Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-31 18:36:30    
Elimu ya ufundi wa kazi ya mkoani Xinjiang inavyosaidia wanafunzi kupata ajira bila matatizo

cri

   

Mwaka 2007 wanafunzi wapatao milioni 5 wamehitimu kutoka vyuo vikuu nchini China. Wakati wengi wao bado wakihangaika kupata ajira, wanafunzi wengi wa vyuo vya ufundi vya mkoa unaojiendesha kabila la wauyghur wa Xinjiang wamepata ajira bila matatizo. Takwimu zimeonesha kuwa, mwaka huu asilimia 90 ya wanafunzi waliohitimu kutoka vyuo hivyo wamepata ajira.

Mwaka huu wanafunzi 2400 walihitimu kutoka chuo cha ufundi wa kazi wa viwanda vyepesi cha Xinjiang, na asilimia 95 kati yao wameajiriwa; katika chuo cha ufundi wa kazi cha Kelamayi cha Xinjiang asilimia 92 ya wahitimu wamepata ajira; idadi ya wanafunzi wahitimu waliopata ajira wa chuo cha ufundi wa kilimo cha Xinjiang imedumisha kiwango cha juu cha asilimia 96 kwa miaka mitatu mfululizo. Katika chuo kikuu cha ufundi wa mashine na elektroniki cha Xinjiang, katika miaka ya hivi karibuni idadi ya wanafunzi wahitimu haijatosheleza mahitaji ya viwanda. Mkuu wa chuo hicho Bw. Wang Jianming alisema:

"katika miaka ya hivi karibuni, wanafunzi wanaohitimu katika fani ya mashine na usimamizi wa chuo chetu hawakidhi mahitaji ya jamii, na wote waliosoma masomo hayo wamepata ajira mara baada ya kuhitimu. Hata makampuni kutoka sehemu nyingine yalikuja kwenye chuo chetu kuandikisha wanafunzi, wanafunzi wanaohitimu mwaka huu wote wameajiriwa. Hata wanafunzi watakaohitimu mwaka 2008 na 2009 wameanza kuombwa kuandikishwa."

Katika miaka ya hivi karibuni, mkoa unaojiendesha wa kabila la wauyghur wa Xinjiang umeweka mkazo katika elimu ya ufundi wa kazi, katika miaka miwili iliyopita, serikali ya huko imetenga Yuan milioni 300 katika ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi wa kazi. Hivi sasa mkoa huo una vyuo 250 vya mafunzo ya ufundi, pamoja na shule zaidi ya elfu mbili za ufundi wa kazi kwa ajili ya wakulima na wafugaji na matawi zaidi ya elfu 8 ya shule hizo vijijini. Mtandao wa elimu ya mafunzo ya ufundi wa kazi katika mkoa mzima wa Xinjiang umeanzishwa.

Wakati wa kuendeleza hatua kwa hatua mbinu ya elimu ya mafunzo ya ufundi wa kazi, vyuo na shule mbalimbali za mafunzo ya ufundi wa kazi mkoani humo zimefanya juhudi kuanzisha utaratibu mpya wa elimu, kusukuma mbele ushirikiano kati ya shule na makampuni na kuanzisha utaratibu wa kuchanganya masomo ya darasani na mazoezi ya kazi. Masomo yaliyowekwa yanahusiana kwa karibu na mahitaji ya kazi, na elimu ya ufundi wa kazi inalenga kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Idara ya upashanaji na utangazaji wa habari katika chuo cha ufundi wa kazi wa viwanda vyepesi cha Xinjiang ilianzishwa kwa pamoja na gazeti la uchumi la Xinjiang, chuo hicho kilisaini mkataba wa kuajiri wanafunzi wakati kilipoanzishwa. Mwezi Julai mwaka huu, wanafunzi zaidi ya 80 walipita kwenye mtihani wa kuhitimu mafunzo na wote wamepata ajira. Ushirikiano huo kati ya vyuo na makampuni umetatua kwa haraka na kwa ufanisi suala la kupata ajira kwa wanafunzi wahitimu, makampuni mbalimbali pia yanaikubali njia hiyo. Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa nguvukazi ya gazeti hilo Bw. Wu Hongming alisema:

"Hivi sasa bado ni ngumu kwa makampuni ya magazeti kuajiri watu hodari wenye ujuzi maalum. Katika kampuni yetu, licha ya wahariri na waandishi wa habari, wafanyakazi wengi zaidi wanashughulikia utangazaji na uchapishaji. Lakini hivi sasa bado hakuna shule zinazotoa mafunzo maalum kuhusu utangazaji na uchapishaji, ndiyo maana tulianzisha ushirikiano huo. Kwa wanafunzi hao 80, shule inafundisha masomo ya msingi, na kampuni yetu inawafundisha masomo maalum."

Muda mfupi baada ya kutolewa kwa utaratibu huo wa ushirikiano kati ya vyuo na makampuni, utaratibu huo ulianza kuenezwa kote mkoani Xinjiang. Mkurugenzi wa ofisi ya chuo cha ufundi wa kilimo cha Xinjiang Bw. Zhu Lihong alipofafanua utaratibu huo alisema:

"tulifanya uvumbuzi kwa utaratibu wetu wa elimu na kuanzisha utaratibu wa kunufaisha pande mbalimbali. Chuo chetu kumefungua mlango na kuanzisha ushirikiano mbalimbali na makampuni, hata wanafunzi wetu wanaweza kufundishwa hapo papo au kufanya mazoezi ya kazi viwandani. Baada ya masomo ya miaka miwili na nusu, wanafunzi wataanza kufanya mazoezi katika makampuni ambayo wataajiriwa baada ya kuhitimu."

Mbali na hayo, Chuo cha ufundi wa kilimo cha Xinjiang pia kimeanzisha ushirikiano na vyuo mbalimbali vya nchini na vya nchi za nje, ili kutumia kwa ufanisi raslimali za elimu na kuandaa wataalamu hodari. Mwezi Desemba mwaka 2004, chuo kikuu kilianzisha ushirikiano na chuo cha Stamford ambacho ni chuo kikubwa kabisa binafsi nchini Malaysia na kimejenga tawi la chuo kikuu cha Stanford. Mwezi Juni mwaka huu, kundi la pili la wanafunzi wa chuo hicho walienda kwenye chuo cha Stamford kuendelea na masomo yao.

Kutokana na uvumbuzi huo wa utaratibu wa elimu, hivi sasa elimu ya mafunzo ya ufundi wa kazi mkoani Xinjiang imepata maendeleo makubwa. Hali ya zamani ya shule hizo zenye tatizo la kuandikisha wanafunzi na ugumu kwa wanafunzi kupata ajira imeondolewa, hivi sasa shule hizo zinafuata njia ya maendeleo endelevu.