Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-01 18:53:26    
Mke na mume wanaosimamia kituo cha mabasi mjini Beijing

cri

Katika vituo vya mabasi vilivyoko katikati ya mji wa Beijing, kuna watu wanaovaa kofia nyekundu na fulana za rangi ya malai, na wanaoshika vibendera. Wao ni wasimamizi wa vituo vya mabasi, ambao kazi yao ni kuyaelekeza mabasi yanapoingia vituoni, kusimamia utararibu vituoni, kusafisha vituo hivyo na kuwasaidia abiria.

Katika kituo kimoja cha mabasi kwenye mtaa wa Yaojiayuan mjini Beijing, wasimamizi wa kituo hicho ni mke na mume, Bibi Han Xiuling na Bw. Dong Qizhao.

Asubuhi, mke na mume hao wanaondoka nyumbani kwao kabla ya saa 11. Wakifika kwenye kituo cha mabasi, kwanza wanasafisha kituo, huku Bw. Dong Qizhao akiwataka abiria washiriki pamoja katika kuhifadhi usafi wa kituo cha mabasi, akisema,

"Hamjambo abiria. Ili kulinda afya zenu, tafadhali msiteme mate ovyo sakafuni wala msiache takataka. Asanteni."

Kutokana na jitihada za Bibi Han Xiuling na Bw. Dong Qizhao, sura ya kituo hicho cha mabasi imeboreshwa sana, ambapo hivi sasa takataka zikiwemo vikaratasi na vichungi vya sigara havionekani, na kuna utaratibu mzuri. Toka siku ya kwanza tangu mke na mume hao waanze kufanya kazi kwenye kituo hicho cha mabasi, wamekuwa wakiendelea kuwashawishi abiria wajipange kwenye mstari wanaposubiri wakati wa kupanda mabasi. Zaidi ya hayo Bw. Dong anawaelimisha abiria manufaa ya kujipanga kwenye mstari.

"Manufaa ya kwanza ni kwa wazee, wagonjwa, walemavu na wajawazito. Hili ni suala la kwanza, si ndiyo? Na suala la pili ni kwamba, tukijipanga kwenye mstari na kupanda mabasi mmoja baada ya mwingine, ni vigumu kwa wezi kuiba mali zetu."

Kutokana na ushawishi, watu wengi kabisa wanajipanga kwenye mstari kwa hiari. Kwa hiyo hata kama kituoni kuna watu wengi, utaratibu haupotei, na wazee na watoto wanapewa kipaumbele kinachostahili.

Watu karibu elfu moja wanapita kwenye kituo hicho kidogo cha mabasi kila siku. Si ajabu kutokea kwa matatizo. Lakini mke na mume wanaondoa matatizo mbalimbali kwa uvulimivu mkubwa. Bibi Han Xiuling alieleza tukio moja lililotokea hivi karibuni.

"Siku moja alikuja kijana akiwa kifua wazi, alikuwa amebeba begi mkononi na uso wake ulikuwa mwekundu. Nilimwuliza, kwa nini hujavaa nguo kwenye sehemu ya juu ya mwili? Alijibu ni kwa sababu ya joto kali. Nilimwambia angalia barabarani kuna watu wanaovaa kama wewe? Tunapaswa kuwa na vitendo vya ustaarabu, kuna kauli isemayo 'panda mabasi kwa ustaarabu, mimi natangulia kufanya hivyo', si ndiyo? Basi kijana huyo alisema, mama, basi linakuja, navaa."

Kushughulikia matukio madogo madogo kama hilo ni kazi wanayofanya mke na mume hao kila siku. Bibi Han Xiuling ana kisanduku cha dawa chenye dawa za kupunguza joto, anakwenda nacho kwenye kituo cha mabasi. Alisema aliweka dawa hizo kutokana na hali ya joto kali kwa siku za hivi karibuni, na siku chache zilizopita, alizitumia dawa hizo kumsaidia kijana aliyepata joto kali.

Kazi hodari ya mke na mume hao inatambuliwa na abiria, ambao mmoja wao anasema, (sauti 4) "Huyu mama ni hodari katika kusimamia utaratibu. Nimepita vituo mbalimbali vya mabasi, naona kituo hicho ni kizuri, hiki ni kituo safi na chenye utaratibu mzuri."

Bw. Liu anayefanya kazi karibu na kituo hicho cha mabasi anapitia kwenye kituo hicho kila siku. Alitoa maoni kuhusu kazi ya mke na mume hao. Akisema "Wanatekeleza majukumu yao kwa ustaarabu. Ukiwauliza njia, hakuna njia wasiyofahamu. Wao ni kama ramani ya Beijing, abiria wanaridhishwa na kazi yao."

Mbali na kusimamia kituo cha mabasi, Bibi Han Xiuling na Bw. Dong Qizhao wameteuliwa na kampuni ya mawasiliano na uchukuzi wa umma ya Beijing kuwa wasimamizi wa kazi za madereva na makondakta, ili kuinua kiwango cha huduma zao.

Bibi Han Xiuling alisema "Tunapotumia mabasi, tunasimamia kazi za madereva na makondakta, kama wanafanya kazi kwa ustaarabu au la, na wanaegesha mabasi kwa kufuata kanuni au la. Na makondakta wanapotangaza majina ya vituo na kuongea, tunafuatilia kama wanaweza kutumia lugha kwa ustaarabu au la. Mimi ni msimamizi, natoa ripoti kuhusu wale wasiofuata kanuni."

Katika muda wa zaidi ya mwaka mmoja tangu mke na mume hao waanze kufanya kazi hiyo, wamekuwa wakijulikana miongoni mwa abiria kutokana na uhodari wao katika kazi, pia wanapewa sifa mbalimbali na serikali ya mji wa Beijing. Wao wanathamini sifa hizo na kazi hiyo ya kawaida. Bibi Han Xiuling alisema "Inapaswa kufanya kazi kwa bidii na kufanya kazi kwa uhodari, ama sivyo usifanye kazi hiyo. Mtoto wangu aliniambia kuwa, mama unapaswa kufanya kazi vizuri zaidi."

Hapa mjini Beijing kuna wasimamizi zaidi ya elfu 4 kama Bibi Han Xiuling na Bw. Dong Qizhao, wao wanasimamia vituo vya mabasi 1,805. Bila kujali joto kali au baridi kali, wanachapa kazi kwa ajili ya uendeshaji mzuri wa mawasiliano ya umma barabarani mjini Beijing.