Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-05 18:34:21    
Hekalu la Wanshou na jumba la makumbusho la sanaa la Beijing

cri

Kwenye sehemu ya magharibi ya mji wa Beijing kuna hekalu moja la kale linaloitwa hekalu la Wanshou, ambalo lilijengwa miaka 430 iliyopita. Hekalu hilo liliwahi kuwa mahali pa kufanya sherehe na kupumzika kwa wafalme wa enzi za Ming na Qing, hivyo hekalu hilo pia linaitwa kuwa ni "Jumba dogo la wafalme la zamani". Hekalu hilo limehifadhi vitu vya sanaa zaidi ya elfu 70, vikiwemo vya maandiko, michoro, kazi za tarizi na kauri, watalii wengi wa nchini na wa nchi za nje wanavutiwa kwenda huko kuangalia hekalu hilo.

Mtaalamu kuhusu mambo ya hekalu la Wanshou, Bw. Kong Xiangli amefanya uchunguzi na utafiti kwa karibu miaka 20, alieleza kuhusu chanzo cha hekalu hili, akisema,

"Hekalu la Wanshou lilijengwa mwaka 1577. Ujenzi wa hekalu ulihusiana sana na ukoo wa mfalme. Katika kipindi cha utawala wa mfalme Wan Li, mama wa mfalme alikuwa muumini wa dini ya kibudha. Wakati ule, ukoo wa mfalme ulikuwa na jengo la kuhifadhia misahafu ya dini ya kibudha, lakini lilichakaa, na lilitakiwa kufanyiwa matengenezo. Mama wa mfalme Wan Li alieleza wazo lake la kujenga hekalu badala la lile jengo la kuwekea vitabu vya dini ya kibudha. Hatimaye yeye mwenyewe alitoa fedha zake kwa ajili ya ujenzi wa hekalu hilo, baada ya ujenzi kukamilishwa, vitabu vya dini ya kibudha vilihamishwa kwenye hekalu la Wanshou."

Bw. Kong Xiangli alisema, hapo baadaye hekalu la Wanshou lilifanyiwa matengenezo mara kadha, hatimaye likawa kundi kubwa la majengo ya ukoo wa mfalme yakiwa ni pamoja na ya hekalu, nyumba ya kuishi pamoja na bustani. Hivi sasa, watalii wanatembezwa kwenye hekalu la Wanshou kwa kufuata njia ya mashariki na njia ya magharibi, kwenye njia ya mashariki, kuna nyumba zenye nyua za kuishi kwa watawa wa hekalu, ambazo ni nyumba rahisi sana zinazoendana na imani yao ya kujizuia kufanya mambo ya anasa; Kwenye njia ya magharibi, kuna jengo la kuishi watu wa ukoo wa mfalme, majengo hayo ni ya fahari sana na yanaonesha ukuu wa kifalme. Mwelezaji wa watalii kwenye hekalu la Wanshou, Bibi Sun Qiuxia alisema, hekalu la Wanshou lilikuwa hekalu la kifalme, ambalo lilipokea watu wa ukoo wa mfalme tu na kufanya sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mfalme, na lilifunguliwa kwa siku kumi na kidogo tu kwa mwaka kwa watu wa kawaida.

"Hekalu la Wanshou lilikuwa hekalu muhimu la kifalme katika enzi mbili za Ming na Qing. Likiwa hekalu la kifalme, katika siku za kawaida ni wale maofisa wakubwa tu, ambao waliruhusiwa kwenda kuchoma udi na kufanya sala, isipokuwa katika siku za kuzaliwa kwa mabudha, watu wa kawaida waliruhusiwa kwenda kuwaabudu.

