Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-23 16:55:46    
Barua 1021

cri

Mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha kikomunisti cha China ulifunguliwa tarehe 15 Oktoba na utafungwa leo tarehe 21. Tarehe 15 Oktoba, Katibu mkuu wa Kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China Bwana Hu Jintao kwa niaba ya Kamati kuu ya 16 ya chama ametoa ripoti isemayo: "Nyanyua Bendera ya ujamaa wenye umaalum wa China, na fanya juhudi kwa ajili ya kujipatia ushindi mpya katika kujenga jamii yenye maisha bora kote nchini".

Ripoti hiyo imegawanyika kwenye sehemu 12 kuhusu kutathmini kazi za miaka mitano iliyopita, kujumuisha kinadharia mchakato wa kihistoria wa mageuzi na ufunguaji mlango nchini China karibu miaka 30 iliyopita, kufafanua maana halisi ya wazo la kujiendeleza kwa njia ya kisayansi na umuhimu wake mkubwa kwa maendeleo ya China, kuweka mipango ya kazi za China katika sekta za uchumi, siasa, utamaduni, jamii, ulinzi wa nchi, mambo ya kidiplomasia, muungano wa taifa na ujenzi wa chama.

Wajumbe wanaohudhuria Mkutano huo walipojadili walisema, ripoti hiyo ni Taarifa ya siasa na Mpango wa utekelezaji wa Chama cha Kikomunisti cha China kwa ajili ya kuendeleza mambo ya ujamaa wenye umaalumu wa kichina katika kipindi cha mwanzo mpya wa historia. Ripoti hiyo imejumuisha kisayansi mafanikio yaliyopatikana katika kazi za China katika miaka mitano iliyopita na uzoefu wa mageuzi na ufunguaji mlango katika miaka karibu 30 iliyopita. Ripoti hiyo inatoa kipaumbele kwa maslahi ya wananchi, imezungumzia zaidi masuala kuhusu maisha ya wananchi, hii imeonesha vilivyo wazo la chama la kujipatia maendeleo kwa ajili ya wananchi, kuwategemea wananchi katika kujiendeleza, na kuwawezesha wananchi wanufaike na matokeo ya maendeleo.

Tangu Mkutano huo ufunguliwe, wasikilizaji wetu wanafuatilia Mkutano huo, na wametuletea barua pepe wakieleza maoni yao.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 wa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu anasema katika barua pepe aliyotuandikia kuwa, kuanza kwa Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama Cha Kikomunisti cha China mnamo tarehe 15 Oktoba mwaka kuu mjini Beijing, kunamaanisha kuwa hilo ni tukio muhimu kabisa la kisiasa sio tu kwa mamilioni ya raia wa Jamhuri ya Watu wa China, lakini hata kwa wao wasikilizaji wa Radio China Kimataifa.

Kwani Mkutano huo unaweza kuhesabiwa kama ni msingi mkuu wa maamuzi ya kisiasa na kiuchumi kwa Jamhuri ya Watu wa China katika wakati huu, na pia kwa wakati wa baadaye, hivyo umuhimu wa kufatilia kwa makini maswala yote yatakayohusu mkutano huo chini ya viongozi wakuu wa Kikomunisti wa China pamoja na wajumbe wanaowakilisha mikoa mbalimbali ya nchi hii, ni jambo muhimu sana na lenye kusisimua sana.

Anasema yeye binafsi amekuwa akifuatilia kwa makini matukio yote ya Mkutano Mkuu wa 17 wa Chama Cha Kikomunisti cha China tangu pale ulipofunguliwa kupitia tovuti yenu ya Radio China Kimataifa, na ni matumaini yake makubwa kwamba wasikilizaji wenzake pia watakuwa na shauku kubwa ya kufatilia kwa makini Mkutano huo muhimu kabisa na wenye maana kubwa kwa Wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China.

Bila shaka yoyote matukio ya mkutano huo yanasubiriwa kwa hamu na wananchi wa China pamoja na wasikilizaji, ili kuona namna gani viongozi na wajumbe wakuu wa Chama Cha Kikomunisti wataweza kutoa maamuzi juu ya maswali mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi kwa faida ya Umma wa China na dunia kwa ujumla. Mimi binafsi naamini kuwa viongozi hao watatumia busara zao na vipaji walivyo navyo ili kuhakikisha kwamba wanatoa maamuzi yatakayokuwa na msingi muhimu wa kuboresha maisha na maendeleo ya watu wa China pamoja na kusaidia ulimwengu wa tatu kujikwamua katika umasikini na ukosefu wa maendeleo, pamoja kubuni sera na mikakati mizuri ya kisiasa ndani na nje ya Jamhuri ya Watu wa China.

