw Ehud Olmert na waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Palestina Bw Salam Fayyad. Mbali na hayo, atajadiliana na maofisa wa ulinzi wa Israel kuhusu tukio la Israel kukalia ardhi ya Palestina iliyoko karibu na Jerusalem. Pia Bi Rice ana nia ya kuzitembelea Misri na Jordan.

Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati, ambao ulipendekezwa kufanyika na rais George Bush wa Marekani, utafunguliwa tarehe 26 mwezi Novemba nchini Marekani. Israeli, Palestina, pande nne husika za Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani na Russia, pamoja na nchi jirani za Israel na Palestina zitashiriki kwenye mkutano huo. Pande mbili za Israel na Palestina zilianza na mazungumzo tarehe 8 mwezi huu, ili kuandaa taarifa ya pamoja itakayotolewa kwenye mkutano huo. Lakini pande hizo mbili bado zina misimamo tofauti kuhusu baadhi ya masuala muhimu. Lengo la ziara hiyo ya Bi Rice ni kuendelea kupunguza tofauti ya maoni yao, ambayo ni vigumu kupatanishwa, na kutaka uungaji mkono wa nchi jirani za kiarabu juu ya mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati.

Habari zinasema katika mazungumzo ya kikundi cha kazi ya mazungumzo cha Palestina na Israel, wajumbe wa Palestina wanaendelea kutaka kutekeleza kanuni za "mambo halisi" zilizopendekezwa na mwenyekiti wa mamlaka ya taifa ya Palestina Bw Mahmoud Abbas, na kuweka ratiba ya utatuzi wa masuala muhimu ya mpaka wa mwisho wa Palestina, hadhi ya Jerusalem pamoja na haki ya kurejea kwa wakimbizi.

Kiongozi wa kazi ya mazungumzo wa upande wa Palestina ambaye ni waziri mkuu wa zamani wa Palestina Bw. Ahmed Qureia, tarehe 13 alidokeza kwenye mazungumzo kati yake na msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayeshughulikia mambo ya mashariki ya karibu Bw. David Weilch kuwa, mazungumzo rasmi ya kikundi cha kazi cha mazungumzo kati ya Palestina na Israeli yaliyoanza tarehe 8, hadi sasa bado hayajafikia makubaliano yaliyoandikwa kuhusu masuala muhimu ya mpaka, hadhi ya Jerusalem na kurejea kwa wakimbizi wa Palestina. Bw. Ahmed Qureia alisisitiza kuwa, taarifa ya pamoja ya Palestina na Israel inatakiwa kueleza kwa uwazi na ukamilifu kuhusu utatuzi wa masuala muhimu.

Endapo mkutano wa mwezi Novemba hautaweza kuweka msingi "unaoonekana wazi" kwa ajili ya amani ya Palestina na Israel, matokeo yake yatashindwa kuridhisha watu. Kabla ya hapo alisema, kama mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati utashindwa kufikia makubaliano, basi hakuna haja ya kuitisha mkutano huo. Israel imepinga kabisa matakwa ya upande wa Palestina ya kuweka ratiba ya mazungumzo. Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert tarehe 14 mwezi Oktoba kwenye mkutano wa baraza la mawaziri alisema, "Kuweka ratiba ya mazungumzo, licha ya kutoweza kutatua matatizo, kutaleta matatizo mapya". Alisema "Mazungumzo kati ya Palestina na Israel yanatakiwa kufanyika kwa utulivu na kwa uangalifu, ili kuhimiza pande mbili zifikie makubaliano kwenye taarifa ya pamoja katika muda wa mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati. Lakini taarifa hiyo kamwe isiwe sharti la kuitishwa kwa mkutano huo."

Wachambuzi wanasema, mgogoro kati ya Palestina na Israel ulisababishwa na mambo mengi ya kihistoria na ya sasa, hivyo haiwezekani kupata mafanikio makubwa katika muda wa siku chache kama anavyotarajia Bi Rice.