Jengo la Daxiongbaodian lililoko kwenye sehemu ya mbele ya hekalu ni jengo kubwa zaidi kwenye hekalu la Wanshou. Mbele ya jengo hilo kuna mawe mawili yaliyochongwa maneno ya shairi lililotungwa na mfalme wa Qianlong kwa ajili ya kutimiza miaka 100 tangu mama yake azaliwe. Ndani ya jengo hilo kuna sanamu moja budha ya shaba nyeusi ya enzi ya Ming. Chini ya sanamu hiyo kuna ua la yungiyungi, ambalo kwenye kila kichane chake ilichongwa picha ya Sakyamuni, na jumla yake ni elfu moja. Kama ukiendelea kwenda sehemu ya nyuma ya hekalu kutoka kwenye jengo la Daxiongbaodian, kuna milima mitatu ya mandhari iliyotengenezwa na binadamu wakati lilipojengwa hekalu. Juu ya milima kuna majengo, milima hiyo inatengwa na mabonde na kuunganishwa kwa madaraja ya mawe. Kwenye milima hiyo ya mandhari, imeota miti mingi ya misonobari na mivinje, kati yake kuna miti miwili ya ginkgo, ambayo ina zaidi ya miaka 300 iliyopita. Mtalii Bibi Chen Huilin kutoka mkoa wa Taiwan, aliyetembelea kwa mara ya kwanza hekalu la Wanshou, alisema,.

"sikutarajia kama ua wake ni mkubwa hivyo, kitu kizuri cha hapa ni ukimya, sehemu ya nje ni majengo mengi marefu, lakini humu ndani ni mazingira yasiyo na kelele. Inasemekana hapa panaitwa "Majengo ya mfalme ya zamani", hapa nimeona mambo ya historia."

Hivi sasa, hekalu la Wanshou limerekebishwa kuwa jumba la makumbusho la sanaa la Beijing lenye eneo la mita za mraba zaidi ya elfu 30, ndani yake vinaoneshwa vitu vya sanaa vya dini ya kibudha vya enzi za Ming na Qing, maonesho ya sanaa ya kauri, maonesho ya sanaa ya kazi za mikono na maonesho ya sanaa ya uchoraji ya enzi za Ming na Qing. Jumla kuna vitu vya sanaa zaidi ya elfu 70 kuhusu sanaa ya maandiko, uchoraji, ufumaji na utarizi, vyungu na vyombo vya kauri na samani. Maonesho yanayopendeza zaidi ni maonesho ya vyombo vya kauri. Mwelezaji wa maonesho, Bibi Sun Qiuxia alisema,

"Vyombo vya kauri ni vitu vyenye umaalumu zaidi katika jumba letu la makumbusho, ambavyo vinaonesha umaalumu wa vyombo vya kauri vya enzi za Ming na Qing. Kwa mfano, hiyo sahani lenye rangi ya pinki na umbo la tunda la pichi, rangi zake zinabadilika kuwa nyepesi kutoka rangi nzito, na kufanana na sanaa ya michoro ya kichina. Taswira iliyoko katika ya sahani na taswira iliyoko kwenye sehemu ya nje ya sahani zinaungana na kuonesha maana ya furaha na maisha marefu."

Mbali na hayo, maonesho ya sanaa ya dini ya kibudha ya enzi za Ming na Qing yaliyofanyika katika jumba la makumbusho la sanaa la Beijing, pia ni maonesho maalumu. Zaidi ya vitu 80 vya dini ya kibudha vya enzi za Ming na Qing vilivyooneshwa kwenye maonesho ya vitu vya sanaa vya dini ya kibudha, vinahusu sanamu za budha na Arhat, pamoja na vyombo vinavyotumika katika sala za dini ya kibudha, sanamu za budha ni zenye maumbo mbalimbali, sura zao na mavazi yao yalitengenezwa kwa ustadi mkubwa na zinaonekana kama za kweli kabisa, vitu hivyo vimehifadhiwa vizuri vikiwa kama vitu adimu vya dini ya kibudha. Maonesho ya vitu vya sanaa vya enzi za Ming na Qing ni pamoja na vitu vya aina mbalimbali vinavyopendeza vya kuwekwa chumbani kama mapambo, vitu hivyo vilitengenezwa kwa ufundi mkubwa, ni vitu vinavyotumika katika maisha ya watu.