Mkutano wa nishati wa Umoja wa Ulaya, Afrika na Mashariki ya Kati ulifunguliwa tarehe mosi huko Sharm el-Sheik, nchini Misri. Mkutano huo ulitoa taarifa ikisisitiza kuwa, pande mbalimbali zinatakiwa kuimarisha ushirikiano na mazungumzo katika mambo ya nishati. Mawaziri, maofisa waandamizi, na wajumbe kutoka nchi 68 walihudhuria mkutano huo. Mada muhimu za mkutano huo zilikuwa ni pamoja na kuimarisha usalama wa nishati, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, kuzalisha na kutumia nishati endelevu, kurahisisha uwekezaji katika mambo ya nishati, kuboresha miundo mbinu ya nishati, kuendeleza teknolojia ya kuzalisha nishati zisizosababisha uchafuzi, na kutoa nishati yenye usalama ambayo inaweza kupatikana kwa urahisi na kutumiwa kwa muda mrefu.
Kwanza mkutano huo ulisisitiza kuwa ni lazima nchi hizo ziimarishe mazungumzo kuhusu nishati kwenye msingi wa ushirikiano, ili kuhakikisha usalama wa nishati, kusukuma mbele maendeleo ya uchumi, na kutimiza maslahi ya pamoja. Taarifa iliyotolewa na mkutano huo ilisisitiza kuwa, ni lazima nchi zinazozalisha nishati, nchi zinazotumia nishati na nchi zinazosafirisha nishati ziendelee kufanya mazungumzo, na kukabiliana na changamoto kwa pamoja kupitia ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya, baraza la ushirikiano la nchi za Ghuba, nchi za Afrika ya Kaskazini zilizoko kando ya Bahari ya Mediterranean na nchi nyingine za Afrika.
Kwenye ufunguzi wa mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Misri Bw. Ahmed Abul Gheit alitoa hotuba akisisitiza kuwa, suala la nishati lenye utatanishi mkubwa limekuwa ni changamoto kwa dunia nzima, na lina athari kubwa zaidi kwenye mambo ya siasa na mikakati ya kijeshi duniani. Alisema kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika mambo ya nishati, ni kazi muhimu ambayo itatoa uhakikisho wa kuwepo kwa nishati kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Mjumbe anayeshughulia mambo ya nje na sera za ujirani mwema wa Umoja wa Ulaya Bibi Benito Ferrero-waldner alisema, kamati ya Umoja wa Ulaya imedhamira kupanua uhusiano kati yake na wenzi wake katika mambo ya nishati, na Umoja wa Ulaya unalenga kuchukua hatua kadhaa ambazo pande husika zinaweza kushiriki, ili kuhakikisha usalama wa nishati wa sehemu zote zinazohusika. Mjumbe anayeshughulikia mambo ya nishati Bw. Andris Piebalgs pia alisema, Umoja wa Ulaya utaimarisha ushirikiano na nchi za Mashariki ya Kati na Afrika, ili kuhakikisha usalama wa utoaji wa nishati.
Pili, mkutano huo ulitoa mwito kuzitaka nchi hizo ziimarishe ushirikiano kuhusu nishati endelevu na nishati zisizosababisha uchafuzi. Kwa upande mmoja, Asia ya Magharibi, Afrika ya Kaskazini na nchi nyingine kadhaa ikiwemo Nigeria ni nchi na sehemu zinazozalisha mafuta na gesi ya asili kwa wingi. Umoja wa Ulaya, nchi za Mashariki ya Kati na nchi za Afrika zinapanua ushirikiano kwa kuyaruhusu makampuni ya nchi za nje yashiriki kwenye kazi za kuchimba nishati, kujenga viwanda vya kuzalisha mafuta na gesi ya asili, na kujenga mabomba ya kusafirisha mafuta na gesi ya asili. Na kwa upande mwingine, mustakabali wa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya, Mashariki ya Kati na nchi za Afrika katika uzalishaji wa nishati endelevu na nishati zisizosababisha uchafuzi ni mzuri.
Tatu, kutumia nishati ya nyukilia kwa amani ni suala lililofuatiliwa na wajumbe wengi kwenye mkutano huo. Waziri wa mambo ya nje wa Misri Bw. Ahmed abul Gheit alisisitiza kuwa, tarehe 29 mwezi Oktoba Rais Hosni Mubarak wa Misri alitoa uamuzi wa kimkakati kuhusu kujenga vituo kadhaa vya kuzalisha umeme kwa nishati ya nyukilia kutokana na ushirikiano kati ya Misri na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki. Tarehe mosi Mwezi Novemba Jordan ilitangaza kuwa, Umoja wa Ulaya na Jordan zilisaini taarifa ya pamoja ya kazi muhimu za ushirikiano wa nishati mjini Sharm el-Sheik.
|