Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-24 16:30:33    
Kuzifanya nchi zote ziwe na maendeleo ni jukumu la pamoja la jumuiya ya kimataifa

cri

Mkutano wa 62 wa mawaziri kuhusu ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya maendeleo ya uchumi ulifanyika tarehe 23 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, wajumbe kutoka nchi zaidi ya 100 na mashirika ya kimataifa walishiriki kwenye mkutano huo wa siku mbili. Kwenye mkutano katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alitoa ripoti kuhusu hali ya utekelezaji baada ya mkutano wa kimataifa uliopita kuhusu ukusanyaji wa fedha, alitathmini changamoto itakayokabili maendeleo ya uchumi duniani, na pia alieleza hali ya utekelezaji wa "Makubaliano ya Monterrey" ya kuandaa mkutano wa Doha utakaofanyika katika nusu ya pili ya mwaka kesho.

Mwaka 2002 makubaliano yalifikiwa kwenye mkutano wa kimataifa kuhusu kukusanya fedha uliofanyika mjini Monterrey, Mexico. Makubaliano hayo yalisema kila mwaka nchi zilizoendelea zitatenga 0.7% ya thamani ya uzalishaji mali ya taifa iwe misaada ya kiserikali kwa nchi zinazoendelea. Kauli mbiu ya mkutano huo wa mawaziri ni "hali ya utekelezaji wa 'Makubaliano ya Monterrey' na kazi za baadaye". Katika miaka kadhaa iliyopita hali ya utekelezaji wa makubaliano ilikuwaje? Mwenyekiti wa mkutano huo Bw. Srgjan Kerim alisema, hali ya utekelezaji wa makubaliano hayo hairidhishi.

"Katika ukusanyaji wa fedha tumekuwa kwenye njia panda, ingawa tuliahidi lakini utekelezaji unakwenda polepole kuliko tulivyotarajia, ingawa tumepata mafanikio kidogo lakini bado tuko mbali na lengo lililowekwa kwenye mkutano wa kimataifa wa mwaka 2002."

Hivi sasa nchi zinazokabiliwa na changamoto kubwa, nyingi ziko barani Afrika. Kabla ya mkutano huo, ripoti iliyotolewa na Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa ya Umoja wa Mataifa ilisema, nchi nyingi za Afrika ziwekuwa na sera za kuvutia uwekezaji binafsi wa nchi za nje, lakini wawekezaji hawajaonesha mwitikio kwa juhudi, nchi nyingi hazijatoa masharti nafuu ya kibiashara kwa nchi hizo kama zilivyoahidi, na misaada pia haikutimizwa kama nchi hizo zilivyoahidi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon kwenye mkutano huo alisema, katika miaka ya hivi karibuni ingawa maendeleo yamepatikana kwa kiasi fulani duniani kote, lakini tofauti ya maendeleo ni kubwa, nchi za kusini mwa Sahara bado hazijafuata njia ya kawaida. Alisema umuhimu wa maendeleo ya uchumi kwa amani na usalama unafahamika kwa wote, kwa hiyo kwa mara nyingine tena nchi husika zinapaswa zifanye juhudi ili kutimiza ahadi. Alisema,

"Ili kutimiza malengo ya milenia na malengo yaliyowekwa na jumuiya ya kimataifa, huu ni wakati muhimu kuliko nyakati zote zilizopita katika kujenga uhusiano wa kiwenzi unaoaminika."

Bw. Ban Ki-moon alisema, malengo hayo hakika yataweza kutimizwa, lakini masharti ya kutimiza malengo hayo ni kuwa nchi zote ziheshimu ahadi zao na zitekeleze wajibu wao. Alisema,

"Nahimiza jumuiya ya kimataifa itimize ahadi kwa juhudi zote ili kuzifanya nchi zote maskini zinufaike."

Shirika la Fedha Duniani ni chombo muhimu cha kutoa misaada kwa ajili ya maendeleo, naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Bw. Murilo Portugal alisema, ingawa changamoto ni nyingi na ni kubwa, hata hivyo ana uhakika mkubwa kuhusu kutimizwa kwa malengo ya maendeleo ya dunia nzima. Alisema,

"Uhakika wangu unatokana kuwa nchi zinazoendelea zimeanza kunufaika kutokana na mageuzi ya kiuchumi na sera za soko huria zinazorekebishwa hatua kwa hatua, hali yao ya kiuchumi imekuwa bora ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita."

Idhaa ya kiswahili 2007-10-24