Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-30 19:19:42    
Barua 1028

cri

Michezo ya 29 ya Olimpiki ya majira ya joto itafunguliwa mwezi Agosti mwaka 2008. Ili kuwawezesha wasikilizaji wetu waelewe vizuri zaidi na kushiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 na kuenzi moyo wa Michezo ya Olimpiki, kuanzia tarehe 1 Novemba mwaka 2007 hadi tarehe 25 Aprili mwaka 2008, idhaa mbalimbali za Radio China Kimataifa zitatangaza makala 4 za Mashindano ya chemsha bongo yasemayo: Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki, makala hizo zinahusu "Maendeleo ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing", "Kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing na wanasesere wa alama ya Baraka ya michezo hiyo", Viwanja na majumba ya michezo vya Michezo ya Olimpiki ya Beijing" na "Miji mingine itakayoshirikiana na Beijing kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008".

Kama ilivyokuwa kwenye mashindano ya miaka iliyopita, kila baada ya kusoma makala moja, tutauliza maswali mawili. Baadaye kamati yetu ya uthibitishaji itachagua wasikilizaji washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu pamoja na nafasi maalum.

Kila mshiriki wa mashindano hayo ya chemsha bongo atapata kadi moja ya kumbukumbu; washindi watakaopata nafasi za kwanza, pili na tatu watapewa kadi ya kumbukumbu na zawadi; na wasikilizaji washindi watakaopata nafasi maalum wataalikwa kuja China ambapo watapewa tuzo ya kikombe na kadi, watatembelea mji wa Beijing kwa siku 10, watatembelea viwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki na kukutana na wachezaji maarufu wa China.

Kuanzia tarehe 11 Novemba, kwenye Kipindi cha Sanduku la Barua, Idhaa ya Kiswahili itatangaza rasmi makala nne za mashindano ya chemsha bongo zisemazo: Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki. Na matangazo ya makala hizo nne yatarudiwa kuanzia tarehe 9 Desemba mwaka huu, msikose kutusikiliza.

Sasa tunawaletea barua tulizopata kutoka kwa msikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Kaziro Dutwa wa S.L.P 209 Songea, Ruvuma, Tanzania ametuletea barua akisema, anafarijika sana kupata wasaa huu kwa mara nyingine kuweza kutuandikia waraka huu mfupi akitumai kuwa sote tu wazima wa afya njema, na afya yake ni buheri wa afya. Bwana Dutwa anasema tangu mwezi wa pili mwaka huu hakuwa na nafasi ya kusikiliza wala kutuandikia barua, kwani alikuwa kwenye majukumu mazito ya kikazi, bila shaka amekosa mambo mengi sana yaliyojiri kwenye matangazo yetu kwani kutoka mwezi wa pili hadi mwanzoni mwa mwezi wa saba ni kitambo kirefu sana!

Anasema alipoanza kutusikiliza, aligundua mambo mengi sana yameongezeka na mengine mengi yamefanyiwa marekebisho ambayo yameleta ladha murua na kunogesha zaidi matangazo yetu na vipindi vyetu kwa ujumla. Mfano wa kipindi ambacho kimebadilika sana ni kile cha salaam; awali kipindi hiki kilikuwa ni kifupi sana na hakukuwa na muziki mnono wa kusindikiza salamu hizo! Lakini leo ni kinyume kabisa, baada ya salamu kusomwa muziki unapigwa kusindikiza salamu hizo, hakika hii inatia motisha sana. Siyo kama unapigwa muziki tu bali pia muziki unamalizika kabisa, si hayo tu bali kuna mambo mengi mengineyo ambayo yameongezeka ambayo ni mazuri sana! Anaona kuwa hatua hiyo bila shaka kubwa, lakini kama kawaida hatua zaidi zinahitajika ili kukidhi kiu ya wasikilizaji.

Pia anasema amekuta zawadi ya jarida zuri la "China Today". Hakika limemfurahisha sana kwa makala zake, picha nzuri za kupendeza, hakika amevutiwa sana na makala inayohusu "Viriba-tumbo nchini China". Makala hii imeeleza kwa kirefu juu ya madhara na athari nyingine za viriba tumbo, njia za kuzuia au kuviondoa. Njia mbalimbali zimetajwa zikiwemo: njia maalum ya matibabu ya kichina: Akyupancha, kufanya mazoezi, kuacha uvivu hasa wa mazoezi au kubweteka na kubadili milo, pia kuna mengi sana ya kujifunza. Bwana Dutwa anasema sasa anaendelea kusikiliza vipindi vyetu kwa bidii ili kuvielewa vizuri, ili atuandikie kirefu iwapo kunahitajika mabadiliko au kuboresha zaidi kwa sasa vipindi vyetu anavyoviona vipya na vigeni kidogo kwake. Bila shaka tutakuwa pamoja hewani hadi atakapoandika barua yake nyingine.

