Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-22 14:55:43    
Mfasiri na mshairi Shu Cai

cri

Hivi karibuni, mshairi wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 83 Bw. Yves Bonnefoy alipata tuzo kubwa ya Franz Kafka ya fasihi ya Ulaya kwa mwaka 2007. Habari hiyo ilimfurahisha sana mshairi wa China Bw. Shu Cai, kwa sababu katika miaka mingi iliyopita aliwafahamisha wasomaji wa China kuhusu mshairi huyo, tuzo hiyo inathibitisha kuwa yeye hakukosea kuchagua mwandishi aliye hodari na kufasiri vitabu vyake.

Bw. Shu Cai anaishi kwenye nyumba iliyoko kando ya ziwa mjini Beijing. Majarida mengi ya fasihi ya Ufaransa yaliyokuwa mezani kwake yanaonesha kuwa Bw. Shu Cai ana uhusiano na fasihi ya Ufaransa.

Bw. Shu Cai ni mtafiti kwenye Taasisi ya Utafiti wa Fasihi ya Nchi za Nje ya China, lakini kabla ya kuwa mtafiti aliwahi kuwa mwanadiplomasia katika ubalozi wa China nchini Senegal, na pia aliwahi kuwa msimamizi wa kampuni moja ya biashara ya China, lakini kutokana na upendo wake wa mashairi, aliacha kazi yake na kujifungia ndani ya chumba chake kilicho kimya na kuandika, kutafsiri na kuhakiki mashairi. Alisema,

"Nilipokuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari nilianza kupenda mashairi ya kisasa na pia nilijaribu kuandika mashairi kwa mtindo wa kale. Baadaye nilipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu mjini Beijing nilianzisha klabu ya fasihi na jarida moja lililoitwa "Test", kwa sababu katika muda wote wa miaka minne ya masomo fasihi ilienea sana chuoni, hali hiyo ilinipa msukumo wa kuandika mashairi."

Bw. Shu Cai alipokuwa mtoto maisha yake yalikuwa magumu sana. Mama yake alifariki dunia alipokuwa na umri wa miaka minne, na miaka miwili baadaye bibi yake aliyekuwa akimtegemea kimaisha pia aliiaga dunia. Uchungu na ugumu wa maisha ulimwachia kumbukumbu isiyosahaulika, na uliathiri vibaya ukuaji wake. Mwaka 1983 Bw. Shu Cai alijiunga na Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing na kusomea lugha ya Kifaransa. Wakati huo ulikuwa mwanzo wa mageuzi ya kiuchumi nchini China, Beijing ikiwa kitovu cha utamaduni nchini China upepo wa mageuzi ulifanya watokee waandishi wengi wa fasihi, na hali moto moto ya fasihi katika vyuo vikuu ilipamba moto, wakati huo Shu Cai alianza kuandika mashairi ambayo yalichapishwa katika majarida. Alisema,

"Mwaka 1986 mashairi yangu kadhaa yalichapishwa, lakini nililotilia maanani ni shairi langu liitwalo 'Ndege Wawili' lililoko kwenye kitabu cha 'Mashairi Yaliyochaguliwa ya Washairi wa Vyuo Vikuu'."

Baada ya kuhitimu, Bw. Shu Cai alifanya kazi katika Wizara ya Biashara na Nchi za Nje ya China, kutokana na kujua lugha ya Kifaransa, mwaka 1990 alitumwa kwenda kufanya kazi katika ubalozi wa China nchini Senegal, maisha ya kidiplomasia pia yalikuwa na athari kwa maisha na uandishi wake wa baadaye.

"Usipokwenda barani Afrika hutafahamu uzuri wa bara hilo, nilipokuwa huko nilivutiwa sana na uzuri wake ambao ni wa kiasili kabisa, ambao haujawahi kugeuzwa na kupambwa na binadamu. Nilifanya kazi Afrika ya magharibi, utamaduni wa huko ni wenye uchangamfu sana na uchangamfu huo una uwezo mkubwa wa kuyeyusha na kuyafanya matatizo kuwa ya furaha, niliathiriwa sana na uchangamfu huo ambao ni tabia ya Waafrika waliyozaliwa nayo."

Mwaka 1994 Bw. Shu Cai alirudi nyumbani China baada ya kufanya kazi nchini Senegal kwa miaka minne, kisha aliandika kitabu chenye mashairi 150 aliyoyaandika katika muda wa miaka 10.

Ili aweze kuandika mashairi bila kuweka mawazo yake kwenye shughuli nyingine, mwaka 2000 aliacha kazi yake yenye mshahara mkubwa katika kampuni ya biashara, alijiunga na taasisi ya utafiti wa fasihi ya nchi za nje, akiandika mashairi na kufasiri vitabu vya Ufaransa. Aliandika vitabu viwili vya mashairi yake na vitabu kadhaa vya washairi wakubwa wa Ufaransa. Kutokana na mashairi ya Ufaransa alipata kitu kilichogusa hisia zake. Alisema,

"Sikutafsiri mashairi yote ya Ufaransa, bali natafsiri tu yale yaliyogusa hisia zangu na yale yaliyoandikwa na washairi ninaowapenda, kwa sababu ninapotafsiri nazama ndani ya mashairi na utamu nilioupata kutoka kwenye mashairi hayo ni virutubisho vya uandishi wangu wa mashairi."

Bw. Shu Cai alisema, anashindwa kueleza nini sababu ya kumfanya aanze kuandika mashairi, lakini kila baada ya kuandika shairi moja ndivyo alivyozidi kuwa na hamu ya kuandika mashairi mengine. Anatumia moyo wake wote na muda wake mwingi, lakini hajuti kwa sababu akiwa mshairi hana tamaa binafsi, anaamini kuwa mashairi yake yatapata wasomaji wengi.

Licha ya kazi ya utafiti wa fasihi ya nchi za nje na kuandika mashairi, pia anashiriki kwenye shughuli nyingi za kijamii zinazohusiana na fasihi. Kwa niaba ya washairi aliwahi kushiriki kwenye matamasha mengi ya kimataifa ya washairi, alikuwa mmoja wa waandaaji wa tamasha la kimataifa la washairi lililofanyika hivi karibuni huko kwenye Ziwa Qinghai, na mara nyingi aliwaalika washairi wa nchi za nje kuja kufanya maingiliano ya fasihi nchini China.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-22