Tafrija ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu Mkutano wa wakuu wa Beijing wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ufanyike, ilifanyika tarehe 4 usiku hapa Beijing, ambapo mjumbe wa taifa wa China Bwana Tang Jiaxuan, na mabalozi wa nchi za Afrika nchini China wapatao 200 walihudhuria tafrija hiyo.
Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika tarehe 4 Novemba, mwaka 2006 hapa Beijing, ambapo wakuu wa nchi na serikali pamoja na wajumbe wa nchi 48 walihudhuria Mkutano huo. Mkutano huo ulipitisha "Taarifa ya mkutano wa Beijing wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika" ukikubali kwa kauli moja kuanzisha na kuendeleza uhusiano wa aina mpya wa kimkakati na kiwenzi kati ya China na Afrika ulio wa usawa na uaminifu wa kisiasa, ushirikiano wa kunufaishana kwenye mambo ya kiuchumi, kufanya maingiliano na kufundishana katika mambo ya kiutamaduni. Rais Hu Jintao wa China akiiwakilisha serikali ya China alitangaza hatua 8 za kuimarisha ushirikiano halisi kati ya China na Afrika na kuzisaidia nchi za Afrika kujiendeleza.
Katika mwaka mmoja uliopita, kazi za kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kwenye Mkutano huo zimeanzishwa na kuendelea vizuri, ambapo uhusiano wa kisiasa kati ya China na Afrika unaendelezwa kwa kina, ushirikiano halisi unaimarishwa kwa pande zote, hali mpya ya mshikamano imeonekana na ushirikiano kati ya pande mbili za China na Afrika umekuwa barabara zaidi. Kwenye tafrija hiyo, mjumbe wa taifa wa China Bwana Tang Jiaxuan alisema:
"China inafanya juhudi kubwa kutekeleza hatua 8 ikiongeza misaada kwa maendeleo ya Afrika; hatua za kusamehe madeni na kufuta ushuru wa forodha zinakaribia kukamilika; ujenzi wa kituo cha Mkutano wa Umoja wa Afrika umewekewa jiwe la msingi; Mfuko wa maendeleo ya China na Afrika umeanzishwa vizuri; na kazi za kujenga hospitali, vituo vya vielelezo vya ufundi wa kilimo, na shule za vijijini barani Afrika zinafanyika kwa haraka".
Kutoa misaada ya kilimo ni moja kati ya hatua 8 za misaada ilizoahidi China kwa Afrika. China iliahidi kujenga vituo 10 vyenye umaalum vya vielelezo vya ufundi wa kilimo barani Afrika, na kuwatuma wataalamu 100 wa ufundi wa kilimo kwenda kwenye nchi za Afrika. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, China imetuma vikundi vitano kwenda kwenye nchi 14 za Afrika kufanya ukaguzi kuhusu ujenzi wa vituo vya vielelezo vya ufundi wa kilimo, na miradi mbalimbali inayohusika inaanza kutekelezwa kwa mfululizo. Hivi karibuni kituo cha vielelezo vya ufundi wa kilimo kilichojengwa kwa msaada wa China kimezunduliwa nchini Msumbiji.
Mwezi Februari mwaka huu Kituo cha kwanza cha kinga na tiba ya ugonjwa wa malaria kilichojengwa kwa msaada wa China kilizinduliwa nchini Liberia. Na kabla ya mwishoni mwa mwaka huu, China itazisaidia nchi 10 za Afrika kuanzisha vituo vya kinga na tiba ya ugonjwa wa malaria, ambapo wataalamu 60 wa China watakwenda kwenye nchi za Afrika kushiriki kwenye kazi ya kuwaandaa madaktari. Aidha, mwaka huu China imezisaidia nchi za Afrika kuwaandaa watu wa sekta mbalimbali wapatao zaidi ya 4000. Maendeleo makubwa mapya yamepatikana katika ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye mambo ya fedha, sayansi na teknolojia na safari za ndege. Bw. Tang Jiaxuan alisema:
"China itashirikiana na nchi za Afrika katika kutekeleza vizuri makubaliano ya Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, na kutekeleza hatua 8 ilizoahidi China".
Kiongozi wa kundi na mabalozi wa nchi za Afrika nchini China ambaye pia ni balozi wa Cameron nchini China Bwana Eleih Elle Etian alipotoa hotuba kwenye tafrija hiyo, pia alisifu mafanikio mengi yaliyopatikana kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika uliofanyika Beijing. Alisema huu ulikuwa Mkutano wa uvumbuzi, Mkutano huo wa kihistoria umeweka msingi mpya kwa ajili ya ushirikiano kati ya China na nchi rafiki za Afrika. Nchi za Afrika zinapenda kushirikiana na China kwa moyo wote, ili kujitahidi pamoja kuinua uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye kiwango kipya. Alisema:
"Utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano huo, umepata maendeleo katika mambo mengi mbalimbali. Tuna matumaini makubwa zaidi kuhusu ushirikiano wa kunufaishana kati yetu katika siku za usoni".
|