Tunafurahi kupata barua ya Bwana Kaziro Dutwa na tunamshukuru sana, ingawa siku nyingi alikuwa hajawasiliana nasi, lakini tunaelewa hali yake ya kuwa na pilikapilika za kazi, na tunajua msikilizaji wetu huyo wa tangu zamani sana hakika anatufuatilia na akipata nafasi anaweza kusikiliza vipindi vyetu kwa makini, ili kuleta maoni na mapendekezo, ni matumaini yetu kuwa mawasiliano na urafiki kati yetu utaendelea kudumu daima, na tunamtakia kila la heri.

Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa S.L.P. 69 Injinia, Kinangop ya Kaskazini, Kenya ametuletea barua akisema, ana matumaini makubwa kuwa sote hatujambo. Anasema anachukua fursa hii kuwapa hongera wasikilizaji kumi kutoka nchi mbalimbali za ng'ambo walioshinda nafasi maalum katika Chemsha Bongo iliyoanza tarehe 27-11-06 na kumalizika tarehe 15-4-07.

Ushindi huu umewapa nafasi ya kualikwa kuutembelea mkoa wa Sichuan, maskani ya panda. Safari hii bila shaka itakuwa ya kuvutia kwani watajionea vivutio vingi kama vile Bonde la Jiuzhaigou lenye vijiji tisa vya kabila la Watibet. Watajionea pia Mlima E Mei ulio mmoja kati ya sehemu takatifu za dini ya Kibuddha nchini China, na huenda pia watajionea sanamu ya Buddha mkuu ya Leshan ambayo ni sanamu kubwa kabisa duniani. Mwisho anapenda kuwasalimu, Baba yake Mwangi Gichimu akiwa Injinia, Kenya, Mama yake Margaret Muthoni akiwa Injinia, Kenya, na Mke wake Joyce Waithera Mungai akiwa Injinia, Kenya.

Msikilizaji wetu Mbarak Mohammed Abucheri wa sanduku la posta 792 Kakamega Kenya ametuletea barua kwanza akianza kuwasalimu watangazaji na wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa na watu wachina kwa jumla wanapoadhimisha miaka 10 tangu Hongkong irejee China tarehe 1 Julai, 1997. Anasema ama kwa hakika Hongkong kama mkoa wa utawala maalum umepata ustawi na utulivu baada ya kuandaa kwa ushindi Mkutano wa kila mwaka wa Benki ya dunia na Shirika la fedha la kimataifa. Mamia ya mawaziri wa fedha, mameneja wa mabenki na maofisa wanaohusika na mambo ya fedha kutoka nchi mbalimbali, walihudhuria Mkutano huo, na waliona mafanikio yalipatikana huko Hongkong. Hongkong inashiriki katika biashara ya rejareja, utalii, hoteli na hata katika masoko ya hisa, na uuzaji wa nyumba, vilevile Hongkong ina msingi imara wa uchumi na akiba kubwa ya fedha za kigeni, hivyo kuhimili na kushikilia uwiano wa thamani ya dola ya Hongkong na fedha za kigeni, na kizuri zaidi ni kuwa maingiliano baina ya Hongkong na China bara yameimarika zaidi.

Anasema wanafurahi kusikia kuwa mfumo na desturi za Hongkong hazibadiliki, lakini wahongkong wamebadilika katika hisia zao za kulipenda taifa lao, na wana uhakika kuwa sera ya nchi moja mifumo miwili na wahongkong kuiendesha Hongkong itakuwa na mafanikio kiuchumi na kuleta maendeleo. Anasema pia hana budi kuwapongeza watangazaji wa Radio China Kimataifa kwa juhudi za kuhakikisha wasikilizaji wetu wanapata habari kwenye vipindi mahsusi vilivyowafahamisha kuhusu mkoa wa utawala maalum wa Hongkong, ambao ni kituo cha mambo ya fedha duniani. Hivyo basi yeye anaungana na wahongkong na wachina katika kuadhimisha miaka 10 tangu Hongkong irejee China kwa kupandishwa Bendera nyekundu ya nyota tano ya taifa la China na Bendera ya mkoa wa utawala maalum wa Hongkong, China iliporejesha mamlaka ya utawala wa Hongkong kutoka kwa Uingereza.

Anasema anachukua fursa kuomba uongozi wa Radio China Kimataifa umtumie picha za majengo ya kituo bora cha utalii na vivutio mbalimbali vinavyoifanya Hongkong kuwa mahali pazuri pa kuzuru, pia atafurahi akitumiwa DVD ili kuufahamu mkoa wa Hongkong kwa karibu na kwa undani zaidi, pia atashukuru akitumiwa ramani ya China pamoja na ya mkoa wa utawala maalum wa Hongkong. Anatutakia kila la kheri na Baraka watangazaji na wafanyakazi wote wa CRI.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Mbarak Mohammed Abucheri kwa barua yake ya kutuelezea usikivu wake wa vipindi vyetu kuhusu maadhimisho ya miaka 10 tangu Hongkong irudi China. Ufuatiliaji wa makini wa wasikilizaji wetu unatuhimiza tuchape kazi zaidi kwa ajili ya kuandaa vizuri zaidi vipindi vyetu ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu, na maombi yako kuhusu picha zinazohusu mambo ya Hong Kong yametufikia.