Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-18 17:29:33    
Madaktari wanaohudumia wagonjwa kwa moyo wote

cri

Chama cha Kikomunisti cha China, ambacho ni chama tawala cha China kitaitisha mkutano mkuu wa 17 kuanzia tarehe 15 mwezi Oktoba. Wajumbe zaidi ya 2,200 wanaohudhuria mkutano huo wanatoka sehemu mbalimbali za China wakiwakilisha wanachama wapatao milioni 70 wa chama hicho. Daktari Tang Xiaoping na daktari Zhan Shengjun ni miongoni mwa wajumbe hao. Wao walichaguliwa na wanachama wenzao kuhudhuria mkutano mkuu wa chama kutokana na kuwa madaktari hodari na kushikilia maadili ya udaktari.

Kama tunavyofahamu kuwa, ukimwi na homa ya manjano inayosababishwa na virusi ni kati ya magonjwa 10 ya kwanza yanayotishia maisha ya binadamu. Lakini daktari Tang Xiaoping ambaye sasa ni mkuu wa hospitali ya 8 ya umma ya Guangzhou, mji wa kusini mwa China, aliamua kutumia muda wake mwingi kwenye tiba ya magonjwa hayo mawili ya kuambukiza. Katika miaka 21 iliyopita daktari huyo alikuwa anashughulikia kinga na tiba ya magonjwa ya kuambukiza. Akijumuisha kazi yake ngumu, yenye shida na hatari, alisema  "Nikikumbuka miaka hiyo 21 tangu nianze kujishughulisha na kazi ya kinga na tiba ya magonjwa ya kuambukiza, hisia mbalimbali zinanijia. Naona mambo niliyopata ni mengi zaidi kuliko niliyopoteza, hususan kukabiliana na maambukizo ya magonjwa, tulijitahidi tukafanikiwa kudhibiti makali ya maambukizo ya magonjwa, wakati huo huo tuliona furaha kubwa ambazo siwezi kueleza kwa maneno."

Mwaka 2003 mjamzito mmoja aliyekuwa anaishi na virusi vya ukimwi alilazwa kwenye hospitali aliyokuwa anafanya kazi daktari Tang Xiaoping. Kulikuwa na hatari ya kuambukizwa virusi vya ukimwi kwa njia ya damu wakati mjamzito huyo alipokuwa anajifungua. Ili kuepuka hatari hiyo na kuhakikisha usalama wa mjamzito na motto wake, daktari Tang aliamua kutumia wodi moja iliyopo kwenye eneo la kuwahudumia wagonjwa wa ukimwi kuwa chumba cha muda cha kujifungua, na yeye mwenyewe kuwa mkunga.

Akiwa mtaalamu wa ugonjwa wa ukimwi, daktari Tang alitambua wazi hatari kubwa ya uamuzi huo. Hata hivyo aliweka kando hatari inayomkabili, bali alizingatia namna ya kuhakikisha usalama wa maisha ya mjamzito na mtoto wake. Baada ya daktari Tang kufanikiwa kumsaidia mjamzito ajifungue, mjamzito huyo, jamaa zake na wauguzi walitokwa na machozi.

Ugonjwa wa ukimwi unatia hofu kwenye jamii na kwa kawaida wagonjwa wa ukimwi ni wadhaifu kiroho. Ili kupunguza shinikizo kwa wagonjwa hao, daktari Tang Xiaoping anawatembelea wagonjwa hao kwenye wodi zao kila siku, kushikana mikono na wagonjwa wa ukimwi na kuzungumza nao. Kila zinapofikia sikukuu muhimu, anakula chakula pamoja na wagonjwa wa ukimwi.

Daktari mwenzake Bi. Xu Min ambaye ni mkurugenzi wa kitivo cha magonjwa makubwa ya ini kwenye hospitali ya 8 ya umma ya Guangzhou alitoa maoni yake kuhusu daktari Tang, akisema  "Yeye anaona kutibu wagonjwa si tu kuwanywesha dawa, bali pia kuwapa uungaji mkono wa kiroho, ili wawe na hiari kufuata matibabu."

Kutokana na juhudi za daktari Tang Xiaoping, hospitali yake ni ya kwanza nchini China kutenga eneo maalumu kuwahudumia wagonjwa wa ukimwi, vile vile ilianzisha shirika la kuwatunza watu wenye ukimwi ambalo ni la kwanza kuanzishwa kwenye sehemu ya kusini mwa China.

Daktari Zhan Shengjun ni mkuu wa hospitali ya msalaba mwekundu ya kata ya Xinfa, mkoani Heilongjiang, kaskazini mashariki mwa China. Tofauti na hospitali kubwa za mijini, hospitali anakofanya kazi daktari Zhan ni ndogo inayowahudumia wakazi wa vijijini, ambapo hakuna madaktari wengi wa taaluma mbalimbali. Kwa hiyo daktari Zhan alijifunza taaluma ya mifupa, na magonjwa ya wanawake. Kutokana na uhodari wake wa matibabu alipendwa na wagonjwa wengi kiasi kwamba, aliwahi kufanya upasuaji mara 13 kwa siku moja.

Mbali na kuwa daktari hodari, Bw. Zhan Shengjun anafuata kwa makini maadili ya udaktari. Watu wanaokwenda kwenye hospitali yake kuomba huduma za matibabu wengi kabisa ni wanavijiji wa jirani, ambao ni pamoja na wagonjwa wenye matatizo ya kiuchumi. Bibi Wei Shuxia kutoka kijiji cha Qianjin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, miaka minne iliyopita aliwahi kukumbwa na hali ya kupoteza fahamu kutokana na kupunguliwa damu. Kutokana na umaskini, alipopelekwa hospitali jamaa zake walikuwa wamekusanya Yuan 700 tu, lakini gharama za upasuaji na matibabu ya baadaye kwenye hospitali zilikuwa Yuan 3,500. Wakati huo walimkuta daktari Zhan Shengjun, ambaye alisema ni lazima kwanza aokoe maisha ya mgonjwa, na suala la kulipa gharama lijadiliwe baadaye. Kwa hiyo Bibi Wei Shuxia alifanyiwa upasuaji kwa wakati.

Mwaka 1987 daktari Zhan Shengjun aliteuliwa kuwa mkuu wa hospitali ya msalaba mwekundu ya Xinfa. Wakati huo huo hospitali hiyo ilikuwa na vyumba zaidi ya 10 na ilikuwa na upungufu wa vifaa vya matibabu, zaidi ya hayo ilikuwa na deni la zaidi ya Yuan laki moja. Hivi sasa kutokana na jitihada za daktari Zhan na madaktari na wauguzi wanzake, hospitali hiyo imelipa madeni yote na mali zake zisizohamishika zimeongezeka hadi Yuan milioni 1.92. Kwa kutumia fedha hizo hospitali hiyo ilinunua vifaa vya kisasa vya matibabu vyenye thamani ya Yuan milioni 1.5. Basi je mafanikio hayo yalipatikanaje? Daktari Zhan Shengjun akijibu alisema "Tulihesabu kwa makini matumizi yetu hata senti moja. Pia tunajitahidi kupanua wigo wa faida. Tunainua kiwango cha ufundi na huduma zetu ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa mbalimbali na kutibu magonjwa ya aina mbalimbali."

Idhaa ya kiswahili 2007-10-18