Idara ya takwimu ya Shirikisho la Uswisi tarehe 22 ilitangaza matokeo ya mwisho kuhusu uchaguzi wa bunge uliofanyika tarehe 21, kwamba Chama cha umma cha Uswisi kilipata kura nyingi zaidi kuliko vyama vingine. Kwa kuwa chama hicho kina msimamo mkali wa kutetea kuzuia vikali wahamiaji kutoka nchi za nje kuingia nchini Uswisi, na kuwafukuza vijana wahalifu pamoja na wazazi wao, ushindi wa chama hicho unawafanya watu wafuatilie kama mwelekeo wa kisiasa wa Uswisi katika siku zijazo, utakuwa wa mrengo wa kulia au la.
Chama cha umma cha Uswisi kiliundwa na wafanyakazi wa shughuli za mikono na wakazi wa sehemu ya watu wanaoongea lugha ya Kijerumani nchini Uswisi zaidi ya miaka 70 iliyopita. Chama hiki kilijitokeza mara ya kwanza kwenye uchaguzi wa bunge mwaka 1999, na mwaka 2003 kilipata asilimia 27 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi wa bunge, na kuwa chama tawala kikubwa cha kwanza. Katika uchaguzi uliofanyika tarehe 21 mwezi huu, chama hicho kilipata viti 62 kati ya viti 200 kwenye Baraza la chini la bunge, hili ni ongezeko la viti 7 kuliko kikao kilichopita. Na chama hiki kilipata asilimia 29 ya kura zilizopigwa, hii ni rekodi mpya katika historia ya uchaguzi nchini Uswisi.
Kiongozi wa sasa wa chama cha umma Bw. Christopher Blocher ni mwanasiasa aliyekuwa mwanakampuni, siku zote anajidai kuwa yeye ni "mlinzi wa mtizamo wa jadi kuhusu maadili nchini Uswisi", ambaye anapinga Uswisi kujiunga na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, anapinga nchi hiyo kuwapokea wahamiaji wengi kutoka nchi za nje, msimamo wake huo wa kuwachukia wageni ni dhahiri. Mwaka huu chama hicho kilichapisha matangazo ya kampeni ya uchaguzi yenye picha ya "Kondoo weupe wakiwafukuza kondoo weusi", kwenye matangazo hayo kondoo watatu weupe waliwafukuza kondoo weusi hadi kwenye mpaka wa Uswisi, mwelekeo dhahiri wa kuwachukia watu kutoka nje ulikosolewa na mtoa ripoti maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, pia ulikosolewa na watu wengi nchini humo. Watu wenye siasa kali wa mrengo wa kushoto waliwahi kupambana na polisi kwa sababu ya kutaka kuzuia Mkutano wa hadhara wa chama cha umma, ambapo hali ya wasiwasi ilitokea nchini humo, picha kuhusu polisi wa Uswisi kufyatua bomu la machozi dhidi ya waandamanaji iliwahi kuchapishwa kwenye kurasa za kwanza za magazeti ya Marekani na Uingereza.
Vyombo vya habari vya Uswisi vilipochambua sababu ya kupata ushindi kwa chama cha umma vilisema, utetezi wa uhafidhina wa chama cha umma unalingana na wasiwasi walio nao baadhi ya waswisi, ambao wanaogopa utandawazi wa uchumi duniani, wanahofia wahamiaji kutoka nje wataleta mzigo wa kiuchumi na kunufaika ma huduma zao za jamii, na kuleta hali wasiwasi kwenye soko la ajira; na kampeni ya uchaguzi iliyofanywa na chama hiki pia ilikisaidia chama hiki kijulikane zaidi.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, ushindi wa chama cha umma cha Uswisi utaleta athari fulani kwa hali ya mambo ya siasa nchini Uswisi. Kwanza, itakuwa vigumu zaidi kwa Uswisi kujiunga na Umoja wa Ulaya, Bara la Ulaya litakabiliwa na nchi ya Uswisi yenye msimamo mkali zaidi wa kutofanya ushirikiano. Nchi ya Uswisi ina ukosefu wa maliasili na nguvu kazi, mambo yake ya uchumi yanategemea kwa kiasi kikubwa soko la nje. Umoja wa Ulaya ni mwenzi mkubwa wa kwanza kwa Uswisi katika biashara, kutokana na kupanuka kwa Umoja wa Ulaya na kuongezeka kwa utandawazi wa uchumi kwenye umoja huo, soko la uuzaji bidhaa la Uswisi limepungua zaidi. Miaka kadhaa iliyopita viongozi wa Uswisi walitoa ushauri wa kujiunga na Umoja wa Ulaya, lakini watu wengi wa nchi hiyo hawaungi mkono ushauri huo, na chama cha umma kilipinga kithabiti zaidi kuliko vyama vingine. Aidha wahamiaji nchini Uswisi ni wengi zaidi ambao wanachukua asilimia 15 ya idadi ya watu wa nchi hiyo, hivyo utetezi wa chama cha umma wa kuwafukuza wahamiaji umewafanya wahamiaji wawe na wasiwasi, hali hii huenda itasababisha mapambano na mifarakano kati ya watu, na kuleta hali wasiwasi, hata kusababisha kupungua kwa uwekezaji wa moja kwa moja wa nchi za nje.
Wachambuzi wanasema ingawa ushindi wa chama cha umma utaleta mabadiliko kwenye mambo ya siasa nchini Uswisi, lakini bado kuna hali nyingi zinazoweza kudhibiti mwelekeo wa nchi hiyo kwenda kwenye mrengo wa kulia, walimwengu watafuatilia maendeleo ya hali ya mambo.
|