Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-23 17:03:42    
China kukamilisha huduma za ushirikiano kuhusu watu wanaofanya kazi kwa mikataba katika nchi za nje

cri

   

Kutokana na maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za nje, na kuharakishwa kwa utekelezaji wa mkakati wa kuanzisha shughuli nje ya nchi, Wachina wengi zaidi wamekwenda kufanya kazi nchi za nje. Ili kulinda haki na maslahi yao, serikali ya China inafanya juhudi kukamilisha huduma za ushirikiano kuhusu watu wanaofanya kazi kwa mikataba nchi za nje.

Mfumo wa utoaji wa ushauri kwa njia ya simu kuhusu huduma za ushirikiano kuhusu watu wanaofanya kazi kwa mikataba katika nchi za nje ulianzishwa na wizara ya biashara ya China hivi karibuni.

Mfumo huo unatoa huduma kwa watu wanaotaka kufanya kazi nchi za nje. Watu wenye maswali wakipiga simu hiyo, watapata habari mbalimbali bila ya malipo. Habari hizo ni pamoja na uhalali wa makampuni yanayowapeleka wafanyakazi kwenda nchi za nje, hali halisi ya miradi iliyoko nchi za nje, utaratibu na masharti ya kufanya kazi katika nchi za nje, na mambo muhimu yanayohitaji kutiliwa maanani wakati wafanyakazi wanaposaini mikataba.

Mkurugenzi wa idara ya ushirikiano ya wizara ya biashara ya China Bw. Wu Xilin alisema, lengo la kuanzisha mfumo huo wa utoaji wa ushauri kwa njia ya simu ni kuwaelekeza wafanyakazi waende kufanya kazi nchi za nje kwa njia halali, na kulinda haki na maslahi yao, alisema,

"Mfumo huo wa utoaji ushauri unawawezesha wafanyakazi wafahamu sera za ushirikiano kati ya China na nchi za nje kuhusu kufanya kazi nje kwa mikataba, na ujuzi wa kimsingi kuhusu kufanya kazi nchi za nje, unawasaidia kupunguza hatari na gharama ya kwenda nchi za nje, na kulinda maslahi yao."

Kutokana na nguvu kazi ya kutosha na yenye bei nafuu nchini China, katika miaka ya karibuni Wachina wengi zaidi walikwenda kufanya kazi katika nchi za nje. Kwa mujibu wa takwimu, kwa ujumla Wachina milioni 4 walikwenda kufanya kazi nchi za nje, na hivi sasa Wachina laki 7.3 wanafanya kazi nchi na sehemu zaidi ya 160, ambao shughuli zao zinahusu ujenzi, mikahawa na uchukuzi.

Wakati idadi ya Wachina wanaofanya kazi nchi za nje inapoongezeka, masuala kadha wa kadha yanatokea. Bw. Wu Xilin alisema,

"Makampuni na watu kadhaa wanawadanganya wafanyakazi kwa kisingizio cha ushirikiano na nje kuhusu kufanya kazi kwa mikataba. Makampuni na watu hao hawana mikataba ya kazi, lakini wanaandikisha wafanyakazi na kuwatoza ada kubwa, lakini mwishoni wafanyakazi hawakupelekwa nje."

Ili kutatua masuala hayo na kulinda maslahi ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, wizara ya biashara ya China imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kutoa idhini ya uendeshaji wa makampuni, kuthibitisha mikataba, na kukagua ukweli wa miradi na vigezo vya kutoza ada; wakati huo huo, wizara hiyo inatekeleza kwa makini utaratibu wa kuwaandaa na kuwafanyia mtihani wafanyakazi watakaopelekwa nje ili kuinua uwezo wao

Habari zinasema ili kuzuia wafanyakazi wasidanganywe, wizara ya biashara ya China imechapisha vitabu laki 5 kuhusu kufanya kazi nchi za nje, na kuwapa wafanyakazi bila ya malipo; wizara hiyo pia imeweka makala maalumu kwenye tovuti yake katika mtandao wa Internet, kuwafahamisha wafanyakazi sera husika, kujibu maswali yao, na kutoa onyo kuhusu usalama wa kufanya kazi katika nchi za nje na habari kuhusu miradi isiyoaminika.

   

Zamani makampuni mengi yalikuwa na wasiwasi wa kupata hasara kwa kuwa wafanyakazi hawatatekeleza mikataba kutokana na sababu mbalimbali, ili kuzuia jambo hilo lisitokee, makampuni hayo yaliwataka wafanyakazi watoe fedha za uhakikisho kabla ya kwenda nchi za nje. Hivi sasa fedha hizo zimefutwa, na wafanyakazi wanatakiwa kununua bima ya utekelezaji wa mikataba tu, ambayo inapunguza mzigo kwa kwa kiasi kikubwa. Bw. Wu Xilin alisema,

"Wafanyakazi wengi wana matatizo ya kiuchumi, kutoa pesa nyingi za dhamana kabla ya kwenda nchi za nje ni mzigo mkubwa kwa familia za wafanyakazi hao. Tumechukua hatua kuwasaidia kununua bima ya utekelezaji wa mikataba, ambayo inahitaji yuan mia kadhaa tu."

Kituo cha kimataifa cha masoko ya watu wenye ujuzi cha China ni idara ya wakala wa uajiri. Kituo hicho kina ofisi kumi kadhaa duniani, kimekuwa kinawasiliana na kukagua makampuni ya nchi za nje kwa muda mrefu. Kikiwa na idara inayotoa huduma za ushirikiano kuhusu kufanya kazi nje kwa mkataba, ili kutoa uhakikisho kwa wafanyakazi wanaofanya kazi kwa mikataba nchi za nje, kituo hicho kimechukua hatua mbalimbali zikiwemo kukagua makampuni ya nchi za nje na mikataba ya kazi, na kuwasaidia wafanyakazi wapate idhini ya kufanya kazi nchi za nje.

Meneja wa kituo hicho Bw. Bu Xiangyu alisema,

"Mustakabali wa ushirikiano kuhusu watu kufanya kazi kwa mikataba nje ya nchi bila shaka utakuwa mzuri zaidi. Aidha, sifa ya nguvu kazi nchini China unainuliwa siku hadi siku, hivi sasa wafanyakazi ambao wanaelewa Kiingereza na walihitimu kutoka shule za kazi za ufundi pia wameshiriki kwenye ushirikiano huo, Kutokana na kuinuliwa kwa sifa ya nguvu kazi, mahitaji ya nguvu kazi ya nchi za nje yameongezeka, hivyo naona kuwa mustakabali wa ushirikiano huo ni mzuri."

Msaidizi wa waziri wa biashara wa China Bw. Chen Jian alisema, hivi sasa kazi hiyo imekuwa sehemu muhimu ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za nje. Ushirikiano huo si kama tu unaweza kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kuongeza mapato ya familia za wafanyakazi wanaofanya kazi nchi za nje, bali pia unaweza kupunguza shinikizo la ajira nchini China, kushirikiana na kusaidiana na nchi mbalimbali ili kupata maendeleo ya pamoja.

Bw. Chen Jian pia alisema, kimsingi wafanyakazi hao watarudi nchini China baada ya mikataba ya kazi kwisha, hivyo hawatasababisha masuala ya kijamii yakiwemo uajiri na uhamiaji katika nchi za nje.