Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-16 18:29:33    
Sifa na usalama wa mazao ya majini ya China vimehakikishwa

cri

Sifa na usalama wa mazao ya majini ni suala linalofuatiliwa sana na nchi za nje. Mwandishi wetu wa habari alipotembelea katika mikoa ya Guangdong na Jiangxi ambayo inazalisha mazao ya majini kwa wingi, alifahamishwa kuwa sifa na usalama wa mazao ya kilimo ya China vinainuliwa hatua kwa hatua na una uhakikisho, hasa sifa za mazao yanayouzwa katika nchi za nje.

China ni moja ya nchi zinazozalisha mazao ya majini kwa wingi duniani. Mwaka 2006 uzalishaji wa mazao ya majini nchini China ulifikia tani milioni 53, ambao ulichukua nafasi ya kwanza duniani. Wakati China inapoendeleza shughuli za mazao ya majini, serikali ya China inatunga kanuni na kusimamia sifa na usalama wa mazao ya majini katika upande wa mazingira, uzalishaji, uuzaji na uidhinishaji wa mazao, ili kuharakisha mazao ya majini ya China yafikie vigezo vya kimataifa.

   

Naibu mkurugenzi wa idara ya uvuvi ya wizara ya kilimo ya China Bw. Cui Lifeng alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni, sifa na usalama wa mazao ya majini ya China vinainuliwa hatua kwa hatua. Katika miaka minne iliyopita, asilimia 97 ya mazao ya majini yaliyokaguliwa yalifikia vigezo vya kiasi cha dawa kinachobaki kwenye mazao hayo. Kwa ujumla sifa ya mazao ya majini inahakikishwa."

Bw. Cui alisema ingawa kwa ujumla sifa ya mazao ya majini inahakikishwa, lakini kutokana na kuwa vituo vinavyozalisha mazao ya majini ni vingi na vinamesambaa katika sehemu mbalimbali, na kutokana na uwezo tofauti wa watu wanaoshughulikia kazi hiyo, bado kuna mazao ya majini ambayo kiasi cha dawa kinachobaki hakijafikia vigezo. Hivi sasa idara za uvuvi za China zinaimarisha uwezo wake ili kuondoa matatizo hayo.

Habari zinasema China imekamlisha sheria na kanuni husika ili kupiga marufuku matumizi ya dawa mbalimblai zikiwemo Malachite Green na Chloramphenicol kwenye uzalishaji wa mazao ya majini, na kuadhibu kithabiti vitendo haramu vya kutumia dawa zilizopigwa marufuku; tena China inachukua hatua kueneza ufundi wa kuzalisha mazao ya majini yasiyo na madhara kwa afya ya binadamu, na kuwataka wazalishaji waimarishe usimamizi wa sifa ya mazao na kufanya uzalishaji kwa mujibu wa vigezo vya kimataifa.

Sehemu mbalimbali za China zinachukua hatua kuimarisha usimamizi wa sifa na usalama wa mazao ya majini. Mkoa wa Jiangxi ni mmoja kati ya mikoa inayozalisha mazao ya majini kwa wingi, mazao muhimu ya majini yanayozalishwa mkoani humo ni pamoja na samaki aina ya mkunga, mazao hayo yanauzwa katika nchi na sehemu mbalimbali zikiwemo Marekani, Japan na Umoja wa Ulaya. Kiongozi wa idara ya mazao ya majini ya mkoa huo Bw. Xu Youguang alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"Tunatekeleza utaratibu wa uandikishaji, na kuvitaka vituo au makampuni yanayozalisha mazao ya majini yasitumie dawa zilizopigwa marufuku. Pili tunaweka kumbukumbu ya rekodi ya uzalishaji ili tuweze kukagua hali ya uzalishaji ya kila aina ya mazao. Tatu tunaimarisha ukaguzi na usimamizi, kuyaonya vikali makampuni yanayotumia dawa zilizopigwa marufuku, na hasa kuwaondolea idhini ya kuingia kwenye masoko ya kimataifa."

