Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-29 16:44:28    
Je Marekani itashambulia Iran?

cri

Hivi karibuni, msimamo wa serikali ya George Bush dhidi ya Iran umekuwa mkali zaidi, na maneno ya kutishia kutaka kuishambulia Iran yanasikika mara kwa mara. Watu wengi wanajiuliza, je kweli Marekani itaishambulia Iran?

Tarehe 17 rais George Bush kwa mara nyingine kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema, kama Iran ikiwa na silaha za nyukilia, basi itatishia usalama wa dunia, na huenda itasababisha kutokea kwa vita vya tatu vya dunia. Tarehe 21 makamu wa rais wa Marekani Bw Dick Cheney alionya kuwa nia ya Iran ya kujipatia silaha za nyuklia itailetea "matokeo mabaya sana". Hali kadhalika waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice kwenye bunge pia alisisitiza kuwa, Iran itakuwa ni tishio kubwa dhidi ya usalama wa Marekani.

Mbali na hayo wiki iliyopita Bi. Condoleezza Rice alitangaza Marekani kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya idara zaidi ya 20 za kiserikali, benki na watu binafsi, na ikiwa ni pamoja na vikwazo vikali kwa wizara ya ulinzi ya Iran na jeshi la ulinzi la mapinduzi ya Kiislamu la Iran. Hatua hizo ni kali kabisa kuchukuliwa toka mwaka 1979 wakati uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulipovunjika, na pia ni mara ya kwanza kwa Marekani kulitangaza jeshi la taifa moja kuwa kundi la kigaidi.

Pamoja na hayo, wahafidhina wapya wanaounga mkono na kuichochea serikali ya Bush kuishambulia Iran pia wameanza shughuli zao. Hivi karibuni, Rais George Bush alifanya mazungumzo na mwungaji mkono mkubwa wa wahafidhina kwa muda wa zaidi ya dakika 40 kuhusu suala la Iran. Mwungaji mkono huyo alimhimiza Bw. George Bush achukue mapema hatua za mabavu dhidi ya Iran. Si hayo tu bali vile vile mwungaji mkono huyo wa wahafidhina aliandika makala akimfananisha Bw. Mohamoud Ahmadinejad na Hitler, na kusema kwamba Iran inataka kufanya mapinduzi ya utaratibu wa sasa wa kimataifa na kuitawala dunia kwa ufashisti.

Aidha watu kadhaa wanaotafuta nafasi ya kugombea urais wa Marekani wa Chama cha Republican pia wanakubali kuichukulia Iran hatua kali, kwa kauli moja wote wanaishutumu Iran kuunga mkono ugaidi na kutetea kuichukulia Iran hatua kali ikiwa pamoja na kutumia mabavu. Meya wa zamani wa New York Bw. Rudolph Juliane alisema, kama akichaguliwa kuwa rais wa Marekani, hataruhusu kabisa Iran imiliki silaha za nyuklia. Alisema, Marekani lazima iwe na msimamo mkali dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kijeshi.

Kutokana na maneno kama hayo, wachambuzi wanaona kuwa serikali ya George Bush inavyosema hivi sasa, inafanana na ilivyosema kabla ya kuanzisha vita dhidi ya Iraq, itakayofuata ni kuwa serikali ya Marekani itasema imetumia njia zote za kidiplomasia na za kiuchumi bila mafanikio, lakini ili kuzuia Iran isimiliki silaha za nyukilia vita ni njia pekee. Wachambuzi wanaona kuwa vita dhidi ya Iran vinakaribia.

Wachambuzi wa mambo ya kijeshi nchini Marekani wana uhakika kwamba Marekani hakika itaishambulia Iran. Wanasema baada ya Marekani kuitangaza wizara ya ulinzi na jeshi la ulinzi kuwa kundi la kigaidi, Marekani imeiorodhesha Iran kwenye harakati zake za mapambano dhidi ya ugaidi duniani.

Lakini pia kuna baadhi ya watu wanaoona kuwa, vikwazo vilivyowekwa na Marekani ni sehemu ya njia za kidiplomasia za Marekani, lengo lake ni kuishinikiza Iran iache mradi wa nyukilia na kusimamisha kuunga mkono vikundi vya Iraq vinavyoipinga Marekani, lakini hii si dalili ya kuanzisha vita. Serikali ya George Bush pia iliwahi kusema kwamba itashikilia njia ya kidiplomasia kutatua suala la Iran. Lakini kadiri msimamo wa Marekani unavyozidi kuwa mkali, watu wa Marekani wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Iran.