Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-17 16:43:04    
Maisha mazuri ya watu wa Diqing

cri

Wilaya ya Diqing iko kaskazini magharibi mwa mkoa wa Yunnan, na iko jirani na mkoa unaojiendesha wa Tibet. Maana ya Diqing kwenye lugha ya Kitibet ni sehemu yenye baraka na heri, watu wa makabila 26 likiwemo kabila la Watibet, la Walisu, la Wanaxi na la Wahan wanaishi kwenye wilaya hiyo, na miongoni mwao, watu wa kabila la Watibet wanachukua theluthi moja ya idadi ya watu wa huko.

Wilaya ya Diqing ilianza kujulikana duniani miaka kumi iliyopita kutokana na riwaya moja. Kwenye riwaya hiyo ya Lost Horizon iliyochapishwa mwaka 1933, mwandishi wake Mmarekani Bw. James Hilton alisimulia sehemu moja iliyoko milimani yenye amani, utulivu na mandhari nzuri, sehemu hiyo iitwayo Shangri-la ambayo iko mashariki mwa dunia. Baada ya kutafuta kwa miaka zaidi ya 60, watu waligundua wilaya ya Diqing, China. Wilaya ya Diqing hali yake ya kila kitu ni sawa na ile iliyosimuliwa kwenye riwaya ya Bw. Hilton, mbali na hayo Shangri-la ni jina la lugha ya kitibet la mji mkuu wa Diqing Zhongdian, maana yake ni jua na mwezi moyoni, hatimaye jina la mji wa Zhongdian lilibadilishwa kuwa Shangri-la.

Diqing ilithibitishwa kuwa Shangri-la iliyosimuliwa kwenye riwaya ya Bw. Hilton siyo tu Diqing ina mazingira mazuri ya uwanda wa juu yaliyoelezwa kwenye riwaya hiyo, bali pia wakazi wa huko kudumisha maisha yenye amani na utulivu kwa muda mrefu. Mkuu wa idara ya utamaduni ya wilaya inayojiendesha ya Diqing Bw. Pu Jiang alisema,

"Undani wa Shangri-la tuliyozungumzia inapaswa kuwa ni masikilizano, utulivu na heri na baraka. Kwenye sehemu ya Diqing, watu wa makabila tofauti na wenye dini tofauti wanaishi pamoja kwa masikilizano, ambapo watu wanaishi kwenye hali ya mapatano na mazingira ya asili, sehemu hiyo ina mandhari nzuri, na asilimia ya sehemu zilizofunikwa na misitu ni kubwa zaidi mkoani Yunnan. "

Mazingira na maisha mazuri ya Diqing yanawavutia watu wa nchi mbalimbali duniani, hata baadhi ya watalii kutoka nje waliamua kuhamia na kuishi kwenye sehemu hiyo. Bibi Cater Saher Malik ni mke wa Bw. Khalid Malik ambaye ni mjumbe mkuu wa Shirika la Mipango ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini China. Mwaka 2004, bibi Malik alipotembelea mji wa Shangri-la mara ya kwanza, aliupenda sana mji huo na kuamua kuishi huko. Katika miaka ya hivi karibuni, amefanya mambo mengi kwa ajili ya sehemu hiyo yakiwemo kujulisha utamaduni wa makabila madogo madogo ya Diqing kwa marafiki zake duniani, kuanzisha mfuko wa mabaki ya milima mkoani Yunnan, kuchangia fedha kwa shughuli za elimu, na mwaka huu alipewa uraia wa heshima na serikali ya Diqing. Kwenye sherehe ya kumpa heshima hiyo, binti yake Sahra Malik alisema,

"Mama yangu alikuja hapa mara ya kwanza miaka minne iliyopita, baadaye alirudi kwa mara nyingi huko Shangri-la. Amefanya mambo mengi ya kuwasaidia watu wa Shangri-la. Mama yangu anafanya kazi hapa, na sasa mimi pia nafanya kazi hapa, kwa sababu ninaupenda sana mji wa Shangri-la, una mandhari mazuri na watu wakarimu."

Ukitembea kwa miguu kwenye mitaa mjini Shangri-la, utawaona wakazi wengi waliovaa nguo za kikabila na majengo yenye umaalumu wa makabila madogo madogo, hii ni picha nzuri inayowavutia watu. Ukienda vijijini, utaona maisha ya kikale yenye utulivu na starehe, bendera za kidini zinapepea juu ya majengo, ng'ombe na mbuzi wanakula nyasi, na kwenye maeneo ya kando ya mto, kuna mashamba makubwa ya mazao.

Wakati watu wa makabila madogo madogo wa Diqing wanapoishi maisha mazuri ya jadi, pia wananufaishwa na maendeleo ya uchumi. Mkulima wa kabila la Wanaxi bibi Yang Chunsheng alisema,

"Nyumbani kwangu kuna vyombo mbalimbali vya umeme, vikiwemo televisheni na jokofu. Tunaishi maisha mazuri, baada ya kumaliza kazi mashambani mimi na mume wangu na mtoto wangu tunafanya utalii mkoani Yunnan mara kwa mara."

Katika miaka ya hivi karibuni, ongezeko la thamani ya uzalishaji wa mali wa wilaya ya Diqing ni karibuni asilimia 22 kwa mwaka, na mapato ya wakulima na wafugaji yanaongezeka kwa asilimia 14.2 kwa mwaka, hivyo kwenda nje kufanya utalii kumekuwa ni jambo la kawaida kwa watu hao. Mbali na kufanya utalii, njia nyingine za kufanya mawasiliano na nje ikiwemo kufanya biashara na kusoma kwenye sehemu za nje zimepanua mtazamo wa watu wa Diqing, pia zimewafanya waone fahari kuwa wakazi wa Shangri-la. Bibi Zhaxi Quchu kutoka wilaya hiyo sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Uhandisi cha Beijing, anapenda sana maskani yake, alisema,

"Ninasoma Beijing, niliporudi nyumbani baada ya miaka mitatu, ninaona mabadiliko mengi makubwa mjini Shangri-la, hata niliona sehemu nyingi mjini ni ngeni kwangu. Tunaona fahari kubwa kwamba tunatoka Shangri-la."

Watu wa Shangri-la wanajivunia kwa kuwa Shangri-la ni sehemu ya peponi wanayotarajia binadamu, na watu wa Diqing pia wanajivunia kwa sababu Diqing ni nyumbani kwa Shangri-la.

Kila usiku, watu kutoka mji wa Diqing na viongoji vyake wanakusanyika na kucheza ngoma kwenye uwanja ulioko karibu na ofisi ya serikali ya wilaya, na ngoma hiyo huwavutia na kuwashirikisha wageni kutoka nchini na nchi za nje.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-17.