Baada ya kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango karibu miaka 30 iliyopita, China imeingia kwenye safu ya nchi tatu zenye nguvu kubwa kabisa katika mambo ya biashara duniani. Kwenye kongamano maalum kuhusu "Umuhimu wa China katika biashara kote duniani", Mjumbe wa China kwenye Shirika la biashara duniani Balozi Sun Zhenyu alisema, China imekuwa nchi kubwa kibiashara inayoleta fursa nyingi zaidi kwa dunia nzima.
Balozi Sun alisema, katika historia China iliwahi kuwa ni nchi kubwa kibiashara. Katika miaka ya hivi karibuni, kasi ya uagizaji wa bidhaa wa China kutoka nchi za nje imewashangaza watu kama ilivyo kasi ya uuzaji bidhaa nje wa China. Alisema:
"Mwaka 2001, thamani ya uagizaji wa bidhaa wa China kutoka nchi za nje ilikuwa dola za kimarekani bilioni 243, na mwaka 2006, thamani hiyo iliongezeka na kufikia dola za kimarekani bilioni 790. Kuanzia mwaka 2001 hadi 2006, wastani wa ongezeko la mwaka la thamani ya biashara hiyo kati ya China na nchi nyingine zinazoendelea ulikuwa asilimia 65. Na mwaka jana kiasi cha mchango wa China kwa ongezeko la uchumi wa dunia kilifikia asilimia 25".
Balozi Sun Zhenyu alisema, China iliagiza pamba kutoka kwa nchi kadhaa za Afrika ambazo ni nchi zinazozalisha pamba kwa wingi zaidi, kufanya hivyo kumepunguza hasara kwa wakulima wa pamba wa Afrika kutokana na wakulima wa pamba wa Marekani kuuza pamba kwa bei chini kwa wingi na kusababisha bei ya pamba kwenye soko la dunia kuanguka.
Kuhusu watu wanaofuatilia kama China itatimiza maendeleo endelevu au la, Balozi Sun alisema serikali ya China imeweka mpango wazi kuhusu mustakabali wa maendeleo, na China haitachukua ongezeko la thamani ya jumla ya uzalishaji wa mali kuwa lengo pekee la kutathimini maendeleo yake. Alisema:
"Kwenye Mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China uliofanyika hivi karibuni, katibu mkuu wa chama Bw. Hu Jintao alieleza sera mbalimbali za China kuhusu kujenga jamii yenye masikilizano, kutoa kipaumbele katika kuboresha maisha ya wananchi, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kushughulikia mazingira ya asili, na kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati, sera hizo zitaielekeza China katika njia ya kujipatia maendeleo katika siku zijazo".
Alipozungumzia kazi inayostahili kufanywa na China katika biashara duniani na katika Shirika la biashara duniani, Bw. Sun alisema katika miaka 6 iliyopita tangu China ijiunge na Shirika la biashara duniani WTO, China inafuata kwa makini kanuni mbalimbali, na kuonesha sura yake ya nchi inayowajibika. Wakati huo huo China inazingatia ufuatiliaji wa nchi kadha wa kadha kuhusu maslahi, kutilia maanani utaratibu wa biashara ya pande nyingi, ambapo China inapenda kuchukua hatua mwafaka kunufaishana na wenzi wake wa biashara, ili kupata maendeleo ya pamoja. Alisema China ikiwa nchi inayoendelea itaunga mkono kithabiti nchi zinazoendelea kulinda maslahi yao. Alisema:
"China itafanya ushirikiano barabara na nchi zinazoendelea ambazo ni wanachama wa Shirika la biashara duniani WTO, kwani China na nchi hizo zina maslahi ya pamoja, na maoni yanayofanana, China inaunga mkono kithabiti matakwa halali ya nchi wanachama zinazoendelea, hasa China inapaswa kulinda maslahi ya nchi zile zilizoko nyuma kabisa kimaendeleo".
Balozi Sun aliongeza kuwa, China imesaini makubaliano ya ushirikiano wa kikanda na nchi nyingi na jumuiya nyingi za kikanda, na imefungua soko lake kwa bidhaa za nchi zilizoko nyuma kimaendeleo, kufuta ushuru wa bidhaa zao na kuzisaidia nchi hizo kujiendeleza.
Balozi Sun pia alidhihirisha kuwa, kuhusu China kuwa nchi kubwa kibiashara, nchi kadhaa za magharibi hazichukulii hali hiyo halisi kuwa ni fursa, bali zinaona ni changamoto dhidi yao, hivyo zikachukua hatua za kujilinda kibiashara, ambapo China ikawa shabaha kubwa kabisa duniani kwa nchi mbalimbali kupinga uuzaji wake wa bidhaa zenye bei ya chini, hata kutoa mashitaka mara kwa mara dhidi ya China kwa Shirika la biashara duniani. Hata hivyo nia imara ya China ya kushikilia kufuata njia ya mageuzi na ufunguaji mlango haibadiliki hata kidogo.
|