Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-25 16:22:20    
Mabadiliko ya viwango vya mishahara ya watu wa China

cri

Kwa wafanyakazi wa kawaida wa China wanaotegemea mishahara, mbadiliko ya viwango vya mishahara yanahusiana moja kwa moja na maisha yao.

Mzee Du mwenye umri wa miaka 98 anaishi mjini Qingdao, mashariki mwa China. Mzee huyo sasa anaishi pamoja na familia ya mwanaye. Kabla ya kustaafu, mzee Du alikuwa anafanya kazi kiwandani, hivi sasa analipwa pensheni kila mwezi. Mzee huyo akikumbuka alisema,  "Kabla ya kuasisiwa kwa China mpya mwaka 1949, nilikuwa sipati chakula cha kutosha mara kwa mara. Na baada ya ukombozi, nilianza kuwa na mapato ya uhakika. Mwaka 1975 nilistaafu, wakati huo pensheni ilikuwa si kubwa, ni kama Yuan 70 hadi 80 hivi."

Katika miaka ya 1960 wastani wa mishahara ya wafanyakazi wa China ilikuwa Yuan 38 kwa mwezi, kiasi ambacho kulitosha kujikimu, na wakati huo watu wa China walikuwa hawana vyanzo vingine vya mapato.

Mwaka 1978 China ilianza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango. Mabadiliko makubwa yalianza kutokea katika jamii ya China. Mzee Du ambaye alikuwa amestaafu alianza kunufaika na mafanikio ya sera hiyo. Alisema"Pensheni iliongezwa kwa mara kadhaa. Nilipokuwa na umri wa miaka 80, pensheni ilifikia Yuan 1,700 kwa mwezi. Hususan mwaka 1999 nilihamia kwenye nyumba wanazoishi wazee, ambapo gharama za chakula na malazi zilikuwa Yuan 380 kwa mwezi, niliridhika na huduma za wafanyakazi wa huko."

Hivi sasa pensheni ya mzee Du imepanda imeongezeka mara 20 zaidi kuliko ile aliyokuwa anapewa wakati alipostaafu. Mzee Du anaishi kwa raha mustarehe, isipokuwa ana wasiwasi kwa mjukuu wake Bibi Xiaoxin anayefanya kazi katika mji mwingine, Shanghai.

Shanghai ni mji mkubwa wenye pilikapilika nyingi. Baada ya kuhitimu kutoka kwenye chuo kikuu, Bibi Xiaoxin alipata ajira kwenye kampuni moja ya kiserikali mjini Shanghai. Alipoanza kazi alikuwa analipwa Yuan 3,000 hivi kwa mwezi, lakini huko Shanghai gharama za nyumba ni kubwa sana, mshahara wake ulikuwa unatosha kulipia nyumba ya kupanga tu. Mwaka huu dada huyo amenunua nyumba yenye eneo la mita za mraba 60. Alisema wazo la kununua nyumba lilimjia mwaka 2006 kutokana na ongezeko la malimbikizo kwenye mfuko wa nyumba. "Pesa zinazowekwa kwenye mfuko wa nyumba ziliongezeka sana katika miaka miwili iliyopita, tunanufaika sana. Hivi sasa naweza kupata Yuan zaidi ya 1,000 kutoka kwenye mfuko huo, kiasi ambacho kiliongezeka sana, hii inasaidia kupunguza shinikizo tunalokabiliwa nalo kwa ajili ya kulipa mkopo wa nyumba."

Nchini China mfuko wa nyumba ni mfumo wa kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na nyumba za kuishi. Kila mwezi mfanyakazi anatoa asilimia fulani ya mshahara na kampuni anayofanyia kazi pia inatoa fedha kiasi hicho hicho, fedha za pande hizo mbili zinawekwa kwenye akanti maalumu. Mfanyakazi akinunua, au kupanga au kukarabati nyumba, anaweza kutumia fedha hizo. Sawa na mishahara, fedha zinazowekwa kwenye mfuko wa nyumba pia zinaongezeka sambamba na kuongezeka kwa muda wa utumishi wa wafanyakazi.

Mwaka 2006 kutokana na msaada wa wazazi wake na mkopo wa benki, Bibi Xiaoxin alinunua nyumba kwenye sehemu ya katikati ya Shanghai, na analipa mkopo kwa mwezi kwa kutumia mfuko wa nyumba.

Baba wa Xiaoxin ni msimamizi wa ngazi ya kati kwenye kampuni moja ya ubia. Yeye alieleza kuridhika na kiwango cha mshahara wake. Alisema "Nilianza kazi kwenye kampuni ninayofanyia kazi sasa mwaka 1990. Wakati huo nilikuwa nalipwa Yuan 400 tu kwa mwezi. Sambamba na utekelezaji wa sera ya mageuzi na kufungua mlango pamoja na kuongezeka kwa faida ya kampuni, hivi sasa mshahara wangu ni karibu mara 10 zaidi kuliko ule niliokuwa napata mwaka 1991."

Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2006 wafanyakazi wa China walilipwa Yuan trilioni 23 kwa jumla, kiasi ambacho ni ongezeko la asilimia 13.5 kuliko mwaka 2005. Ongezeko la mapato limesababisha kubadilika kwa mtizamo wa watu wa China katika namna ya kutumia pesa zao. Zamani watu walitumia sehemu kubwa ya mishahara yao kwa ajili ya chakula, lakini hivi sasa matumizi kwenye nguo, vyombo vya umeme, elimu, nyumba, utalii na burudani yameongezeka.

Baba wa Xiaoxin alisema  "Zamani tulijitahidi kupata chakula na mahitaji mengine ya kimsingi. Hivi sasa tuna uwezo mkubwa zaidi, kwa hiyo tunalenga mambo makubwa zaidi. Mwaka 1980 nilinunua televisheni ya inchi 9 inayoonesha picha zenye rangi nyeupe na nyeusi tu. Baadaye sambamba na maendeleo ya jamii, nilibadilisha televisheni hiyo kwa televisheni ya rangi ya inchi 17, na hivi sasa tunatizama televisheni kubwa ya rangi ya inchi 29. Teknolojia ya televisheni imeendelezwa na nina mpango wa kununua ile inayotumia teknolojia ya kisasa. Mbali na hayo, hivi sasa tunazingatia sana kiwango cha maisha yetu na kujenga afya. Kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha, tuna uwezo wa kutumia pesa katika shughuli za kujenga afya, kwa mfano kununua vyakula vyenye virutubisho, kufanya mazoezi ya kujenga mwili na hata kufanya utalii."

Huko Shanghai, Bibi Xiaoxin ana mpango wa kwenda nchi za nje kuendelea na masomo baada ya kulimbikiza pesa za kutosha, na huko Qingdao baba yake anataka kununua televisheni kubwa zaidi ya kisasa, huku babu yake akiwa anaishi kwa raha mustarehe kwa kutegemea pensheni. Watu hao kutoka familia ya kawaida nchini China wanajitahidi kutimiza ndoto mbalimbali kwa kutumia mishahara yao.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-25