Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-05 14:23:07    
Moja ya mbinu 36: Kumkamata mwizi baada ya kufunga mlango

cri

"Kumkamata mwizi baada ya kufunga mlango" ni usemi ulioenea miongoni mwa Wachina, usemi huo ni kama usemi wa "Kumpiga mbwa baada ya kufunga mlango", maana ya usemi huo ni kumvutia mwizi aingie kwenye sehemu unayodhibiti na kumkamata. Baadaye watu waliutumia ujanja huo katika mbinu za vita. Katika mambo ya vita mbinu hiyo ni kama vita vya kuzingira maadui kwa pande zote na vita vya kupambana na maadui baada ya kuwavutia ndani ya mtego. Katika zama za kale na zama hizi mbinu hiyo inatumika sana katika vita. Kuhusu mbinu hiyo kitabu cha "Mbinu 36 za Kivita" kinaeleza hivi: "Kumkamata mwizi baada ya kufunga mlango" siyo kwa ajili ya kumzuia tu mwizi asitoroke, bali pia ni kwa ajili ya kutompatia nafasi ya kujiimarisha baada ya kutoroka. Kama mlango haukufungwa kabisa na maadui wakitoroka, basi haifai wewe kuwakimbiza iwapo huna uhakika wa kuwakamata, ili usije ukaingia kwenye mtego uliotayarishwa na maadui. Ufuatano ni mfano wa matumizi ya mbinu hiyo katika vita vya kale nchini China.

Mwaka 880 kiongozi wa waasi wa wakulima Huang Chao aliongoza jeshi lake kuushambulia mji mkuu wa Enzi ya Tang ulioitwa Chang An, mfalme alikimbia haraka na kukusanya askari kupambana tena na jesi la Huang Chao. Baada ya kupambana kwa muda wa mwaka mmoja hivi jeshi la mfalme lilikuwa na nguvu kubwa zaidi na kuukaribia mji wa Chang An.

Huang Chao aliona amezidiwa nguvu na jeshi la mfalme, na angekuwa hatarini kama angeendelea kuukalia mji huo, aliamua kuondoa jeshi lake kutoka kwenye mji huo.

Jeshi la mfalme liliuzingira na kuushambulia mji wa Chang An lakini halikupata upinzani wa jeshi la Huang Chao, jeshi hilo lilistaajabu. Baada ya kuingia mjini liligundua kwamba kumbe jeshi la Huang Chao lilikuwa limeondoka kabisa. Mfalme aliurudisha mji huo chini yake bila mapambano, na majemadari na askari wote walifurahi sana, nidhamu ya kijeshi ikapungua, majemadari na askari walizama katika dimbwi la furaha, kila siku walikuwa wanakunywa pombe bila kuwa na tahadhari ya kujilinda.

Huang Chao alituma mtu kwenda mjini Chang An ili kupeleleza habari, kisha alisema kwa furaha: sasa maadui wameingia mtungini. Katika usiku wa manane aliamrisha askari wake waushambulie mji wa Chang An. Kutokana na kuwa askari wa mfalme hawakujiandaa, wengi waliuawa. Kwa kutumia mbinu ya "Kukamata mwizi baada ya kufunga mlango" Huang Chao aliuteka tena mji wa Chang An.

"Kukamata mwizi baada ya kufunga mlango" ni mbinu ya kuwazingira maadui wenye nguvu dhaifu kwa pande zote na kuwaangamiza, lakini kama maadui wakibahatika kukimbia hali itakuwa mbaya, kwa sababu ukiwafukuza bila kuwaacha pengine watapambana nawe kufa na kupona, na vile vile pengine utaingia ndani ya mtego waliokutegea. Kwa hiyo ni vizuri usiwaache "wezi" wakimbie, bali ukate njia yao ya nyuma na kukusanya nguvu zako kuwaangamiza. Ukiweza kutumia vizuri mbinu hiyo pia unaweza kuwaangamiza maadui wanaokuzidi kwa nguvu, lakini cha muhimu ni kupanga vizuri askari wako kuwazingira maadui na kuacha mlango wazi ili kuwavutia waingie ndani.

Katika jamii ya sasa mbinu hiyo ya "kukamata mwizi baada ya kufunga mlango" pia inatumika katika mambo ya biashara na fedha. Katika soko la hisa, kutokana na kuwa na uhakika sahihi juu ya hali ya soko la hisa baadhi ya watu wanaonunua na kuuza hisa wanaacha faida kwa muda na kusubiri faida ya muda mrefu, bei ya hisa inapopanda na kufikia kileleni mara wanauza hiza zao. Katika ushindani wa kibiashara, pande mbili zinashindana kiakili, fursa nzuri inapofika tu mara upande mmoja unanunua shughuli zote za upande wa pili, hii pia ni njia ya mkato ya kujitajirisha.