Waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Bibi Benazir Bhutto ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha upinzani, Chama cha Umma, tarehe 18 alirudi mjini Karachi Pakistan baada ya kuishi Uingereza kwa miaka minane. Baada ya yeye kufika tu ilitokea milipuko miwili dhidi ya waziri huyo wa zamani. Habari kutoka polisi ya Pakistan zinasema, milipuko hiyo ilisababisha vifo vya watu 124 na watu karibu 400 kujeruhiwa, na idadi hiyo pengine sio ya mwisho.
Asubuhi ya tarehe 18 Bibi Benazir Bhutto alifika mjini Karachi kwa ndege, maofisa zaidi ya mia moja walifuatana naye, lakini mumewe na watoto wake hawakurudi naye. Alipokuwa kwenye uwanja wa ndege wa Karachi alisema, amerudi kwa ajili ya watu maskini na demokrasia ya Pakistan. Nje ya uwanja huo kulikuwa na maelfu wakimkaribisha. Kwa mujibu wa mpango, serikali ya Pakistan ilimpa gari moja la kukinga risasi na ilituma askari polisi wengi kuhakikisha usalama wake.
Lakini sio watu wote wa Pakistan wanamkaribisha Bibi Bhutto. Waziri wa reli Bw. Shaikh Rashid Ahmad alisema, athari ya Benazir Bhutto imefifia sana ikilinganishwa zamani. Alisema, kwenye mji wa Rawalpindi hakuna watu wengi waliokwenda Karachi kumkaribisha. Wakati watu walipokuwa wakimshangilia Bibi huyo kurudi Pakistan karibu na gari lililombeba, milipuko miwili ilitokea na kusababisha vifo vya watu wengi na wengine kujeruhiwa. Habari kutoka polisi ya Pakistan zinasema milipuko ilitokea kwenye maandamano ya watu wanaoumwunga mkono, lakini Bibi Bhutto alikuwa salama na amerudi kwenye makazi yake mjini Karachi. Kadhalika polisi pia ilisema kutokana na uchunguzi wa mwanzo moja ya milipuko miwili ni mlipuko wa kujiua, na mwingine ni mlipuko wa bomu lililotegwa ndani ya gari. Watu walioathirika, wengi ni askari polisi na walinzi wa usalama. Hadi sasa hakuna jumuiya yoyote iliyotangaza kuwajibika na milipuko hiyo.
Rais Pervez Musharraf na waziri mkuu wa Pakistan walilaani vikali tukio hilo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon pia alitoa taarifa akionesha kulaani na kushtushwa na tukio hilo, na anatumai kuwa vikundi mbalimbali vya kisiasa vitafanya juhudi kwa pamoja ili kuimarisha usalama wa taifa. Marekani pia ililaani vikali tukio hilo na kuona kuwa hakuna kisingizio chochote kinachoweza kutetea tukio hilo.
Bibi Benazir Bhutto ni mwenyekiti wa chama kikubwa cha upinzani nchini Pakistan, na alikuwa waziri mkuu wa nchi hiyo mara mbili. Kutokana na kutuhumiwa kwa ufisadi, mwaka 1999 alikwenda kuishi uhamishoni. Mapema mwaka huu Bibi Bhutto alitangaza kuwa atarudi nchini Pakistan kushiriki kwenye uchaguzi akiwa mgombea wa Chama chake cha Umma. Rais Pervez Musharraf tarehe 5 mwezi huu alisaini na kutangaza makubaliano, na kwa mujibu wa makubaliano hayo Bibi Bhutto atasamehewa mashitaka yake ya ufisadi.
Vyombo vya habari vinaona kuwa makubaliano hayo yalimwezesha Bibi Bhutto kurudi nyumbani. Lakini mahakama kuu ya Pakistan tarehe 12 ilitangaza kuwa imekubali ombi la wapinzani la kupinga msamaha wa suala lake la ufisadi. Naibu waziri wa habari na utangazaji wa Pakistan Bw. Tariq Azeem alisema, kama mahakama kuu ikibatilisha makubaliano yaliyotangazwa na rais basi serikali ya Pakistan itaheshimu uamuzi wa mahakama kuu, Bi. Bhutto atakabiliwa tena na mashitaka ya ufisadi. Vyombo vya habari vinaona kuwa ingawa mahakama kuu haikubadilisha moja kwa moja makubaliano ya rais Musharraf, lakini wasiwasi wa kisiasa umeongezeka nchini Pakistan.
Wasiwasi mwingine wa kisiasa nchini Pakistan pia unatokana na kesi nyingine, kuhusu kama rais wa sasa Bw. Musharraf anastahiki kuendelea kuwa rais katika awamu mpya au la. Baada ya mahakama kuu kuchunguza kesi hiyo tarehe 18 imeamua kuahirisha kesi hiyo mpaka tarehe 22. Kipindi cha bunge la sasa kitamalizika tarehe 15 mwezi ujao, na uchaguzi mpya wa bunge utafanyika mwezi Januari mwaka kesho. Waziri wa habari na utangazaji wa Pakistan Bw. Muhammad Ali Durrani tarehe 16 alitangaza kuwa, bunge la sasa litavunjwa tarehe 15 mwezi ujao, rais Musharraf atashirikiana na vyama vya upinzani kuunda serikali ya mpito ili kuandaa uchaguzi mpya wa bunge.
Hivi sasa Pakistan iko katika kipindi muhimu cha kisiasa, hali ya siasa ya Pakistan itakuwaje, tusuribiri tuone.
Idhaa ya kiswahili 2007-10-19
|