Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-01 16:00:17    
Mahakama ya Hispania yatoa hukumu kuhusu tukio la "Machi 11"

cri

Mahakama ya taifa ya Hispania tarehe 31 Oktoba ilitoa hukumu kuhusu milipuko iliyotokea "Machi 11" mwaka 2004 ambayo ililipua magarimoshi manne mfululizo, wahalifu wakuu watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka zaidi ya elfu 30 na miaka zaidi ya elfu 40.

Siku hiyo saa mbili asubuhi majaji watatu akiwemo jaji mkuu wa mahakama ya taifa ya Hispania walikagua na kusaini kisha waliwasomea watuhumiwa 21 hukumu yenye kurasa 600. Baada ya muda wa saa nne, saa 6 na nusu hivi kwa saa za huko hakimu mkuu wa mahakama ya taifa Bw. Gomez Bermudez aliwatangazia watu elfu kadhaa waliodhurika waliokuwa wanasubiri kusikia hukumu hiyo nje ya mahakama.

Hukumu hiyo ikiwa ni pamoja na watu wawili wa Morocco ambao wamethibitishwa kuwa ni watekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi na kuhukumiwa kifungo cha miaka 42924 na 42922 gerezani, mwingine ni Mhispania aliyewapatia magaidi baruti alihukumiwa kifungo cha miaka 38976. Watuhumiwa wengine 18 wamehukumiwa vifungo vya miaka toka mitatu hadi 23.

Asubuhi ya tarehe 11 Machi mwaka 2004, magarimoshi manne ya mjini Madrid, mji mkuu wa Hispania, yalikumbwa na milipuko mfululizo na kusababisha vifo vya watu 192 na wengine 1500 kujeruhiwa. Hilo ni tukio la ugaidi ambalo watu wa Hispania wanaliita tukio la "Septemba 11" nchini Hispania, na ni tukio kubwa la ugaidi katika historia ya Hispania. Tokea mwezi Juni mwaka 2004 kutokana na msaada wa polisi wa kimataifa, watuhumiwa 29 walioshiriki kwenye njama na milipuko wamekamatwa. Baada ya upelelezi wa miaka mitatu kukamilika, mwishowe mahakama ya Hispania imefikia kutoa hukumu kwa watuhumiwa hao.

Kwa mujibu wa sheria ya Hispania, nchini humo hakuna adhabu ya kifo, hatia yoyote inahukumiwa vifungo vya miaka tofauti. Hukumu ya kifungo cha miaka mingi kabisa kwa kosa la ugaidi ni miaka 40. Miaka ya hukumu kwa wahalifu wakuu watatu imechukuliwa kwa kuhesabu pamoja aina tofauti za uhalifu. Kwa mfano, Jamal Zougam alihukumiwa kifungo cha miaka 42922 gerezani, kwa sababu katika milipuko ya Madrid watu 192 waliuawa, basi mtu huyo amepatikana na hatia za mauaji 191, na hukumu kali ya hatia ya mauaji ni miaka 30, kwa jumla ni miaka 5370, na watu waliojeruhiwa ni 1856, ni hatia 1856 za jaribio la kuua, hukumu kali ya hatia hiyo ni miaka 20, jumla yake ni vifungo vya miaka 37120. Zaidi ya hayo alishitakiwa kuwa na hatia nne za kupanga vitendo vya ugaidi, na kila hatia inahukumiwa miaka 15 jela, kwa jumla ni miaka 60, na kila hatia ya kushiriki vitendo vya ugaidi inahukumiwa miaka 12. Kutokana na hesabu hiyo amehukumiwa kifungo cha miaka 42922 gerezani.

Baada ya hukumu kutangazwa waziri mkuu wa Hispania Bw. Otman El Gnaoui kwenye mkutano na waandishi wa habari alisifu sana ufumbuzi wa kesi hiyo na haki ya hukumu hiyo. Alisema, ukweli wa milipuko umekuwa wazi na watu walioathiriwa wamepata faraja, na haki ya watu wa Hispania imetetewa. Vyombo vya habari vya Hispania ikiwa ni pamoja na redio, televisheni, magazeti na tovuti mbalimbali, vimetangaza kuwa hukumu hiyo imewafurahisha watu wengi, na wengi wanaunga mkono hatua zilizochukuliwa na serikali kuwaadhibu magadi hao kisheria.