Bwana Mbarouk anaiomba Radio China Kimataifa isichoke kuwa mstari wa mbele kuwafahamisha wasikilizaji wake juu ya matokeo ya Mkutano huo Mkuu wa 17 wa Chama Cha Kikomunisti Cha China unaoendelea mjini Beijing .

Na msikilizaji wetu wa Kenya Joyce Mhavile ametuletea barua pepe akisema, anafurahia kupata habari nono kuhusu mkutano mkuu wa 17 wa chama cha kikomunisti cha China kwa kupitia matangazo yetu ya FM ya Nairobi. Anasema alivutiwa na taarifa iliyotolewa na Bw. Hu Jintao, inayohusu mafanikio mbalimbali iliyopata China katika miaka mitano iliyopita, pia imeweka malengo ya maendeleo katika siku zijazo. Na alivutiwa sana na maelezo kuhusu China kushikilia njia ya kujiendeleza kwa amani, suala ambalo anakubaliana nalo kabisa.

Anasema nyumbani kwao nchini Kenya, ameshuhudia jinsi wachina wanavyoshirikiana na wenyeji katika kujenga taifa. Kwani wamewekeza sana nchini Kenya, hatua ambayo imewaletea nafasi nyingi za ajira na teknolojia mpya. Pia wananchi wa Kenya wamejifunza mengi kutoka kwa wachina ambao ni wachapa kazi kweli. Anasema ataendelea kufuatilia mkutano huo mkuu, anaona uzoefu wa China katika kuendeleza taifa unafaa kabisa barani Afrika.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu wanaofuatilia Mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China na kutuletea barua pepe kueleza maoni yao, huu ni uungaji mkono kwa kazi zetu, asanteni sana.

Msikilizaji wetu Mramba Emmanuel kutoka Tanzania ametuletea barua akisema ni mara yake ya kwanza kutuandikia barua pepe. Kitu kilichomsukuma atuandikie barua pepe, ni makala kuhusu mkoa wa Qinghai alizosoma kwenye tovuti yetu. Kabla ya hapo hajawahi kusikia habari nyingi kuhusu sehemu hiyo, ni makala zetu alizosoma kwenye tovuti ndizo zilizompa picha ya kuvutia ya mkoa huo.

Anasema yeye ni Mtanzania, na nyumbani kwao pia kuna hifadhi mbalimbali za mbuga, hali ambayo inafanana na ile ya mkoani Qinghai. Kutokana na makala zetu, amepata kujua jinsi wachina wanavyofanya kila wawezalo kuhifadhi mazingira ya asili ya maskani yao, kwa mfano huko kwenye kisiwa cha ndege, wanaendeleza shughuli za utalii bila kuathiri maisha ya ndege, hali hiyo yenye masikilizano imegusa sana hisia zake. Vilevile amevutiwa na somo la ujuzi wa mazingira shuleni. Watoto ni mustakabali wa taifa, kwa hiyo anakubali kabisa hatua hiyo ya kuwafundisha watoto tangu utotoni mwao.

Anasema katika dunia ya hivi leo, suala la mazingira linafuatiliwa na walimwengu wengi sana, hasa tatizo la kuongezeka kwa joto duniani. Afrika pia inaathirika na tatizo hilo, lakini amesoma kuwa Qinghai ni sehemu yenye umuhimu mkubwa wa mazingira, na ni chanzo cha mito mikubwa barani Asia, kwa hiyo anaona kuwa wakazi wa huko ni mashujaa walioko mstari mbele katika kuhifadhi mazingira, anatoa shukrani na pongezi kwa jitihada zao na mafanikio waliyopata. Kuhusu marufuku ya matumizi ya mifuko nyororo ya plastiki, huko nchini Tanzania marufuku kama hiyo ipo, lakini utekelezaji wake bado haujafanywa kwa makini.

Anasema amevutiwa na hatua zilizochukuliwa na Yushu katika kutekeleza marufuku hiyo, anaona inafaa hatua hizo zitekelezwe pia hata kwenye nchi nyingine ili kulinda mazingira. Anaona kuwa iwapo serikali za nchi zote zikiweza kutilia mkazo shughuli za hifadhi ya mazingira kama China inavyofanya, basi dunia yetu itakuwa na sura ya kupendeza zaidi. Anasema ana hamu ya kupata habari zaidi kuhusu Qinghai na juhudi za China katika uhifadhi wa mazingira kwa kupitia matangazo yetu. Anatutakia kazi njema.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu wa Tanzania, ambaye hakuandika jina lake kamili na anuani yake kwenye barua yake pepe kuhusu aliyosikiliza kwenye kipindi chetu cha uhifadhi wa mazingira mkoani Qinghai nchini China. Kweli amesikiliza kwa makini sana, pia ametueleza jinsi kazi ya kuhifadhi mazingira ilivyo nchini Tanzania. Maelezo yake kwenye barua hiyo kweli yanatutia moyo sana, na tunamshukuru kwa dhati.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-23