Tarehe 24 Oktoba ni siku ya maadhimisho ya miaka 62 tangu Katiba ya Umoja wa Mataifa ianze kufanya kazi na tangu Umoja wa Mataifa uanzishwe. Siku hiyo shughuli za maadhimisho zilifanyika huko New York, kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa na katika miji mikuu ya nchi nyingi duniani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa hotuba akitoa mwito wa kuitaka jumuiya ya kimataifa ifanye juhudi za pamoja ili kuuwezesha Umoja wa Mataifa uoneshe umuhimu wake kwa mafanikio zaidi, na kuwa kiini cha mfumo wa ushirikiano wa pande nyingi ambao ni lengo la pamoja la jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Mataifa ni jumuiya ya kimataifa ya serikali za nchi mbalimbali iliyoanzishwa baada ya kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia. Kuanzishwa kwake kunaonesha kuthibitishwa kwa uhusiano wa kimataifa wa aina mpya. Lakini Umoja wa Mataifa ulioanzishwa katika hali hiyo wakati huo ulikuwa unaonesha fikra ya "utawala wa nchi kubwa", lakini kanuni ya "kauli moja ya nchi kubwa" pia inasisitiza wajibu wa pamoja wa nchi kubwa katika kushughulikia mambo ya kimataifa, hii imeonesha matumaini ya binadamu ya kutaka kutumia kanuni zinazotambuliwa na wengi katika kutatua masuala ya pamoja ya dunia nzima, hali hii kwa kweli ilikuwa hali asili ya ushirikiano wa pande nyingi tunayosisitiza hivi leo. Zaidi ya miaka 60 iliyopita, Umoja wa Mataifa umeonesha umuhimu wake mkubwa katika kulinda amani na usalama wa dunia na kusukuma mbele maendeleo ya jamii ya binadamu, Umoja wa Mataifa umekuwa jumuiya kubwa ya kimataifa isiyokosekana katika jamii ya binadamu.
Lakini Umoja wa Mataifa umekubalika na kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa siku hadi siku baada ya kupita mitihani mingi katika miongo kadhaa iliyopita, pamoja na kukabiliana na changamoto ya maamuzi ya upande mmoja katika miaka ya hivi karibuni. Mafunzo ya vita vya Iraq yanatosha kuifanya jumuiya ya kimataifa ijikosoe kwa kina, wakati huo huo, masuala makubwa ya dharura yanayowakabili binadamu katika zama za utandawazi wa uchumi duniani kuhusu kuondoa umaskini, mabadiliko ya hali ya hewa, upunguzaji wa silaha na kuzuia kuenea kwa silaha za nyukilia, na kulinda haki za binadamu, yote hayo yanaihimiza jumuiya ya kimataifa itoe hoja kwamba, binadamu wote wanatakiwa kushirikiana zaidi na kufanya juhudi za pamoja katika kuzuia na kuepusha vita, na kujenga mazingira ya amani chini ya uongozi, uratibu na uingiliaji wa lazima wa mfumo wa ushirikiano wa pande nyingi ambao kiini chake ni Umoja wa Mataifa. Kama alivyosema katibu mkuu Ban Ki-moon kwenye risala aliyosoma siku ya Umoja wa Mataifa mwaka huu kwamba, hali ya dunia inaendelea kwa mwelekeo unaosaidia Umoja wa Mataifa, na watu wengi zaidi wametambua umuhimu wa ushirikiano wa pande nyingi, hivi leo binadamu wanategemeana na kukuza utandawazi wa uchumi duniani, ni lazima kukabiliana na masuala ya dunia nzima kwa mpango wa dunia nzima, hii ni njia pekee sahihi ya ufumbuzi wa matatizo.
Kutokana na matumaini yaliyoelezwa na nchi nyingi duniani, mfumo wa ushirikiano wa pande nyingi chini ya kiini cha Umoja wa Mataifa unawataka watu wajenge utaratibu mpya ulio wa haki na halali duniani, kuufanya uhusiano wa kimataifa uwe wa Kidemokrasia, na kuhimiza kuwepo kwa ncha mbalimbali duniani. Kuufanya uhusiano wa kimataifa uwe wa Kidemokrasia kunamaanisha kuwa nchi kubwa na ndogo, nchi maskini na tajiri, na nchi yenye nguvu na dhaifu zote ni wanachama wenye usawa katika jumuiya ya kimataifa, zinapaswa kuheshimiana, kufanya mashauriano katika hali ya usawa, na nchi yoyote haina haki ya kuilazimisha nyingine ikubali nia yake; na kuwepo kwa ncha mbalimbali duniani kunamaanisha kuwepo kwa nguvu za aina mbalimbali katika hali ya masikilizano na maendeleo yenye uwiano, ili kulinda pamoja utulivu wa jumuiya ya kimataifa. Baada ya kutimiza malengo hayo, ndipo utaratibu mpya utakapoweza kuanzishwa kwa pande zote, ili nchi mbalimbali ziheshimiane kisiasa, zihimizane kiuchumi na kutafuta maendeleo ya pamoja; zifundishane kiutamaduni ili kupata ustawi wa pamoja; ziaminiane katika mambo ya usalama ili kulinda pamoja amani na maendeleo ya binadamu wote.
Jumuiya ya kimataifa inatakiwa kufanya juhudi za pamoja katika kusukuma mbele mageuzi ya Umoja wa Mataifa hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili liweze kukabiliana na hali ilivyo sasa duniani.
|