Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-24 16:40:45    
Utamaduni wa makabila madogo madogo huko Shangri-la

cri

Katika kipindi cha wiki iliyopita tuliwaletea maelezo kuhusu maisha mazuri ya watu wanaoishi kwenye sehemu ya Shangri-la mkoani Yunnan, na leo tutawaelezea utamaduni wa makabila madogo madogo ya sehemu ya Shangri-la ya wilaya ya Diqing.

Shangri-la ni mji mkuu wa wilaya inayojiendesha ya kabila la Watibet ya Diqing mkoani Yunnan kusini magharibi mwa China. Kwenye sehemu hiyo kuna makabila madogo madogo 25 yakiwemo makabila ya Watibet, Walisu, Wanaxi, Wabai, na Wayi, ukitembea kwenye mtaa wa mji wa Shangri-la, mandhari yenye umaalumu wa makabila madogo madogo itakuvutia sana.

Wapendwa wasikilizaji, mliousikia ni wimbo wa kitibet ulioimbwa na bibi Amu. Bibi huyu mwenye umri wa miaka zaidi ya 60 ni mwimbaji maarufu wa Shangri-la. Bibi Amu anajua kuimba nyimbo za kitibet za aina mbalimbali, pia anajua kutunga nyimbo papo hapo kutokana na mambo yanayotokea. Bibi Amu alisema,

"Nilianza kuimba wakati nilipokuwa mtoto. Naimba nyimbo za aina mbalimbali. Wakati nilipokuwa mtoto, nilikwenda milimani kutafuta kuni, huko nikiimba nyimbo. Watu wa kabila la Watibet ni hodari katika kutunga nyimbo, nyimbo hizo zinapaswa kuhifadhiwa vizuri."

Bibi Amu anaishi mjini Shangri-la, na mara kwa mara anaalikwa kuimba nyimbo za Kitibet kwa ajili ya kuwaburudisha wageni wanaotoka nje, na wageni hao kufurahia sana nyimbo zake. Shangri-la kuna waimbaji kadhaa hodari kama bibi Amu, pia kuna kikundi cha waimbaji vijana, ambacho mwaka 2005 kilipewa tuzo ya fedha katika mashindano ya waimbaji vijana nchini China kutokana na nyimbo zao za kiasili zilizopendwa na watu.

Kwenye sehemu ya Shangri-la, karibu kila mtu anaweza kuimba, hasa wakulima na wafugaji ni hodari zaidi katika kuimba. Msemo wa Shangri-la unasema mtu anayejua kuongoa anajua kuimba, na mtu anayeweza kutembea anaweza kucheza ngoma, na kuimba nyimbo na kucheza ngoma ni mambo muhimu sana katika maisha ya watu wa makabila madogo madogo.

Katika sherehe ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa wilaya ya Diqing iliyofanyika hivi karibuni, wakulima na wafugaji wengi waliovaa nguo zenye umaalumu wa makabila madogo madogo walicheza ngoma ili kuonesha furaha yao. Mchezaji ngoma mmoja wa kabila la Wanaxi Bw. Li Wenming alisema,

"Watu wa kabila letu la Wanaxi wanapenda zaidi kucheza ngoma ya watu wengi, hasa kwenye sherehe za sikukuu. Sikukuu yetu kubwa zaidi ni tarehe nane mwezi Februari kwa kalenda ya kilimo cha China, wavulana na wasichana wanakusanyika na kufanya sherehe ya sadaka, huku wakicheza ngoma, kuimba nyimbo, na kufanya mashindano ya kuimba nyimbo. Wakati mwingine wanakusanyika kucheza ngoma ili kujiburudisha."

Kila usiku kwenye viwanja mbalimbali mjini Shangri-la, watu hukusanyika na kucheza ngoma. Michezo hiyo inaungwa mkono sana na serikali ya wilaya ya Diqing. Mkuu wa idara ya utamaduni ya wilaya ya Diqing Bw. Pujiang ni wa kabila la Watibet, alisema,

"Ngoma hizo zilizochezwa kwenye viwanja mjini Shangri-la zilikusanywa na idara yetu ya utamaduni ya Diqing, tulikamilisha ngoma hizo na kuzieneza kwa wakazi wa Diqing. Ilituchukua nusu mwaka kuzieneza ngoma hizo. Ngoma hizo sasa zimeleta nuru kwenye maisha ya utamaduni ya watu wa Diqing."

Kwenye sehemu ya Shangri-la, watu wa makabila madogo madogo wanavaa nguo za makabila yao. Kutokana na maendeleo ya uchumi, nguo zao pia zimeboreshwa sana. Mkuu wa kikundi cha waimbaji na wachezaji ngoma za asili cha Deqin cha Diqing Bw. Zhaxi Suonapinchu ameshughulikia nguo za asili kwa zaidi ya miaka 20, alisema,

"Katika miaka ya 70 na 80 ya karne iliyopita tulikuwa maskini, na tulivaa nguo za bei ya chini. Lakini sasa tunavaa nguo nzuri, hata bei ya seti moja ya nguo nzuri zaidi imefikia yuan milioni moja. Tanavaa nguo nzuri wakati wa sikukuu, na kuvaa nguo za kawaida katika siku za kawaida."

Utengenezaji wa nguo za asili hauhitaji tu kitambaa na ngozi ya hali ya juu, bali pia unahitaji vitu vizuri vya mapambo vikiwemo vito vya thamani, mawe ya matumbawe na vitu vilivyotengenezwa kwa madini ya fedha.

Zamani nguo na mapambao ya kabila la Wazang zilitengenezwa na watu wa kabila hilo wenyewe. Hivi sasa ufundi wa kuzitengeneza umekuwa ufundi wa jadi wa wakazi wa Shangri-la, nguo na vitu vya mapambo hazikidhi tu mahitaji ya wakazi wa huko, bali pia zinapendwa na wageni kutoka nje.

Kwenye mtaa wa kale wa Dukezong mjini Shangri-la kuna maduka mengi yenye umaalumu wa asili, maduka hayo hasa yanauza mapambo. mwenyeduka wa Kamba wa kuuza mapambo yaliyotengenezwa kwa madini fedha, bibi Zhuoma alisema,

"Tulipokuwa watoto tulianza kujifunza kutengeneza vitu hivyo vya fedha, ufundi huo niliurithi kutoka kwa familia yangu. Vitu vyote vinavyouzwa kwenye duka langu tulivitengeneza sisi wenyewe. Tunapata pesa kati ya elfu 40 hadi elfu 60 kila mwaka."

Kwenye mtaa wa Dukezong, maduka hayauzi tu vitu vya fedha, bali pia yanauza vitu vingine vilivyotengenezwa kwa mikono kwa kutumia ngozi na mifupa ya ng'ombe. Hivi sasa wakati ufundi wa kutengeneza mapambo kwa mikono unapoongeza mapato ya wakazi wa Shangri-la, pia umekuwa ni dirisha la kuonesha utamaduni wa makabila madogo madogo kwenye sehemu ya shangri-la.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-24