Makampuni ya uzalishaji wa mazao ya majini ya China yakisimamiwa na serikali, yanatilia maanani zaidi sifa na usalama wa mazao ya kilimo, na kuchukua hatua kuinua sifa ya mazao yao. Mji wa Zhanjiang wa mkoa wa Guangdong ulioko kusini mwa China ni kituo kikubwa zaidi cha ufugaji wa kamba wakubwa nchini China, mazao hayo wanauzwa katika nchi na sehemu mbalimbali zikiwemo Marekani, Japan na Umoja wa Ulaya. Mhandisi wa kampuni ya ufugaji ya Zhonglian ambayo ni kampuni kubwa ya ufugaji mjini Zhanjiang Bibi. Xu Kun alisema,

"Tumejiandaa kukinga maradhi ya kamba wakubwa. Tunatumia maji safi ambayo tunaua vijidudu kwa chlorinated lime na mionzi ya ultraviolet kwenye ufugaji wa kamba wa aina hiyo, hivyo kamba hao hawawezi kupata ugonjwa, kimsingi hatutumii dawa.

   

Ili kudhibiti mabaki ya dawa kwenye mazao ya majini, idara za uvuvi za sehemu mbalimbali za China zinafanya ukaguzi kwenye vituo vya ufugaji mara kwa mara, na kuvitaka vitatue masuala kwa wakati. Vituo vingi vya ukaguzi vimeanzishwa katika mikoa inayozalisha mazao ya majini kwa wingi. Mkuu wa kituo cha ukaguzi wa sifa ya mazao ya majini ya mji wa Zhanjiang Bw. Yang Feng alisema, hivi sasa kituo hicho kinaweza kukagua vijijidudu, dawa za kilimo, mabaki ya dawa na metali. Kuanzia mwaka huu kimefanya ukaguzi asilimia 70 ya vituo vikubwa vya ufugaji na maji ya baharini, alisema,

"Tunaimarisha utekelezaji wa sheria na ukaguzi, na kuteketeza mazao yasiyofikia vigezo. Tukigundua mazao yasiyofikia vigezo, tutaiarifu idara ya utekelezaji wa sheria ya shughuli za uvuvi ili kuyashughulikia mazao hayo kwa mujibu wa ripoti zao, na tunateketeza mazao yasiyofikia vigezo katika uwanja wa takataka kwa mujibu wa sheria na kanuni husika, ili kuzuia mazao hayo yasiingie sokoni."

Kutokana na juhudi za pande mbalimbali, sifa ya mazao ya kilimo yanayouzwa katika nchi za nje inainuka siku hadi siku. Ripoti ya ukaguzi wa vyakula vilivyoingizwa kutoka nchi za nje ya mwaka 2006 iliyotolewa na Japan hivi karibuni inaonesha kuwa, asilimia 99.42 ya vyakula vya China pamoja na mazao ya majini vilivyouzwa nchini Japan vilifikia vigezo, ambayo ni vikubwa kuliko vyakula vya Marekani na Umoja wa Ulaya vilivyouzwa nchini Japan.

Naibu mkuu wa idara ya uvuvi ya wizara ya kilimo ya China Bw. Cui Lifeng alisema, katika siku za usoni China itaendelea kuchukua hatua kukagua matumizi ya dawa kwenye ufugaji, hasa kukagua matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku zikiwemo Malachite Green na Chloramphenicol, alisema,

"Tutayataka makampuni ambayo yana matatizo kwenye uzalishaji kutatua masuala hayo kwa makini, na kuyaadhibu kisheria makampuni yanayokwenda kinyume na sheria. Aidha, tutatoa orodha ya makampuni ambayo yanatakiwa kusimamiwa zaidi ili kuyakagua mara kwa mara.

Alidokeza kuwa, China itaendelea kueneza ujuzi wa kuzalisha mazao ya majini yasiyo na madhara kwa binadamu, na kuwaongoza wafugaji waanzishe utaratibu wa kusimamia sifa na usalama wa mazao yao, ili kuwapatia wateja wa nchini na wa nchi za nje mazao mazuri zaidi ya majini.