|
Tarehe 15 bei ya mafuta kwenye soko ya kimataifa ilipanda tena baada ya tarehe 12 kupanda na kuwa dola za Kimarekani 83,69 kwa pipa. Siku hiyo kwenye soko la New York bei ya mafuta ya mwezi Novemba ilipanda kwa dola za Kimarekani 2.44 na kuwa 86.13 kwa pipa, na katika soko la London bei ya mafuta ya mwezi Novemba ilipanda kwa dola za Kimarekani 2.20 na kuwa 82.75.
Kupanda haraka kwa Bei ya mafuta kunatokana na ripoti iliyotolewa na OPEC na uwezekano wa kutokea kwa mashambulizi ya Uturuki kwa kuvuka mpaka dhidi ya vikosi vya Chama cha Wakurd vilivyoko kwenye sehemu ya kaskazini ya Iraq. Ripoti iliyotolewa na OPEC tarehe 15 ilitangaza kuwa, kwa makadirio kutakuwa na upungufu wa mapipa laki moja na elfu kumi kwa siku na kuwa milioni 51.04 kutokana na upungufu wa uzalishaji wa Mexico, Uingereza, Brazil na Sudan, huku ripoti hiyo hiyo imetangaza kuwa hivi sasa mahitaji ya mafuta duniani yanaongezeka.
Siku hiyo serikali ya Uturuki iliwasilisha kwenye bunge ombi la kutaka kuvuka mpaka na kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya Wakurd vilivyopo kwenye sehemu ya kaskazini ya Iraq. Kabla ya hapo waziri mkuu wa Uturuki Bw. Recep Tayyip Erdogan alisema, ili kulinda maslahi ya taifa, bila kujali nchi nyingine kupinga au kuunga mkono, ombi hilo likipitishwa tu Uturuki itachukua hatua za kijeshi dhidi ya vikosi vya Wakurd kwa gharama yoyote. Wafanyabiashara wana wasiwasi kuwa vita vikitokea mafuta ya Iraq hayataweza kusafirishwa nje.
Sababu nyingine ni kuwa akiba ya mafuta nchini Marekani imepungua. Wizara ya Nishati ya Marekani tarehe 11 ilitangaza kuwa hadi tarehe 5 Oktoba katika wiki moja tu, akiba ya mafuta nchini humo imepungua kwa mapipa milioni 1.7. Zaidi ya hayo akiba ya mafuta katika nchi kubwa kiviwanda imepungua chini ya wastani wa miaka mitano iliyopita. Ripoti inasema, hii ni sababu nyingine ya kuongezeka kwa bei ya mafuta duniani.
Kinachostahili kutiliwa maanani ni kuwa, hali ya kupanda haraka kwa bei ya mafuta kwa mwaka huu si ya kawaida. Kwa kawaida bei ya mafuta hushuka baada ya kupanda katika robo ya tatu ya mwaka, lakini mwaka huu hali ni tofauti, kwamba baada ya kupungua katika robo ya tatu ya mwaka huu, bei inaendelea kupanda katika robo ya nne. Wachambuzi wanaona kuwa kutokea kwa hali hiyo kunatokana na hali mbaya kati ya mahitaji makubwa na upatikanaji mdogo wa mafuta, na upatikanaji huo ni chanzo kikubwa cha kuongezeka kwa bei tokea Septemba mwaka huu. Waziri wa nishati wa Marekani Bw. Samuel Bodman tarehe 12 alisema, sababu kubwa ya kupanda kwa bei ya mafuta ni tofauti kati ya mahitaji makubwa na upatikanaji mdogo wa mafuta.
Wataalamu wana maoni tofauti kuhusu hali ya baadaye ya bei ya mafuta, baadhi wanaona kuwa bei ya mafuta kwa pipa itazidi dola za Kimarekani 90 hata 100, wanasema kupanda kwa bei hakutapungua tena kwa kuwa chanzo cha kupanda kwa bei hakijabadilika hata kidogo, na huku mahitaji yanaongezeka. Lakini wataalamu wengine wanaona kuwa ingawa bei ya mafuta inapanda haraka, lakini haiwezekani kupanda hadi kufikia dola za Kimarekani 100, na baadhi ya wataalamu wanaona kuwa kutokana na hali ya dhoruba ya kuathiri bei ya mafuta kupanda imeanza kupungua, bei ya mafuta hivi sasa katika soko la kimataifa imeanza kujirekebisha.
Idhaa ya kiswahili 2007-10-16
|